NA SHARON SAUWA
28th April 2013
Vikao kati ya Bunge, Serikali vyahamia Dar kutafuta fedha za nyongeza ya bajeti
Kwa matiki hiyo, wizara ya Profesa Jumanne Maghembe bado inahaha kupata fedha za kuziba pengo linalotakiwa kutosheleza fungu la matumizi ya wizara yake.
Uamuzi huo uliotolewa Alhamis wiki iliyopita na Spika Makinda, uliitaka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Kamati ndogo ya bajeti, na Wizara ya Fedha kufanya marekebisho na kisha kuileta bungeni Jumatatu (kesho).
Hatua hiyo inafuatia baada ya wabunge karibu wote wa vyama vya upinzani na tawala kugoma kupitisha bajeti hiyo hadi serikali itakapoongeza bajeti ya Wizara ya Maji.
Habari kutoka ndani ya kamati hizo, zilisema hadi kufikia jana hakukuwa na muafaka uliofikiwa na kwamba kamati ndogo ya bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, (CCM) , Wizara ya Fedha pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wamelazimika kuhamishia kikao Dar es Salaam.
Hatua hiyo imekuja baada ya kushindwa kufikiwa kwa muafaka wa kuongeza shilingi bilioni 187 katika bajeti ya maji iliyotakiwa kuongezwa na Kamati ya Bunge .
Chanzo hicho kimesema Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, imebaki mjini Dodoma ikisubiri majibu ya kamati ndogo ya bajeti na Wizara ya Afya.
Bajeti ya Wizara hiyo ilikwama baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kutoa mwongozo wa kuahirisha mjadala huo baada ya Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) kuomba mwongozo wa Spika.
Katika mwongozo wake, Mwigulu aliomba kiti cha Spika kuiondoa hoja hiyo ili wizara ikutane na Kamati ya Bajeti kuifanyia marekebisho.
Hata hivyo, uamuzi huo ulikuwa ufikiwe mapema kama Waziri Mkuu Mizengo Pinda angekubali wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka hoja hiyo iondolewe ili ikafanyiwe marekebisho.
Mbowe Katika swali lake kwa Pinda wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, aliitaka serikali kuiondoa hoja hiyo kutokana na mwelekeo wa mjadala huo kuonyesha kuwa wabunge wengi hawaiungi mkono.
Katika mwaka huu wa fedha, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliomba Bunge kuidhinisha Sh bilioni 398 kwa ajili ya matumizi ya Wizara hiyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment