• AFUTA KESI YA WABUNGE CHADEMA, AWATAKA WAFUNGUE UKURASA MPYA
na Martin Malera, Dodoma
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amepata wakati mgumu kuwashawishi wabunge wakubali mabadiliko ya kanuni mpya zitakazotumika wakati wa mjadala wa bajeti.
Hali hiyo ilitokea jana ndani ya Ukumbi wa Pius Msekwa ambapo wabunge wote walikutana pamoja na mambo mengine kupitia mabadiliko ya kanuni zitakazotumika kwa ajili ya utaratibu mpya wa kupitisha bajeti.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilisema kuwa kanuni iliyopingwa na wabunge wengi, hasa wa Chama Cha Mapinduzi ni ile iliyotaka majina ya wachangiaji wa mijadala ya bajeti za wizara mbalimbali yapitie na kuteuliwa kwenye vyama vyao.
Kanuni hiyo ni tofauti na ya sasa ambapo majina ya wabunge wanaotaka kuchangia, hupelekwa kwa Spika moja kwa moja na wabunge wenyewe na ndiye anayeteua majina ya wachangiaji.
Kwa mujibu wa habari hizo, idadi kubwa ya wabunge waliopinga ni wa CCM, ambao walidai kuwa utaratibu huo utakuwa na upendeleo, kwani viongozi watakaoletewa majina hayo wanaweza wasiyateua kutokana na tofauti miongoni mwao.
”Sisi tumekataa kwa sababu majina ya wabunge wanaotaka kuchangia yatapitia kwa viongozi wa vyama bungeni, kisha wao wanayapeleka kwa Spika. Viongozi hao ni kina Jenister Mhagama. Kama hakupendi, hatapeleka jina,” alisema Mbunge mmoja wa CCM.
Mbunge machachari mwingie ambaye amewahi kuitwa mara kadhaa na viongozi wa chama chake na kumtaka aache kuishambulia serikali, alisema kuwa utaratibu huo utamnyima haki ya kuchangia bungeni kwani anaamini hata viongozi wa CCM walio nje ya Bunge, wataingilia kati kutaka asipewe nafasi. Mbunge huyo ambaye jina lake tunalihifadhi, alimtaka Spika kuacha kukwepa majukumu yake.
Endapo kanuni hiyo itapita, itaanza kutumika leo baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kusoma hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Kabla ya Pinda kuwasilisha bajeti ya ofisi yake, wabunge wanatarajiwa kupitisha mabadiliko machache ya kanuni na huenda kukawa na mvutano wa kupitisha kanuni hizo.
Bunge litaanza kupitia na kujadili hotuba za bajeti za wizara mbalimbali ambapo mwaka huu zitaanza wizara kabla ya kusomwa kwa bajeti ya serikali.
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Makinda, amefuta kesi ya wabunge wa CHADEMA waliodaiwa kufanya vurugu katika mkutano wa 10 wa Bunge mjini Dodoma.
Spika aliwataka wabunge hao kusahau yaliyopita na kuanza moja, kwani lengo la wabunge ni kuwatumikia wananchi waliowachagua.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilisema kuwa baadhi ya wabunge wa CHADEMA walimwonya Spika kuwa kama ataendelea na staili yake ya kuwabana wapinzani na kukiuka kanuni hawatavumilia.
No comments :
Post a Comment