NA SHARON SAUWA
25th April 2013
Wabunge wamempa wakati mgumu Waziri wa Maji, Profesa Jummanne Maghembe, baada ya kumtuhumu kuwa anajipendelea kutokana na kupeleka Sh. bilioni 32 katika miradi ya maji kwenye wilaya ya Mwanga anayotoka huku fedha za uchangia wa miradi ya maji katika vijiji 10 kwa kila halmashauri nchini ikitengewa Sh. bilioni 13 tu.
Aidha, Waziri huyo amebanwa na Mbunge wa Mwibara, Khangi Lugola (CCM), akitaka athibitishe ukweli wa taarifa alizosoma katika bajeti yake ya mwaka 2013/14 aliyoiwasilisha jana kwamba bomba lenye urefu wa kilometa 23.5 limetandazwa katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara.
Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliyosomwa na Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso, ilisema katika hotuba ya bajeti ya mji wa Same-Mwanga, mradi umetengewa Sh. bilioni 32 na kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 20.6 ni fedha za ndani.
“Na katika miradi yote ya maendeleo ya mwaka huu ya maji hakuna mradi mwingine wowote ambao umetengewa kiasi kikubwa cha fedha za ndani, isipokuwa mradi wa kuboresha huduma za maji katika jiji la Dar es Salaam ulitengewa Sh. bilioni 43,” alisema Pareso.
“Na katika miradi yote ya maendeleo ya mwaka huu ya maji hakuna mradi mwingine wowote ambao umetengewa kiasi kikubwa cha fedha za ndani, isipokuwa mradi wa kuboresha huduma za maji katika jiji la Dar es Salaam ulitengewa Sh. bilioni 43,” alisema Pareso.
Alisema kambi hiyo inataka kupata maelezo ya kina kama fedha zinaweza kutolewa wakati upembuzi yakinifu haujatolewa kwa miradi husika.
“Je, ni kwanini maeneo mengine yanashindwa kupatiwa fedha kwa kigezo kuwa upembuzi yakinifu bado mshauri hajakamilisha?” alihoji.
Alisema suala hilo linapaswa kutolewa maelezo ya kina ili kuondoa manung’uniko ya dhana ya upendeleo katika miradi ya maji na hasa huo ambao ni kwenye wilaya anayotoka Waziri Maghembe kutengewa fedha kabla ya upembuzi yakinifu kukamilika.
“Jambo hili ni hatari sana na hasa ikizingatiwa kuwa mradi huu haukuwa kwenye mpango wa bajeti wa mwaka 2012/2013, sasa leo fedha zinaondolewa kwenye miradi mingine na kurundikwa kwenye wilaya anayotoka Waziri wa Maji au ni nini kilipelekea mgawanyo huo wa fedha?” alihoji.
LUGORA WAZIRI AMEDANGANYA
Lugola aliibuka na kuomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya 68, baada ya Waziri, kamati na msemaji wa kambi ya upinzani kusoma hotuba zao.
“Mimi ni mdau wa maji, atuthibitishie hii kauli kaitoa wapi? Hata mitaro kuchimbwa haijakamilika. Naomba afute kauli hii kwa sababu siyo ya kweli,” alisema na kuongeza kuwa wananchi wa Bunda hawatacheka na mtu wala kuangalia waziri msomi bali kujua ukweli kauli hiyo imetoka wapi.
Alisema yuko tayari kuweka ubunge wake rehani katika jambo hilo kwa kuwa yeye anatokea katika wilaya hiyo na hajaona utekelezaji wa mradi huo licha ya wananchi kusumbuliwa na tatizo la maji.
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai, alimshukuru Lugola kwa ushauri alioutoa kwa serikali na kwamba ujumbe wake umefika.
Wakati akisoma bajeti yake, Profesa Maghembe alisema katika mji wa Bunda kazi ya kulaza bomba lenye urefu wa kilomita 23.5 kutoka kwenye chanzo hadi kwenye matanki iliendelea katika mwaka 2012/2013 na kwamba katika mwaka wa fedha 2013/2014, serikali imetenga Sh. milioni 800 kukamilisha ujenzi wa mradi huo.
Mbunge wa Viti Maalum, Ester Midimu (CCM), alisema katika bajeti ya mwaka jana aliomba kupelekwa kwa maji katika mkoa wa Simiyu, lakini hadi sasa hayajapelekwa.
Mbunge wa Viti Maalum, Amina Amour (CUF), alisema fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya uchimbaji wa visima vya maji zimekuwa zikipotea kwa sababu baadhi ya visima huchimbwa, lakini havitoi maji.
Aidha, alitaka kampuni na viwanda ambavyo vimekuwa vikitumia kiasi kikubwa cha maji kuchangia katika miradi ya maji.
Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo (Chadema), alisema bajeti inayotengwa kwa ajili ya miradi ya maji ni ndogo ikilinganishwa na umuhimu wa sekta hiyo kwa maisha.
Alisema nusu ya watoto hufariki dunia kutokana na magonjwa ya kuambukiza yanayotokana na kukosa maji safi na salama.
Mbunge wa Pangani, Saleh Pamba (CCM), aliitaka serikali kubadili mwenendo wa kutenga fedha za wafadhili katika miradi ya maji na badala yake kutumia fedha za ndani.
Mbunge wa Viti Maalum, Getruda Lwakatare (CCM), alisema serikali ilikataa kutekeleza mradi wa maji ya kutega katika wilaya ya Kilombero ambao ungedumu muda mrefu na badala yake kuchimba visima ambavyo alisema havina tija.
Mbunge wa Viti Maalum, Muhonga Ruhanywa, (Chadema), alilalamikia mmoja wa wahandisi mkoani humo kwa kupeleka mabomba ambayo yako chini ya ubora.
“Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa inatimiza sera yake ya kutaka maji yapatikane umbali wa mita 400?,” alihoji.
Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk. Cyril Chami (CCM), alisema wakati wa kampeni za urais mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete aliombwa na wakazi wa wilaya ya Mwanga wapatiwe maji na alikubali.
Alisema wilaya nyingine za Hai, Moshi Vijijini na Rombo ambalo ni jimbo linaloongozwa na upinzani ziliomba kupatiwa barabara na zimejengewa barabara.
“Mnacholalamika ni nini wakati barabara mlizoomba kujengewa mlijengewa na Mwanga waliomba mradi wa maji wakapelekewa?” alihoji akionekana kujibu hotuba ya upinzani.
Alisema wale wote wanaolalamikia Waziri Maghembe kutenga fedha hizo katika mradi wa maji ni watu ambao wanataka asikamilishe ahadi iliyotolewa na chama chake na hivyo kukifanya kisipate kura katika Uchaguzi Mkuu ujao.
WABUNGE WATAKA NYONGEZA YA BAJETI
Wakati huo huo, Bunge limeitaka serikali kuongeza Sh. bilioni 184 katika bajeti ya maji kwa kuwa Sh. 398,333,474,000 zilizoombwa na Wizara ya Maji hazikidhi mahitaji ya msingi ya kutoa huduma za maji nchini.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusiana na bajeti hiyo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Juma Nkumba, alisema kamati hiyo imepitia kwa undani taarifa ya bajeti na kugundua kuwa wizara ya maji kwa kipindi kirefu imekuwa ikipata bajeti ndogo.
Alisema wizara hiyo imekuwa ikipata bajeti ndogo kutoka fedha za ndani kutekeleza miradi ya maendeleo na fedha za matumizi mengine.
Aidha, alisema fedha zilizoidhinishwa na Bunge hazitolewi zote.
“Kamati hairidhishwi na kitendo cha serikali kupunguza bajeti ya maji ambayo mahitaji yake yanaongezeka kwa kasi mwaka hadi mwaka,” alisema.
Aidha, Nkumba alisema kamati hiyo imebaini kuwa kuna tofauti kubwa kati ya bajeti inayotengwa kwa ajili ya majisafi na salama mijini na vijijini; matokeo yake ni kwamba watu wa wanaopata majisafi na salama mijini ni asilimia 86 huku vijijini ikiwa ni asilimia 58.6.
“Kamati inashauri serikali kuongeza bajeti ya maji vijijini ili kupunguza tatizo kubwa la maji linaloyakabili maeneo mengi,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment