Na Rashid Yussuf Mchenga
Aprili 27 2013 saa 1:17 AM
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa mfano duniani. Ni dola mbili huru zilizoungana na kuunda nchi moja yenye serikali mbili.
Tanganyika ilipata uhuru wake Desemba 9/1961 na ikapata kiti chake katika Umoja wa Mataifa Desemba 14, 1961. Namba ya kiti hicho ni ‘GA resolution 1667 (XVI).’ Zanzibar nayo ikapata uhuru wake Desemba 10, 1963 na ikapata kiti chake katika Umoja wa Mataifa Desemba 16, 1963; namba ya kiti hicho ni ‘GA resolution 1975 (XIII).’
Ilipofika Aprili 26, 1964, mataifa hayo mawili huru yaliungana na hapo ndipo ilipozaliwa nchi iliyojulikana kwa jina la Tanzania.
Novemba 2, 1964 kupitia Wizara wa Mambo ya Nchi za Nje ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliuandikia barua Umoja wa Mataifa na kutaka Zanzibar na Tanganyika ziondoshwe katika orodha ya mataifa na iingizwe nchi inayojulikana kwa jina la Tanzania.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni sawa na muungano wa Siria na Misri walioungana mwaka 1958 na ni sawa na muungano wa Yemen ya Kaskazini na Yemen ya Kusini walioungana mwaka 1990. Kwa bahati mbaya muungano wa Siria na Misri ulivunjwa mwaka 1961 (ulidumu kwa miaka 3).
Kwa sasa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umefikia hatua nzuri na ya kupigiwa mfano duniani kwa sababu umedumu kwa miaka 49 sasa.
Hata hivyo pamoja na kuwa muungano huu una muundo wa kipekee na kuwa umedumu kuliko miungano mingi iliyowahi kuwapo Afrika.
Muungano wa kwanza ulikuwa ni ule wa nchi za Afrika Magharibi, mwishoni mwa miaka ya 50 na mwanzoni mwa miaka ya 60, ulioanza na nchi mbili Ghana na Guinea na baadaye Mali ikajiunga nao. Muungano huu ulitokana na vuguvugu la umajimui wa Afrika (Pan Africanism), vinara wake wakiwa Kwame Nkrumah wa Ghana, Sekou Toure wa Guinea na Modibo Keita wa Mali.
Novemba 1958 uliundwa muungano wa Ghana na Guinea mara baada ya mkutano wa watu wa Afrika (All- African Peoples’ Conference). Ghana ilitoa fedha nyingi na kuipa Guinea ili ijitoe haraka kutoka katika utegemezi wa Ufaransa.
Mei 1959 ikatangazwa kuwa umoja huo utatambulika kama Umoja wa Dola za Kiafrika.
Ilipofika Aprili 1961, Mali nayo ilijiunga na umoja huo. Muungano huo ulivunjika mwaka 1962 kutokana na vita baridi, ambapo Guinea ilionekana ikiinyooshea mikono Marekani wakati wenzake walikuwa wakifuata mrengo wa kushoto wa Karl Marx/Lenin
Muungano mwingine wa nchi za Afrika ulifanyika mwaka 1981 baina ya nchi za Senegal na Gambia, uliojulikana kama Senegambia ambao ulikufa mwaka 1989.
Muungano mwingine wa nchi za Afrika ulifanyika mwaka 1981 baina ya nchi za Senegal na Gambia, uliojulikana kama Senegambia ambao ulikufa mwaka 1989.
Pamoja na kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa kupigiwa mfano, lakini bado si vyema kuacha kusema kuwa una matatizo.
Tatizo kubwa la muungano huu ni ile hali ya upande mmoja kujiona kama unabinywa na upande mwingine wa muungano, nadharia iliyozoeleka ni ‘samaki mkubwa kummeza mdogo.’ Tatizo hilo lilisababisha baadhi ya Wazanzibar kulalamika na kumi katika hao walijitokeza na kwenda mahakamani kudai Hati ya Muungano. Jibu walilopata ni kuwa hakuna Hati ya Muungano (Mkataba).
Mwanasheriaa Mkuu wa Zanzibar alisema hakuna Mkataba wa Muungano kwa kuwa suala la muungano ni kama ardhi kwa sababu muungano ni wa nchi na nchi ni sawa na kuunganisha sehemu mbili za ardhi suala ambalo kisheria linaweza kuhojiwa ndani ya miaka kumi na mbili (12), baada ya hapo huwezi kuhoji, kwa maana hiyo ni halali kwa mujibu wa sheria ukizingatia waliohoji walifanya hivyo mwaka 2004 sawa na miaka 40 tokea nchi ziungane.
Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar umekumbwa na misukosuko mingi ambayo ndiyo hii inayoitwa kero za Muungano ambazo zinatolewa na wananchi wa pande zote mbili.
Kutokana na kelele nyingi kuhusu muungano, iliundwa kamati ya kujadili na kujaribu kutatua kero za muungano ikiongozwa na Makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kutokana na kelele nyingi kuhusu muungano, iliundwa kamati ya kujadili na kujaribu kutatua kero za muungano ikiongozwa na Makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kamati hiyo iliyo na uwiano sawa wa wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano imepokea kero 11 za muungano na kwa sasa wameshazitatua tisa zimebaki tatu ambazo ziko njiani kutatuliwa kwa hivyo kwa upande wa kero wamefikia hatua nzuri sana.
Miungano mingi duniani inakuwa na kero lakini hutatuliwa kwa ushirikiano kwa pande zote zinazohusika. Kwa mantiki hiyo kero ni vitu vya kawaida katika muungano wowote ule uwe wa nchi, mataifa au hata katika jamii. Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia muungano huu.
Nchi nyingi duniani zilizoungana zimeweza kupata maendeleo ya kasi ya kiuchumi na kiulinzi, tunaweza kuuangalia Umoja wa Nchi za Ulaya kama mfano. Vilevile Umoja wa Falme za Kiarabu ambao msingi wake ni uamuzi wa ulinzi wa uchumi wa falme saba ya kiarabu yanayozalisha mafuta yakiongozwa na Abudhabi.
Hivyo muungano kimsingi pamoja na mambo ya kisiasa na kijamii unakuwa na dhamira ya kuendeleza maendeleo ya nchi husika na kutumia rasilimali zao sambamba na rasilimali watu kuweza kujikomboa kiuchumi na kupandisha uchumi wao.
Na kwa Tanzania kupitia Muungano hilo kwa kiasi fulani limewezekana kwa sababu pamoja na kelele zinazopigwa kuhusu rasilimali lakini kimsingi rasilimali zote zinazopatikana Tanzania ni za Watanzania wote kwa sababu zinaelekezwa katika kujenga miundombinu ya maendeleo ya nchi yetu.
Na hata kwa upande wa ulinzi, si rahisi kuichezea Tanzania kwa sababu ina nguvu ya pamoja ambapo pengine Zanzibar peke yake na udogo wake isingeweza kuilinda vyema mipaka yake hasa kwa sababu ni nchi iliyozungukwa na bahari na ni visiwa vya kinacholengwa kwa stratejia za kiuchumi na hata kiutamaduni.
Waasisi wa Muungano huu, kwa kuamini watakuwa na taifa moja madhubuti lisiloyumba wala kuyumbishwa ndipo kwa moyo mmoja walipokubali kuunganisha nchi mbili na kuwa na taifa moja lenye dhamira moja na kwa pamoja kujifaharisha kuwa sisi ni Watanzania, na Tanzania ndiyo nchi inayotambulika Umoja wa Mataifa, si Tanganyika wala si Zanzibar.
Na bado kama kuna nchi ambazo zinataka kuungana basi zije kusoma Tanzania na watajua nini maana ya muungano wa dhati, nini umuhimu wa kuvumiliana, kuaminiana na kusaidiana. Hapa hasa ndipo penye udugu wa kweli hata kama wanagombana lakini hatimaye husuluhishana na kupatana na maisha kuendelea. Waswahili wanasema ‘ndugu wawili wakigombana, chukua jembe ukalime….’
Rashid Yussuf Mchenga ni mwanasiasa mkongwe/mwanaharakati aliyeko Zanzibar
+255 773 560243 / 775-560243
+255 773 560243 / 775-560243
Chanzo:Mwananchi
No comments :
Post a Comment