Ahmed Rajab
JULAI 5, 1969 saa kama kumi na nusu hivi za Alasiri zilinikuta nikiingia hoteli iitwayo Westbury katika eneo la Mayfair jijini London. Nilifuatana na sahibu yangu mmoja Othman Ismail Nombamba kwenda kumsalimia Abdulrahman Babu aliyekuwa waziri wa mipango na maendeleo ya kiuchumi katika serikali ya Julius Nyerere.
Babu alikuwa akipita njia kuelekea Brussels, Ubelgiji, pamoja na mawaziri wenzake kutoka Kenya na Uganda. Aliyetoka Kenya alikuwa Mwai Kibaki. Jina la mwenzao wa Uganda limenitoka ingawa sura yake bado ninaiona hivi hivi.
Mawaziri hao watatu walialikwa na Jumuiya ya Uchumi ya Ulaya (EEC) waende kuieleza jinsi Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) ya siku hizo ilivyokuwa ikiendesha shughuli zake. Jumuiya ya Ulaya ikitaka kujifunza kutoka Jumuiya ya kwetu iliyoundwa 1967.
Nilipokuwa ndani ya hoteli nanyanyua simu kumpigia Babu chumbani mwake macho yangu yalikigeukia kijiduka kilichokuwa kikiuza magazeti. Bango la gazeti la jioni la Evening Standard lilinadi kwa herufi kubwa: “Mboya assassinated” (Mboya ameuawa.)
Mboya alikuwa ni Tom Mboya, katibu mkuu wa chama cha KANU na waziri wa mipango ya kiuchumi na maendeleo.
Alikuwa na umri wa miaka 39.Babu alipoitikia simu nilimuarifu kuhusu msiba huo. Nikamwambia ntalinunua gazeti na kwenda nalo. Miye na mwenzangu tulipofika chumbani tulimuona Kibaki nyuma yetu akipiga mbio huku akihema akifululizia tuliko.
“Babu wacha jokes (mizaha) zako,” alisema Kibaki alipoingia ndani. Babu akanyosha kidole kumuelekeza Kibaki kwenye gazeti nililokuwa naingia nalo. Baada ya kulisoma papo hapo Kibaki alikata uamuzi na kusema: “Siendi tena Brussels. Narudi nyumbani.”
Ingawa walikuwa watu wa mielekeo tofauti ya kisiasa nakumbuka Babu alikuwa akimsifu Mboya kwa uchapaji kazi wake, kwa uhodari wake na jinsi alivyokuwa akijadili mambo kwenye vikao alivyohudhuria naye.
Ingawa walikuwa watu wa mielekeo tofauti ya kisiasa nakumbuka Babu alikuwa akimsifu Mboya kwa uchapaji kazi wake, kwa uhodari wake na jinsi alivyokuwa akijadili mambo kwenye vikao alivyohudhuria naye.
“Wakati mwingine hufunga macho utadhani amelala au huwa anasoma gazeti lakini kumbe huwa hadhir akiyasikia yote yasemwayo,” alinena Babu. Ilikuwa rahisi kumpenda Mboya. Alikuwa mcheshi, mzungumzaji mzuri aliyekuwa na bongo kali. Alivitumia vipaji hivyo kuwaongoza wafanya kazi wa Kenya na kuutetea umajumui Wakiafrika.
Nilionana naye Mboya mara mbili tatu alipokuwa akija London na kuhutubia wanafunzi wa Afrika ya Mashariki katika nyumba tuliokuwa tukikaa ya East Africa House.
Mara ya mwisho kukutana naye ilikuwa miezi kadhaa kabla hajauliwa nilipoambiwa na shirika la utangazaji la BBC nende kumhoji katika hoteli aliyoshukia ya Kensington Palace Hotel.
Siku hizo zile mashini za kurekodia za Uher zilikuwa zimeingia mjini na mtangazaji mwenzangu Mohamed Bakhressa, mzalia wa Mombasa, alijitolea kuja kunisaidia. (Bakhressa alikuwa mtu wa mwanzo kutumia neno ‘kutaifisha’ badala ya ‘kuchukuliwa au kutwaliwa na serikali’.)
Mboya alitupokea kwa bashasha chumbani kwake. Tulimkuta akiwa maridadi, kavalia vizuri, suruwali ya kijivujivu, shati jeupe na tai. Koti alikuwa amelitundika. Nilitambua kwamba alikuwa na miadi na akitaka nianze kumhoji kwa haraka ili aikimbilie.
Lakini mashini ya Uher ilikuwa ikitucheza na baada ya kutuvumilia kwa muda hakuweza tena kujizuia. Hadi leo nayakumbuka maneno aliyotwambia: “Come on boys, fanyeni haraka.” Alitwita watoto lakini yeye mwenyewe hakuwa mtu mzima hivyo.
Nakumbuka tulipomaliza nilikuwa nimejawa na furaha. Mashini ya Uher haikufanya ukorofi na Mboya aliyajibu maswali yangu yote kwa ufasaha.
Mboya alikuwa na usuhuba mkubwa na Kwame Nkrumah. Nadhani chanzo cha usuhuba huo ni utetezi wa Mboya wa ndoto ya Nkrumah ya Afrika moja iliyoungana.
Mwaka 1958 Nkrumah aliwaalika wanasiasa kutoka nchi nyingine za Kiafrika wahudhurie mkutano wa All-African People’s Congress mjini Accra. Mboya alichaguliwa awe mwenyekiti wa mkutano. Alikuwa na umri wa miaka 28.
Mwaka 1958 Nkrumah aliwaalika wanasiasa kutoka nchi nyingine za Kiafrika wahudhurie mkutano wa All-African People’s Congress mjini Accra. Mboya alichaguliwa awe mwenyekiti wa mkutano. Alikuwa na umri wa miaka 28.
Juu ya yote hayo Mboya alikuwa na maadui katika kambi mbili. Kambi ya kwanza ilikuwa ya wale waliokuwa hawataki amrithi Rais Jomo Kenyatta katika uongozi wa Kenya.
Kambi ya pili ilikuwa ya Wakomunisti wa mrengo wa Sovieti waliokuwa wakimuona kuwa si chochote ila kibaraka wa Marekani.
Haikushangaza kwa nini Wakomunisti walimfikiria hivyo. Kwanza alikuwa na mahusiano mazuri na serikali ya Marekani — wengine wanasema hata na Shirika la Ujasusi la CIA la nchi hiyo.
Pili alikuwa mpinzani wa sera za Kikomunisti za Muungano wa Sovieti. Badili yake alipendekeza ‘usoshalisti Wakiafrika.’ Na yeye Mboya pamoja na Kibaki ndio walioandika rasimu ya ile iitwayo Sessional Paper No. 10 iliyowadhihisha ni nini hasa itikadi hiyo na jinsi inavyoweza kutumiwa kwa maendeleo ya Kenya.
Rasimu hiyo baadaye ikafanyiwa kazi zaidi na kamati maalum ya maofisa wa wizara yake na hatimaye Mboya ndiye aliyeihariri. Ndio maana wengi wanasema kwamba Sessional Paper No. 10 ilikuwa kazi ya Mboya. Mmoja wa walioipinga itikadi hiyo ya ‘Usoshalisti wa Kiafrika’ alikuwa rafiki yake mwenyewe Mboya aliyekuwa akifanya kazi wizarani kwake. Akiitwa Barack Hussein Obama, babake Rais Obama wa Marekani.
Mboya si mwanasiasa wa mwanzo wa Kenya kuuliwa tangu nchi hiyo ipate uhuru. Februari 24, 1965 wiki chache tu kabla ya Sessional Paper No.10 kujadiliwa bungeni Pio Gama Pinto, mwandishi habari na mwanasiasa aliyekuwa akifuata itikadi ya Kimarx alipigwa risasi na kuuliwa nje ya nyumba yake jijini Nairobi akiwa na umri wa miaka 38.
Mzalendo huyo ambaye wazazi wake walikuwa Magoa alikuwa mshauri mkuu wa Jaramogi Oginga Odinga. Hadi leo haijulikani nani hasa aliyemuua Pinto na kwa nini. Kuna wasemao kwamba aliuliwa na vigogo katika serikali ya Kenyatta. Kuna wasemao kwamba aliuliwa na wakoloni mamboleo kwa vile alikuwa Mkomunisti shupavu.
Kadhalika hadi leo haijulikani nani hasa aliyemuua Mboya na kwa nini. Kuna wasemao kwamba aliuliwa na vigogo katika serikali ya Kenyatta. Kuna wasemao kwamba aliuliwa na Wakomunisti kwa sababu ya siasa zake za kuupinga kwa nguvu Ukomunisti.
Wala Mboya si mwanasiasa wa mwisho wa Kenya kuuliwa. Kuna wengine waliomfuatia ambao ama waliuliwa au inashukiwa kuwa waliuliwa.
Wala Mboya si mwanasiasa wa mwisho wa Kenya kuuliwa. Kuna wengine waliomfuatia ambao ama waliuliwa au inashukiwa kuwa waliuliwa.
Miongoni mwa waliouliwa ni J.M.Kariuki, Bruce Mackenzie (Mkenya mzungu aliyekuwa waziri wa kilimo katika serikali ya Kenyatta na pia jasusi wa Uingereza), G.G. Njuguna Ngengi, Mugabe Were, Dkt. Robert Ouko, Horace Ongili na Dkt Chrispin Mbai.
Kwa hakika tangu Mboya auliwe kila mwanasiasa wa Kenya akifa ghafla au katika ajali iwe ya barabarani au ya ndege watu huanza kushuku kwamba aliuliwa.
Mwezi mmoja kabla ya Mboya kuuliwa, hasimu yake wa zamani waziri wa mambo ya nje Clem Argwings-Kodhek alifariki katika ajali ya gari. Watu wengi wanaamini kwamba si ajali ya gari iliyomuua bali risasi alizotwangwa. Argwings-Kodhek alikuwa akipenda kusema kwamba “Wamarekani si marafiki zake Mboya, ni mabwana zake.”
Waziri mwingine aliyefariki katika ajali ya gari alikuwa Ronald Ngala. Lakini familia yake haikubali kwamba gari lake lilipinduka baada ya dereva wake kuumwa na nyuki walipokuwa safarini kutoka Mombasa kuelekea Nairobi Desemba 12, 1972. Mwanawe Noah Katana Ngala anataka uchunguzi ufanywe upya kuhusu kifo cha babake.
Masinde Muliro alikuwa mpinzani wa Rais Daniel arap Moi na mmoja wa waliokuwa safu ya mbele kupigania urejeshwe mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Agosti 14, 1992 aliporudi kutoka London alikokwenda kutafuta msaada wa chama chake cha Ford alianguka uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi, na akakata roho.
Madaktari walisema maradhi ya moyo ndiyo yaliyomuua. Wengi hawaamini. Wanasema kwamba kauli hizo zilikuwa za kuwatuliza tu.
Juni 10, mwaka jana waziri wa mambo ya usalama wa ndani ya nchi Profesa George Saitoti pamoja na waziri msaidizi wake Orwa Ojodeh walifariki helikopta yao ilipodondoka kutoka angani na kuangukia Ngong Hills.
Ijapokuwa tume rasmi baada ya kufanya uchunguzi wa kina ilitoa sababu kadha wa kadha za kwa nini helikopta hiyo ilianguka bado mpaka leo kuna watu wenye kuamini ya kuwa ajali hiyo ilikuwa ya kupangwa ili Saitoti afe.
Dhana kama hizo ziliibuka tena Jumamosi iliyopita Seneta wa upinzani Mutula Kilonzo alipokufa ghafla nyumbani kwake kwenye shamba lake huko Maanzoni, kilomita chache kutoka Nairobi.
Inavyosemekana ni kwamba Mutula alikuwa mzima alipokwenda shambani kwake saa nane za mchana siku ya Ijumaa. Alijishughulisha na kazi za shambani kwake na baada ya kula githeri na nyama choma saa moja za usiku aliingia chumbani kwake kupumzika.
Siku ya pili yake mpishi wake aligonga mlango wa chumba chake kwa vile hakutokeza kustaftahi baina ya saa tatu na nusu na nne na nusu kama ilivyo kawaida yake.
Siku ya pili yake mpishi wake aligonga mlango wa chumba chake kwa vile hakutokeza kustaftahi baina ya saa tatu na nusu na nne na nusu kama ilivyo kawaida yake.
Hapo ndipo alipoikuta maiti yake kitandani. Inasemekana kwamba maiti hiyo ilionyesha kwamba Mutula alitokwa na mapovu mdomoni na matapishi yake yalionekana chooni na kitandani.
Karakhana na vinu vya kufua na kuvumisha uvumi na udaku nchini Kenya vimekuwa vikifanya kazi usiku na mchana tangu maiti ya Mutula ilipoonekana. Kati ya minong’ono iliyopo ni kwamba Mutula alilishwa sumu. Kuna sababu kadhaa zinazotolewa za kwa nini inaweza kuwa Mutula aliuliwa.
Mwandishi mmoja wa kike wa gazeti moja la Kenya, kwa mfano, alidai kwamba Machi 28 Mutula alimwambia ana siri ambayo akiitoboa taifa zima la Kenya litatikisika. Itazusha hofu kubwa na msukosuko nchini, alisema.
Mwandishi huyo anasema kuwa alimshikilia Mutula amdokolee siri hiyo lakini Mutula alikataa kumpa maelezo zaidi. Alisisitiza tu kwamba siri hiyo itawashangaza Wakenya na itaweza kuwa na matokeo makubwa kwa taifa. Sasa Mutula atalala nayo kaburini siri hiyo.
Halafu kuna vitisho. Tangu 2008 Mutula akipelekewa maandishi ya simu kuambiwa kuwa atauliwa. Mara moja alidai kwamba aliambiwa kwanza mkewe na binti yao watabakwa kabla yeye kuuliwa.
Binafsi nadhani Mutula alikufa ghafla kutokana na maradhi ya moyo. Hiyo lakini ni dhana yangu tu. Ukweli halisi utajulikana baada ya daktari atayeichunguza maiti atapotoa ripoti yake.
Familia ya Mutula inavyoonyesha haiwaamini madaktari wa Kenya na imeagiza daktari mtaalamu wa mambo hayo kutoka Uingereza.
No comments :
Post a Comment