Ahmed RajabToleo la 29124 Apr 2013
SIASA hazina adabu. Na zenye utovu mkubwa wa adabu ni zile za madola ya Magharibi zenye kuhusika na maingiliano ya madola hayo na nchi kama za kwetu. Haziheshimu uungwana wa kitaifa wa nchi zetu, hazimheshimu Mwafrika wa kawaida, haziwaheshimu viongozi wetu, haziheshimu maadili wala haziuheshimu ukweli.
SIASA hazina adabu. Na zenye utovu mkubwa wa adabu ni zile za madola ya Magharibi zenye kuhusika na maingiliano ya madola hayo na nchi kama za kwetu. Haziheshimu uungwana wa kitaifa wa nchi zetu, hazimheshimu Mwafrika wa kawaida, haziwaheshimu viongozi wetu, haziheshimu maadili wala haziuheshimu ukweli.
Siasa hizo ndizo zenye kuzifanya nchi za Magharibi mara ziwe zinasema hivi, mara ziwe zinasema vile. Asubuhi huwa na msimamo huu, ifikapo jioni huwa na msimamo mwingine ulio kinyume na wa awali. Mfano mzuri ni msimamo wa nchi hizo kuhusu kadhia ya watuhumiwa wa Kenya mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ya mjini Hague.
Wakati wa kampeni ya uchaguzi wa Machi 4 mabalozi wa nchi za Magharibi, hasa wa Uingereza na wa Marekani, walikuwa wakisema kwamba hawatoshirikiana na Uhuru Kenyatta na William Ruto wanaotuhumiwa kwa makosa ya jinai na Mahakama ya ICC endapo watachaguliwa Rais na Naibu wa Rais. Mabalozi hao wakaongeza kusema kwamba Kenya itaathirika vibaya endapo wawili hao watachaguliwa.
Wiki chache zilizopita niliandika kwenye gazeti hili la Raia Mwema (Changamoto zinazowakabili Uhuru na Ruto) kwamba hizo zilikuwa ni ndaro tu za madola ya Magharibi na kwamba madola hayo hayatokuwa na ubavu wa kuiwekea vikwazo Kenya au kuwatenga viongozi wake.
Nilihoji kwamba Kenya si Sudan, nchi ambayo Rais wake Omar Hassan al Bashir, anafanya kila njia kuikwepa Mahakama ya ICC. Mahakama hiyo imekwishatoa amri kwa nchi zilizotia saini Mkataba wa ICC zimkamate al Bashir na kumpeleka Hague mbele ya Mahakama hayo.
Nikaendelea kuhoji kwamba madola ya Magharibi yana rasilimali kubwa nchini Kenya na hata ikiwa Uhuru na Ruto watachaguliwa madola hayo hayatochukua hatua yoyote itakayozidhuru rasilimali zao. Si hayo tu bali Kenya inategemewa sana na madola hayo hayo ya Magharibi kupambana na ugaidi wa kimataifa.
Majasusi na wanajeshi wa madola hayo wanaingia na kutoka Kenya ambako wana fursa ya kutumia kambi maalumu za kijeshi. Ndege zao za kijeshi pamoja na manuwari zao pia zinaingia na kutoka Kenya ambako mara kwa mara hufanya mazoezi.
Kwa ufupi, Kenya na nchi hizo za Magharibi zimetoka mbali, zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu kuhusu shughuli za kijeshi na nchi za Magharibi hazitotaka mahusiano hayo maalumu yaharibike. Nikaongeza kwamba wala Kenya si Iran. Serikali ya Uhuru Kenyatta haitotoa vitisho dhidi ya Israel wala haina Uislamu wenye kuyataabisha madola ya Magharibi katika maingiliano yao na Iran au Sudan.
Hizo ndizo sababu hasa zinazoifanya Marekani na baadhi ya nchi katika Muungano wa Ulaya ziziandame Iran na Sudan.
Sasa Uhuru na Ruto wameshavikalia rasmi viti vyao — mmoja akiwa Rais na mwingine naibu. Na tunayashuhudia yakitokea yale tuliyokuwa tukisema kuwa yatatokea. Kama ilivyo ada yao nchi za Magharibi zimekwishaanza kuulegeza msimamo wao dhidi ya Uhuru na Ruto. Hata Umoja wa Mataifa nao umebadili msimamo wake. Hivi majuzi umetoa mwongozo mpya usemao kwamba maofisa wakuu wa Umoja huo wanaweza kuwa na maingiliano “bila ya vizuizi” na wale waliotuhumiwa na Mahakama ya ICC.
Farhan Haq, ambaye ni msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema kwamba Umoja wa Mataifa sasa unaruhusu pawepo mawasiliano ya moja kwa moja baina yake na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Willian Ruto.
Umoja wa Mataifa hata hivyo umesema kwamba Rais Bashir wa Sudan aendelee kususiwa kwa sababu ya kuendelea kwake kukataa kushirikiana na Mahakama ya ICC. Ni kwa sababu ya ukaidi huo Mahakama hiyo ikatoa amri za kutaka akamatwe.
Ni muhimu wote wale waliochochea ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 zilizosababisha vifo vya Wakenya zaidi ya elfu moja wafikishwe mahakamani, washitakiwe na wapewe hukumu ya adhabu wanayostahili kupewa. Lazima pawepo haki. Itendeke na ionekane kwamba imetendeka. Kwa hivyo, ni sawa kabisa watu — wananchi wa Kenya na wasio Wakenya — wapige kelele kutaka hatua zichukuliwe zitazowafanya wahusika wa hatia hizo za jinai wawajibike.
Lakini namna baadhi ya nchi za Magharibi zilivyoitumia kesi ya ICC dhidi ya Uhuru na Ruto zinatufanya wengi tuamini kwamba nchi hizo zilikuwa na dhamira nyingine na si ile ya kuwatetea walioathirika kwa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.
Hapo ndipo siasa za hayo madola ya Magharibi zilivyokuwa hazina adabu; kwa kukiuka maadili na kuzitumia kesi za ICC kwa ajenda nyingine kabisa.
Wakati wa kampeni ya uchaguzi takriban balozi zote za nchi za Magharibi zilizo Nairobi zilikuwa zikiushabikia Muungano wa CORD wenye kuongozwa na Raila Odinga. Kwa miaka inayokaribia 30 sasa — tuseme tangu wimbi la demokrasia lilipolikumba bara la Afrika, mabalozi wa nchi za Marekani na wa Muungano wa Ulaya walio katika nchi mbalimbali za Kiafrika wamekuwa wakijifanya kama wao ndio upinzani katika nchi hizo.
Mfano mzuri tuliushuhudia katika uchaguzi huo huo wa Kenya pale balozi wa Uingereza Dakta Christian Turner aliposhikilia kwamba kura zilizoharibika katika uchaguzi wa urais lazima zihisabiwe. Si sawa, kiitifaki wala kiungwana, kwa balozi yeyote wa kigeni kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi nyingine na kushurutisha hili lifanywe au lile lisifanywe.
Hizo balozi za kigeni labda zinahisi kwamba zinastahiki ziwe na usemi juu ya namna nchi zetu zinavyoendeshwa kwa vile serikali zao ni wafadhili wakubwa wa serikali zetu na pia wa asasi zetu za kiraia na jumuiya nyingine zisizo za kiserikali.
Na sababu hiyohiyo labda ndiyo inayozifanya nchi za Magharibi ziwe zinazielekeza jumuiya na asasi hizo ni mada zipi kuu zishughulikiwe hata ikiwa mada hizo zinakwenda kinyume na maadili na tamaduni zetu, mfano ni ndoa za watu wa jinsia moja. Aghalabu hutokea baadhi ya jumuiya za Kiafrika zisizo za kiserikali zikazikumbatia mada aina hizo ama kwa sababu za kutaka kuendelea kufadhiliwa au kwa sababu za kisiasa.
Hizo ni siasa chafu. Na siasa hizo ndio msingi wa sera zinazotungwa, kupangwa na kutekelezwa na madola hayo kwa maslahi yao ambayo kwa kawaida huwa yanayadhuru maslahi halisi ya nchi zetu. Mara nyingi madhara hayo huwa ni ya kujitakia sisi wenyewe na hivyo tunaweza kusema kuwa stahili yatufike.
No comments :
Post a Comment