dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, June 23, 2013

Kikwete atwishwa mzigo

23rd June 2013


  Wasomi wahoji, ni binafsi au msimamo wa serikali
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutaka polisi kuwapiga raia wasiotii amri halali ya jeshi hilo, sasa suala hilo limeelekezwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema Rais Kikwete, akiwa Amiri Jeshi Mkuu, anapaswa kueleza tamko la Pinda ni kauli binafsi ama msimamo wa serikali yake.
Chadema inatajwa na `kunyooshewa kidole’, kwamba inahusika katika kuandaa mikutano na maandamano yanayotawanywa na polisi kwa kile kinachodaiwa kufanyika kinyume cha sheria.
Kwa hali hiyo, Chadema kupiti Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, kimesema kinatilia shaka tamko la Pinda bungeni, kikisema huenda ikawa ‘nyuma ya mashambulizi’ yanayodaiwa kufanywa na polisi kwa nyakati tofauti dhidi ya raia wasiokuwa na hatia.
Hata hivyo, akifafanua kuhusu tamko lake bungeni, Pinda, alisema wanaoistahili adhabu ya kupigwa ni raia wanaoshindwa kutii amri ya polisi, inayotolewa kwa lengo la kuepusha vurugu nchini.
Lakini taarifa ya Mnyika iliyosambazwa na Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Mekene, ilisema kuwa majibu ya Pinda bungeni yanatilia shaka kuhusu matukio yanayotajwa kuwahusisha polisi kuwa na mkono wa serikali.
Mnyika alitoa mfano wa maeneo ambayo vyombo vya dola vimetumika na kuwanyima wananchi haki ya kuishi kwa kusababisha mauaji ni pamoja na Mwanza, Ruvuma, Mbeya, Mtwara na Mara.
DK. BANA: PINDA AMEKOSA UVUMILIVU
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema kauli ya Pinda inaonyesha ni jinsi gani alivyoshindwa kuvumilia jambo zito linalohitaji ufumbuzi wa kudumu.
“Pinda hakutoa kauli nzuri bungeni, lazima aangalie jambo zito na alichukuliaje kama kiongozi…si vyema kuruhusu vyombo vya dola viwapige watu kwa kukiuka amri, je, kama hawajakiuka na wamepigwa, itakuwaje,” alihoji.
Akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, Pinda alisema ikiwa serikali (kupitia polisi) itatoa amri au maagizo ili yafuatwe, lakini ikatokea mtu ama watu kukaidi katika hali inayoashiria vurugu, hapatakuwa na namna nyingine zaidi ya kupigwa.
Mbunge huyo alitaka kusikia kauli ya serikali kuhusu vurugu zilizoambatana na raia kupigwa mabomu katika mikoa ya Arusha na Mtwara.

AVIKOSOA CHADEMA, CCM
Dk. Bana alisema kauli zilizotolewa kwa nyakati tofauti na Chadema na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhusu vurugu za Arusha, hazikuwa za kiungwana.
Alisema kitendo cha Chadema kulalamika moja kwa moja kuhusiana na ulipukaji wa bomu katika mkutano wao na kumhusisha polisi, pamoja na CCM kudai chama hicho (Chadema) wamejilipua ni za uchochezi.
“Hizi ni kauli za uchochezi na za kukurupuka kwa viongozi wa Chadema na CCM, lakini pia Waziri Mkuu ametoa kauli nzito sana juzi na kushindwa kuangalia jambo zito lichukuliwaje,” alisema Dk. Bana.
Kuhusu mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa Chadema mjini Arusha, Dk Bana, aliiasa jamii kutambua kwamba ni mapema kujua asili na kusudio lake.
“Lakini suala hilo linaweza likawa la kigaidi ama jinai, na hivyo wanasiasa wasiingilie na kulibeba wakati vyombo vya ulinzi na usalama vinalifanyia uchunguzi,” alisema.
Dk. Bana alisema tukio la kwanza la kulipuka kwa bomu katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Olasiti Jimbo Kuu la Arusha, polisi waliachiwa kufanya uchunguzi, lakini hali haipo hivyo kwa upande wa ilivyotokea kwa Chadema.
“Wakati Chadema wakizungumza kuhusu tukio hilo, Nape naye anakurupuka na kudai chama hicho kinafanya kile wanachotaka…sasa vyombo vya usalama vinafanya kazi gani,” alihoji.
Aidha, alisema iwapo Chadema hakiamini vyombo vya dola hata kupeleka ushahidi polisi, basi wanatakiwa kujenga hoja bungeni kutokuwa na imani na polisi na busara zifanyike ili chombo hicho kifanye kazi yake.
Mhadhiri huyo alivitaka vyama vya siasa kujenga mazingira ya kuaminiana na kuwa na imani kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema ili kufikia mustakabali mzuri wa taifa, lazima kujenga mazingira ya kuheshimiana, kuvumiliana na kujenga ushindani kwa njia ya hoja na upendo.
Alisema kila chama lazima kitafakari wanachokifanya kutokana na ukweli kwamba, vyote vinalenga kuwaongoza Watanzania.
“Tukio la Arusha linalaaniwa na kila mtu, lakini kwanza tuache vyombo husika vifanye kazi yake,” alisema Profesa Mukandala.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment