zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, August 17, 2013

Mwakyembe athubutu

NA THOBIAS MWANAKATWE

17th August 2013


  Awataja maofisa wa usalama wanaodaiwa kusaidia kupitisha dawa Uwanja wa JNIA
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, akiongea mbele ya waandishi wa habari jana.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, ameacha kilio katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), baada ya kuwataja maofisa usalama wanne wanaodaiwa kuhusika katika njama za kusafirishwa dawa za kulevya.

Hali hiyo inaufanya uwanja huo kuwa `uchochoro’ wa kupitisha dawa hizo, hivyo ameagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) wafukuzwe kazi, wakamatwe na kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Ametoa agizo hilo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua ambazo wizara imezichukua, kufuatia kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8 zilizokamatwa Julai 5, mwaka huu nchini Afrika Kusini zikitokea Tanzania, kupitia kwenye JNIA.

Dk. Mwakyembe aliwataja maofisa usalama hao watakaofukuzwa kazi na kufunguliwa mashtaka ya jinai chini ya Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya kuwa ni Yusufu Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana.Mbali na maofisa hao, pia ameliagiza Jeshi la Polisi kumuondoa mara moja katika uwanja huo, askari polisi, Kapteni Ernest na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwake kwenye njama za kupitisha mabegi sita ya dawa za kulevya, yaliyokamatwa nchini Afrika Kusini.

Pia alisema polisi inapaswa kumsaka Nassoro Said Mangunga aliyevikwepa vyombo vya dola nchini Afrika Kusini na kutoroka na mabegi matatu ya dawa hizo.

Dk. Mwakyembe alisema mbeba mizigo katika uwanja huo, Zahoro Mohamed Seleman, anapaswa kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ili kuunganishwa na wenzake kujibu mashtaka ya jinai.

Dk. Mwakyembe pia ameiagiza Idara ya Usalama wa Taifa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa wake waliokuwa zamu siku ya tukio, kwa kuchelewa kuwafikisha mbwa wakati mwafaka kukagua mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya na hivyo kuliletea Taifa fedheha kubwa.

Alisema ameamua kuchukua hatua hizo kwa kuwa tukio hilo si la kwanza, bali ni sehemu ya matukio mengi ya upitishaji wa dawa hizo katika uwanja wa JNIA, ambayo taarifa zake zinaifikia serikali pale watuhumiwa wanapokamatwa nje ya nchi wakitokea Tanzania.

“Tulishasema awali kuwa hii ni fedheha kubwa sana kwa nchi, hivyo hatuwezi kuiachia hali hii iendelee kwenye kiwanja kikuu cha ndege kinachobeba jina la Baba wa Taifa ambalo kwa namna yeyote ile halitakiwi kudhalilishwa,”alisema.

MAOFISA USALAMA WALIVYONASWA NA KAMERA
Dk. Mwakyembe alisema siku ya tukio, mfumo wa kamera za usalama (CCTV) zilizopo JNIA, zilionyesha kuwa kuanzia saa 9:25 hadi 10:30 alfajiri tukio zima lilivyotendeka.

Alisema saa 9:28 alfajiri, kamera hizo zilimuonyesha kijana mmoja mbeba mizigo, Zahoro Mohamed Selemani, akiwa anazungukazunguka eneo la kuingilia abiria katika uwanja huo mithili ya mtu mwenye miahadi.

Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, kamera hizo pia zilimnasa mfanyakazi wa uwanja huo, Yusuf Daniel Issa, akitoka nje ya jengo la abiria na kuingia tena mara kadhaa, huku akiongea na simu kitendo ambacho hakiruhusiwi kwa wafanyakzi wa eneo la ukaguzi wa abiria.

Dk. Mwakyembe alisema wakati huo huo, kamera hizo zilimuonyesha Kapten Ernest akiwa analandalanda eneo la uhakiki wa hati za kusafiria kama vile anasubiri kitu fulani.

Alisema ilipofika saa 10:15, walionekana vijana wawili wa kike na kijana mmoja wa kiume sehemu ya kuingilia abiria wakiwa na mizigo na mabegi tisa yaliyofanana.

Alisema, wasichana hao walitambulika kuwa ni Agnes Gerald Deal maarufu Masogange mwenye hati ya kusafiria ya Tanzania namba AB440180, Melisa Edward aliyekuwa na hati ya kusafiria namba AB440565 na mvulana aliyefuatana nao ambaye ni Nasorro Said Mangunga mwenye hati ya kusafiria ya Tanzania namba AB426496.

Kamera hizo kwa mara nyingine, zilimuonyesha Kapteni Ernest akihangaika kuwasaidia abiria mbalimbali kuweka mizigo yao kwenye mashine ya ukaguzi, kazi ambayo siyo yake .

Aidha, mbeba mizigo Zahoro, alionekana akiwasaidia wasichana hao kupeleka mizigo yao kwenye mashine ya ukaguzi na baadaye kuyazungushia mabegi hayo karatasi za nailoni na kuyafikisha kaunta ya Shirika la Ndege ya Afrika Kusini.

Alisema, mfanyakazi wa uwanja huo Yusufu Daniel Issa ambaye awali alinaswa na kamera akihangaika kupiga simu, alimuondoa mfanyakazi mwenzake, Jackson Manyonyi na kukalia kiti cha mkaguzi wa mizigo (screener) ikiwa ni dakika chache kabla ya mabegi hayo tisa hayajaingia kwenye mashine ya ukaguzi.

Dk.Mwakyembe, alisema kinyume cha utaratibu wa kazi, Issa aliyemuondoa mwenzake kwenye kiti cha mkaguzi wa mizigo hakujiandikisha kwenye kitabu cha wakaguzi , ndipo ilipofika saa 10:16 aliaanza kuipitisha mizigo hiyo mpaka saa 10:22 alfajiri.

Aliongeza kuwa Issa alipomaliza kupitisha mizigo hiyo kwa dakika sita, akamwachia kiti mfanyakazi mwenzake Manyonyi, na kuondoka na akabadilishana maneno kidogo na Kapteni Ernest na kurejea sehemu aliyokaa Manyonyi na kumnong’oneza kitu.

Alisema baadaye, ofisa huyo alielekea ukumbi wa abiria wa ndani ya nchi, huku akiongea na simu na kwamba mambo hayo yalifanyika huku kiongozi wa sehemu ya ukaguzi kwa jina Juliana Thadei, akiwa hapo hapo bila kushtuka.

Dk. Mwakyembe, alisema baada ya kuipitisha mizigo hiyo kwenye mashine ya ukaguzi, vijana hao walihama na mizigo yao kwenye kaunta ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini na mabegi matatu ya kilo 20 kila moja, yalipitishwa yakabaki sita ambayo yalitakiwa yalipiwe malipo ya uzito wa ziada.

“Kwa taratibu za shirika hilo la ndege, kila kilo moja inayoongezeka hulipiwa dola tano na hivyo vijana walitakiwa kulipa Dola 600 za Marekani, kinachonishangaza walitozwa Dola 94 tu ambazo zinathibitishwa na stakabadhi iliyopo,” alisema Dk. Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mangunga ambaye hakuwa na tiketi ya kusafiria siku hiyo baadaye alibadilisha mawazo hapo hapo na kuamua kuondoka siku hiyo kwenda Afrika Kusini ambapo alilipa Dola 60 kwa huduma hiyo (re-booking).

“Hivyo basi, mhakiki wa nyaraka za safari nje ya ukumbi wa abiria siku hiyo, Mohamed Kalungwana hakupaswa kumruhusu Nassoro kuingia ndani ya ukumbi bila tiketi ya siku hiyo,” alisema.

Alisema kwa hali ya kawaida, mizigo ikifikishwa kwa abiria, inakaguliwa tena kwa kutumia mbwa, lakini siku hiyo mbwa walichelewa na waliletwa baadaye wakati mizigo hiyo ikiwa imeingizwa kwenye masanduku ya chuma.

“Kwa abiria watatu tu kuwa na mabegi makubwa tisa, tena yanayofanana si kitu cha kawaida kukwepa jicho la maafisa wa ushuru na forodha na ya vyombo vya usalama walikuwa wapi,”alihoji Dk. Mwakyembe.

WATAKAOBAINIKA KUTANGAZWA HADHARANI
Dk. Mwakyembe alisema kuanzia sasa, mtu atakayekamatwa akisafirisha dawa za kulevya katika viwanja vya ndege vilivyopo nchini, atatangazwa na picha yake kuchapishwa kwenye vyombo vya habari na kwamba wafanyakazi wa viwanja hivyo wakae chonjo wakibainika kula njama zozote watafukuzwa kazi.

“Wapo vijana wengi wa kidato cha nne, sita na chuo kikuu wapo mitaani hawana kazi, kwa hiyo mtu akifanya ujanja ujanja ajue nitamfukuza kazi mara moja na kuwaajiri vijana ambao hawana kazi wanazunguka mitaani,” alisema Dk. Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe amechukua hatua hiyo ikiwa ni siku mbili tu baada ya kufanya ziara ya kushitukiza JNIA na kubaini kuwa tatizo la uwanja huo kufanywa `uchochoro’ wa kupitishia dawa za kulevya, hakutokani na ukosefu wa vifaa bali ni watu wenyewe waliopewa dhamana ya kusimamia.

NIPASHE ndilo lilikuwa la kwanza kuripoti taarifa za kukamatwa kwa wasichana wawili raia wa Tanzania waliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oriver Tambo uliopo eneo la Kempton Park, Afrika Kusini wakiwa na dawa hizo aina ya Crystal Methamphetamine.

Waliokamatwa ni Agnes Jerald (25), Melisa Edward (24), ambao wameshtakiwa Afrika Kusini.

Wanawake hao walikamatwa wakiwa na dawa hizo ambazo pia zinajulikana kama ‘Tik’ na baadaye walikabidhiwa polisi na kufunguliwa mashtaka.

KASI YA WATANZANIA KUKAMATWA NJE
Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 wamekamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.

Katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini na kuharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.

Wiki moja baada ya tukio la wasichana hao, Watanzania wengine wawili walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia Dubai hadi Hong Kong. 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment