SERIKALI kupitia kwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo imetangaza kurudisha adhabu ya viboko kwa wanafunzi shuleni ili kujenga nidhamu na kujituma.
Mulugo alisema kuondolewa kwa adhabu ya viboko shuleni kumewafanya wanafunzi wengi kukosa nidhamu na wakati mwingine kujifanyia mambo kienyeji. Kwamba wasipotandikwa mambo hayaendi.
Alisema watoto wa siku hizi wamekuwa wakitumia vibaya teknolojia ambayo ingeweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika masomo yao.
Mulugo alielekeza lawama kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na haki za binadamu, akidai kuwa yamekuwa yakipigania kuondolewa kwa adhabu hiyo shuleni na kusababisha kushuka kwa nidhamu kwa kiasi kikubwa.
Kadhalika alisema serikali imepiga marufuku matumizi ya simu za mkononi kwa sababu baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakizitumia vibaya jambo ambalo linawarudisha nyuma kimasomo.
Tunachelea kukubaliana na msimamo huo wa serikali alioutangaza Mulugo kwani hilo si suluhisho la matokeo mabaya ya mitihani yanaojitokeza kila mwaka nchini.
Huku ni kubabaika kwa serikali kutaka kuwatetea watendaji wake wakiwemo waziri na naibu wake wenye dhamana ya kusimamia sekta ya elimu kwa kushindwa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili.
Matokeo mabaya kwa wanafunzi si jambo lililoibuka ghafla, bali limekuwa na historia ya uwajibikaji mbovu wa viongozi na watendaji. Kwa hiyo serikali isikimbilie katika kutuhadaa na mambo mepesi badala ya kutafuta suluhisho.
Viboko vilikuwepo shuleni miaka nenda rudi, serikali iliona umuhimu na hasara za adhabu hiyo, lakini ikakubali kuvifuta.
Teknolojia ya simu imekuja na ikaachwa itumike kwa wanafunzi wakati serikali hiyo hiyo ikijua madhara yake.
Hivyo kukimbilia kurejesha adhabu ya viboko shuleni na kupiga marufuku simu kwa wanafunzi si mambo pekee yanayoweza kutupatia suluhisho la matatizo yetu katika sekta ya elimu ambayo imepwaya.
Wanafunzi wanapata muda wa kuhangaika na matumizi ya simu za mkononi shuleni pamoja na kuwa na nidhamu mbovu kwa sababu hawana zana za kujifunzia za kutosha ambazo zinawawezesha kujishughulisha.
Kama shule hazina walimu, vitabu, maabara, maktaba, madawati, madarasa ni lazima wanafunzi wawe na muda mwingi wa kupoteza katika kutumia simu na utovu wa nidhamu unatoka huko.
Ni vyema Mulugo na serikali yake wakajipanga upya na kufikiri namna ya kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu kwa kuhakikisha vifaa vya kujifunzia na kufundishia vinapatikana, walimu wanapata maslahi mazuri badala ya kufikiria kurudisha adhabu za kikoloni.
No comments :
Post a Comment