dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, June 17, 2013

Je, Kikwete aongezewe muda wa urais?

Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Ahmed Rajab
Toleo la 298
12 Jun 2013
WATAALAMU wa mambo ya katiba na hata wasio wataalamu wa mambo hayo haweshi kubishana ni wapi ilikoandikwa katiba ya kwanza duniani. Ni Uyunani ya kale au ni China ya kale? Wapi kulikopandwa mbegu za kwanza zilizozaa matunda ya katiba za nchi?
Kwa hakika, majibu ya maswali hayo si muhimu wala hayatusaidii kitu katika dunia yetu ya leo isipokuwa labda kutukumbusha tu walimwengu tulipotoka tangu katiba za mwanzo kutungwa.
Katiba ya mwanzo iliyoandikwa ya Uyunani ilikuwa na mambo ya ajabu ajabu. Kwa mfano ilisema kwamba “mwanamke yoyote wa kiungwana aruhusiwe mjakazi mmoja tu wa kufuatana naye ila ikiwa amelewa: wala asitoke mjini usiku, asivae dhahabu au kanzu za nakshi za almaria ila ikiwa anajulikana kuwa ni kahaba; hakuna mwanamume anayeruhusiwa kuvaa pete ya dhahabu ila ikiwa ni jambazi.” Katiba hiyo pia ilipiga marufuku unywaji wa mvinyo usiotiwa maji isipokuwa kwa sababu za tiba.
Aliyeitunga katiba hiyo alikuwa Zaleucus. Inasemekana kwamba bwana huyo alikuwa akiwatia adabu wenye kuzini kwa kuwapofoa macho.
Mwanawe alipopatikana na hatia hiyo alikataa kumsamehe. Lakini badala ya kumpofoa macho yote mawili akakhiari apofolewe yeye jicho lake moja na mwanawe jicho moja.
Zaleucus pia aliweka sheria ya kupiga marufuku watu kuingia bungeni wakiwa na silaha. Safari moja alikuwa na dharura na akaingia bungeni akiwa na upanga.
Alipokumbushwa kuhusu sheria hiyo papo hapo akajipiga upanga tumboni akijitolea mhanga kuweka nidhamu katika jamii. Labda sheria yake moja inayotupasa tuizingatie kwa makini ni ile inayohusu katiba.
Sheria hiyo ilisema kwamba mtu yoyote aliyependekeza mfumo mpya wa sheria, yaani katiba mpya, au mageuzi katika katiba iliyopo basi alilazimika kufika mbele ya Baraza la Raia akiwa ametiwa kitanzi shingoni mwake. Baraza likipiga kura kupinga pendekezo lake basi hapo hapo akinyongwa.
Hiyo ilikuwa sheria kali. Hata hivyo inatukumbusha kwamba uandikwaji wa katiba ya nchi si jambo la maskhara wala si kazi nyepesi. Ni kazi nzito yenye dhamana kubwa mno na inahitaji utulivu na uvumilivu wa hali ya juu.
Na si kwetu tu. Nchini Nepal mchakato kama huo umekuwa ukiendelea kwa muda wa miaka minane. Kwa miaka sasa Nepal imekuwa ikiendeshwa kwa katiba ya muda. Katiba ya kudumu ilikuwa izinduliwe Mei 28, 2010 lakini tarehe hiyo ilipofika katiba mpya haikuwa tayari.
Kipindi cha katiba ya muda kikaongezwa kwa mwaka.  Lakini Mei 25, 2011 Mahakama ya Juu Kabisa nchini humo iliamua kwamba si haki kuongeza umri wa hiyo katiba ya muda. Hata hivyo, Bunge la Katiba lilikubali kuongeza muda huo lakini kwa vipindi vya miezi michache michache tu.
Hatimaye Mei 28, 2012, Waziri Mkuu Baburam Bhattarai alilivunja Bunge la Katiba baada ya Bunge hilo kushindwa kukamilisha utungwaji katiba.
Barani Afrika Mei mwaka huu Tunisia ilijipatia rasimu nyingine ya Katiba tangu mchakato wa kutunga katiba mpya uanze baada ya kupinduliwa Rais Zine al-Abidine Ben Ali na utawala wake wa chama cha Destour mnamo 2010. 
Chama hicho ndicho kilichotawala tangu Ufaransa iipe nchi hiyo uhuru wake mwaka 1956 na Habib Bourguiba kuwa Rais wake wa kwanza.
Hiyo rasimu ya Mei ilikuwa ni ya tatu tangu 2010. Wananchi wa Tunisia wamepongezwa kwa kuikamilisha rasimu hiyo. Lakini huo si mwisho wa mambo. Hivi sasa rasimu hiyo inapitiwa na kujadiliwa na Bunge la Katiba.
Ingawa rasimu hiyo ni afadhali kuzishinda zile mbili zilizoitangulia hata hivyo hiyo nayo pia bado ina utata. Kuna wenye kulalamika kwamba baadhi ya vifungu vyake viliingizwa kwa mlango wa nyuma.
Na kuna wenye kutahadharisha kwamba baadhi ya vipengele katika rasimu hiyo vinaweza vikatumiwa na serikali zijazo kuzichimba haki za kimsingi za binadamu na uhuru wa raia.
Wanachoonya ni kwamba ikiwa vipengee hivyo vitaachiwa vibakie katika katiba ya kudumu vinaweza vikatumiwa kuikaba demokrasia.
Katiba zinazotungwa au kuandikwa kwa papara aghalabu huwa dhaifu. Tumelishuhudia hilo nchini Misri ambako Bunge limeipitisha kwa haraka rasimu ya katiba na kuifanya iwe sheria ya nchi.
Kwa sababu rasimu hiyo ya katiba ilipitishwa kwa haraka kuna kero mbalimbali za kikatiba zitazoendelea kutokota chini kwa chini na kuibuka mara kwa mara na hivyo kuzusha mizozano katika jamii. Mizozo aina hiyo aghalabu husababisha marekebisho ya katiba.
Ni bora zaidi kutunga katiba itayodumu kuliko kuwa na waraka ambao huenda baada ya muda mfupi ukahitaji kuchanwa hapa na kutiwa viraka hapa na pale.
Utungwaji wa katiba unahitaji mambo fulani yawe sawa.  Tume inayotunga katiba mpya, kwa mfano, haitoweza kutunga katiba ya kudumu na yenye kuridhisha iwapo chama kinachotawala kitashikilia kuwa lazima kiwe na kauli ya mwisho juu ya nini cha kukubaliwa katika rasimu ya katiba na nini cha kutupiliwa mbali.
Nchini Tunisia chama kinachotawala cha Ennahda kingeweza kuuteka nyara mchakato wote wa utungwaji katiba na kufanya kitakavyo. Lakini hakikufanya hivyo. Kiongozi wake Rachid Ghannoushi alikuwa na busara ya kutaka pawepo maafikiano baina ya chama chake na wapinzani.
Lengo la katiba ni kuwa na sheria zitazozifunga serikali na kuzizuia zisifanye mambo hovyo hivyo yatayoweza kuwadhuru wananchi.
Wakati huo huo sheria hizo huwa zinailinda demokrasia kwani kuna hatari ya serikali iliyochaguliwa kwa njia za kidemorasia kuchukuwa hatua zinazoweza kuwadhuru raia au hata kuuchimba mfumo wenyewe wa kidemokrasia.
Lililo muhimu katika mchakato kama huo ni kwamba jamii, kwa jumla, iwe inaafikiana kuhusu misingi au mihimili mikuu ya huo waraka uitwao ‘katiba.’
Ili jamii iweze kuafikiana itahitaji kwanza ipate fursa ya kuweza kujadiliana, bila ya vipingamizi, kuhusu misingi au mihimili mikuu ya katiba inayotungwa.
Makundi ya kijamii, ya kisiasa na wananchi, kwa jumla, waweze kuchangia fikra zao katika utungwaji wa katiba kiasi cha kuwafanya waamini kwamba hiyo katiba ni yao, walioitunga wao wenyewe.
Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Kenya kwa namna ambavyo Wakenya walihusishwa katika utungwaji wa katiba yao mpya. Jambo moja la kupigiwa mfano ni jinsi mijadala ya hadhara ilivyokuwa ikiendeshwa Kenya kuhusu vipengele mbalimbali vya rasimu ya Katiba yake mpya.
Mijadala hiyo iliyokuwa ya hadhara iliwawezesha Wakenya wakubaliane kuhusu vipengele mbalimbali vya rasimu ya Katiba. Likiwa taifa linatapatapa, haliwezi kuamua kuhusu vipengele maalumu vya katiba basi taifa litajivunja moyo lenyewe na litapata shida ya kuukamilisha mchakato mzima kwa muda lililojipangia.
Nchini Tanzania mchakato wa kulipatia taifa katiba mpya unaendelea huku wanasiasa wakiwa wanajiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao wa 2015. Uchaguzi kama tujuavyo ni moja ya misingi mikuu ya mfumo wa kidemokrasia unaofuatwa na nchi nyingi za Kiafrika. 
Ilivyopangwa ni kwamba uchaguzi ujao uendeshwe kwa mujibu wa Katiba mpya itayozinduliwa 2014, miaka 50 baada ya kuzaliwa Tanzania. 
Swali linalozuka ni kuwa je, endapo patatokea taahira ya kuzinduliwa Katiba mpya Jakaya Kikwete aruhusiwe kuendelea kuwa Rais? Katiba mpya huenda ikachelewa kupatikana ikiwa patazuka mizozano mikubwa kuhusu rasimu ya Katiba.
Lipi lililoakhasi, baya zaidi, kumuongozea Kikwete muda wa urais au kufanya papara ya kuwa na Katiba mpya 2014 ilimradi Tanzania iwe tuna katiba mpya wakati huo hata kama itakuwa na dosari?
 Chanzo: Raia Mwema

No comments :

Post a Comment