Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, April 27, 2013

Rais Kikwete aongoza maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano

Na Salum Vuai, Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, leo aliwaongoza maelfu ya Watanzania katika sherehe za maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Sherehe hizo zilifanyika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wote wa kitaifa nchini, mawaziri wa Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar, viongozi wa ngazi zote na watendaji wakuu pamoja na wananchi mbalimbali.
Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal, na Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Peter Pinda.
Wengine ni Marais wastaafu wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume, Mawaziri Wakuu wastaafu Fredrick, Sumaye, Edward Lowasa na John Malecela, Spika wa Bunge Anne Makinda na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho na viongozi wengine.
Pamoja na mvua ya wastani iliyokuwa ikinyesha mapema asubuhi, wananchi mbalimbali walijitokeza kwa wingi uwanjanihapo kusherehekea Muungano huo wa kihistoria ulioziunganisha nchi za Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, mwaka 1964.
Shamrashamra mbalimbali zilipamba sherehe hizo, likiwemo gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama, halaiki ya muungano wa wanafunzi kutoka Zanzibar na Bara, ngoma za asili, Sindimba kutoka mkoani Lindi, Gonga-Kusini Pemba na Nyaketari kutoka Tarime, Mara.
Aidha, kikosi cha kwaya cha JKT Msange kutoka mkoa wa Tabora, nacho kilishuka uwanjani kuhitimisha maadhimisho hayo, ambapo kilitia fora kutokana na manjonjo ya kiongozi wake aliyekuwa kivutio kikubwa uwanjani hapo.
Mapema baada ya kuwasili uwanjani hapo, Rais Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, alipigiwa mizinga 21 na kukagua vikosi vya gwaride, kabla kupokea saluti ya utii kwa Rais.
Baada ya hapo, vikosi mbalimbali vya gwaride vilipita mbele ya mgeni rasmi na waalikwa wengine, kwa mwendo wa polepole na ule wa haraka, huku vikishangiriwa kwa nguvu na wananchi waliovutiwa na ukakamavu wa wapiganaji hao.
Kwa upande wao, vijana wa halaiki walinogesha sherehe hizo kwa kuonesha sura nne za maonesho, ambayo ni ulinzi, uchumi, afya na utamaduni, na kumalizia kwa sarakasi iliyowafurahisha wageni na wananchi wote waliohudhuria sherehe hizo.
Miongoni mwa maumbo waliyotengeneza na kufurahisha umma, ni maandishi yaliyosomeka “Miaka 49 ya Muungano”, pamoja na “Tusichanganye Kiswahili na Lugha nyengine”.
Tukio jengine lililosisimua hadhira uwanjani hapo, ni maonesho ya ndege za kivita za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), zilizoruka katika anga ya uwanja huo, huku zikitoa moshi wenye ishara ya bendera ya Taifa.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliasisiwa Aprili 26, 1964 kutokana na makubaliano ya Rais wa kwanza wa Tanganyika Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyeyere, na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Amani Karume.
Sherehe za mwaka huu zinabebwa na kaulimbiu isemayo, “Amani, utulivu na maendeleo ni matokeo ya muungano wetu, tuulinde na kuutunza.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments :

Post a Comment