Chanzo: ZanzibariYetu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Zanzibar iko katika harakati za kukifufua upya kituo cha kupandishia ng’ombe kilichopo katika eneo la Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ili kirejee katika utaratibu wake wa kutoa huduma bora kwa wafugaji wa ngo’mbe wa kisasa hapa nchini.
Kituo hicho kilianzishwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya 70 na kusitisha huduma zake kutokana na mabadiliko ya sera ya ufugaji kwa kuachwa suala hilo liendeshwe na wananchi moja kwa moja.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Zanzibar Dkt. Kassim Gharib alieleza hayo wakati wa ziara fupi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika katika eneo hilo kukagua juhudi zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika kukifufua tena kituo hicho.
Dkt. Kassim alimueleza Balozi Seif kwamba Wizara hiyo imeanza na hatua ya kuzungushia ukuta eneo hilo ili kuzuia uvamizi wa ujenzi holela wa nyumba pamoja na uchimbwaji hovyo wa mchanga uliokuwa ukitishia uchafuzi wa mazingira.
Alisema hatua hiyo itakapokamilika itatoa fursa kwa wafanyakazi wa mifugo kuendelea na hatua ya pili ya upandaji majani kwa ajili ya malisho ya madume ya ng’ombe watakaotumiwa kutoa mbegu na kuendelea kusambazwa kwa wafugaji kwenye maeneo mbali mbali nchini.
Dkt. Kassim alifahamisha kwamba licha ya matatizo na changamoto mbali mbali zilizokuwa zikikikabili kituo hicho lakini bado kinaendelea kutoa huduma za upandishaji ng’ombe hadi sasa kikiwa na madume sita bora ya kisasa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif pia alipata fursa ya kukagua karakana inayohudumia matengenezo ya dharura ya vyombo vya moto vya Wizara hiyo ya Mifugo na Uvuvi iliyopo jirani na kituo hicho.
No comments :
Post a Comment