Na Mwinyi Sadallah
IGP Said Mwema.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, kimesema hakiridhishwi na utendaji wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja (RPC), Ahmada Khamis, kutokana na kushindwa kusimamia usalama wa raia na vitendo hatarishi vinavyotishia kuvunja umoja wa kitaifa.
Malalamiko hayo yalitolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Haji Juma Haji, wakati akitoa utangulizi katika mkutano wa majumuisho ya ziara ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, Kinduni Mkoa Kaskazini Unguja juzi.
Haji alisema RPC Ahmada, ameshindwa kuchukua hatua za kiusalama dhidi ya wafuasi wa Uamsho ambao wameendelea na kampeni za kupandikiza chuki miongoni mwa jamii akiachia kupepea kwa bendera za jumuiya hiyo wakati kamati ya ulinzi na usalama mkoa iliamua ziondolewe.
“Mheshimiwa Rais, RPC wako Mkoa Kaskazini hatumtaki kwa kujali maslahi ya umma ukiondoka hapa ondoka naye, tumechoka na vitendo vyake visivyoheshimu taratibu za kiusalama,” alisema Haji.
Alisema tangu kuibuka kwa vitendo vinavyoashiria kuvunjika kwa amani katika mkoa huo vinavvyofanywa na wafuasi wa Uamsho, amekuwa mzito kuchukua hatua za kisheria na kusababisha kuzorota kwa amani na umoja wa kitaifa mkoani humu.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa CCM alisema hata pale walipojaribu kuchukua hatua za kukosoa udhaifu wake wa kiutendaji kwenye vikao ili ajali maslahi ya umma, alijibu kuwa yeye anawatumikia mabwana wawili ambao ni Kamishna wa Polisi Zanzibar na IGP Said Mwema.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema CCM Mkoa imeamua kuliwasilisha katika taarifa yake maalum ya kimaandishi kwenye ziara ya Rais, lakini jambo la kushangaza tangu kuwasilishwa kwa taarifa hiyo, Kamanda Ahmada amekuwa akiisaka taarifa hiyo bila kueleza madhumuni yake.
Hata hivyo, akijibu suala hilo, Rais Dk. Shein aliwataka viongozi wa chama hicho mkoa kutulia na kuahidi kulifuatialia suala hilo ili kupata ukweli juu ya utendaji wa Kamanda huyo.
Dk. Shein alisema kama Polisi wanasaka na kuitafuta taarifa hiyo wamfuate yeye na yuko tayari kuwapa ili kujua kilichoandikwa na kulalamikiwa dhidi yao.
“Kama kusomewa taarifa nimesomewa mimi, yeye anaitafuta ya nini kwani aliyesomewa ni yeye au mimi, akiwa na shida, anifuate nitampatia,” alisema Dk. Shein.
Alisema Serikali inazo taarifa za kuonekana kwa bendera za Uamsho zikipepea katika mkoa huo kana kwamba bendera yake imesajiliwa kisheria kama vilivyo vyama vya siasa.
“Tulieni kama maji ndani ya mtungi, mmenipa taarifa, bendera nimeziona, nitauliza ili kupewa majibu na Mkuu wa Mkoa pamoja na RPC,” alieleza Dk. Shein.
Alisema katika kuongoza Zanzibar, anamuogopa Mwenyezi Mungu pekee na siyo mtu mwingine yeyote kwa vile Zanzibar inaongozwa kwa kufuata Katiba na sheria zake na kumtaka kila mmoja kutii taratibu hizo.
“Serikali ya Zanzibar taratibu zake zilivyo kama Serikali nyingine duniani, inaoongozwa na mihimili mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahakama. Vyombo vyote hufanya kazi zake bila kuingiliwa na mhimili mwingine, lazima tufuate na kuheshimu sheria, kimya kikubwa kina mshindo mkubwa,” alisisitiza Dk. Shein.
Akizungumza na NIPASHE kufuatia malalamiko hayo, Kamanda Ahmada, alisema taarifa hizo kwa kweli ni za kushangaza kwa vile yeye ni mtumishi wa Serikali na si mtendaji wa vyama vya siasa nchini.
“Nimeyasikia malalamiko hayo, lakini ninachofahamu ni kwamba, mimi ni mtumishi wa serikali ninayeongoza kwa kufuata sheria na taratibu za kanuni kipolisi, sifanyi kazi kwa kufuata utashi wa vyama vya siasa. Vyama vya siasa viko vingi nchini,” alisema Kamanda Ahmada.
Alisema utendaji wake wa kazi kama ni mbovu au wenye manufaa, wakuu wake wa kazi ndiyo wenye uwezo wa kumtathmini na kwamba amekuwa makini mkoani humo kusimamia wajibu wake kwa mujibu wa sheria.
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki), imekuwa na kampeni za kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusibabisha vurugu kati ya Mei na Oktoba, mwaka jana na kuiathiri sekta ya utalii huku polisi mmoja kuuawa kwa kupigwa mapanga huko Bububu Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment