NA MWANDISHI WETU
9th September 2013
Vile vile, Rais Kikwete ni heri vyama hivyo vikafa kwani havina manufaa kwa wakulima na kwamba serikali haitahangaika kuviinua vyama hivyo.
Rais Kikwete ameyasema hayo juzi usiku, wakati akipokea ripoti ya maaendeleo ya Mkoa wa Mwanza kwenye Ikulu Ndogo katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo.
Alisema siyo kazi ya Serikali kuviokoa vyama vya ushirika kutoka kwenye madeni kwa sababu shughuli za ushirika ni za sekta binafsi na mali ya wanachama wenyewe.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa makosa ya ushirika na wizi wa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika hatimaye yanabebeshwa vyama vya siasa.
Rais Kikwete amewataka viongozi mbali mbali wa mikoa kuwasaidia wananchi ili kupata viongozi waadilifu na waaminifu na wala siyo wezi kama ilivyo sasa kwa vyama vingi vya ushirika.
“Tumewahi huko nyuma kulipa madeni yote ya vyama vya ushirika. Nia ilikuwa kuvisaidia vyama hivyo na wanachama wake kujipanga upya na kupata uhalali wa kuweza kukopa fedha za kjuendesha shughuli zao. Lakini sasa, vyama hivyo, vimerudi kule kule kwenye madeni,”alisema.
Alitoa mfano wa Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Pwani kama moja ya vyama vya ushirika ambavyo madeni yake yalilipwa na Serikali lakini sasa kina deni kubwa zaidi kuliko hata lile lililolipwa na Serikali.
“Wale watu wa Pwani walikwenda kukopa na benki moja ikakubali kuwapa fedha. Wameshindwa kulipa na ule ushirika nadhani utakufa. Njia bora kwa vyama vya namna hiyo ni kuviachia vife tu kwa sababu havina faida yoyote kwa mkulima.”
“Vyama vya ushirika siyo mali ya Serikali. Ni mali ya wanaushirika hivyo ushirika ni sekta binafsi.
Lakini hakuna shaka kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wanatesa wananchi. Wanakopa fedha kwenye mabenki lakini wanashindwa kuzirudisha fedha hizo na hilo linapotokea Serikali inalaumiwa kwa hali hiyo,”alisema.
Rais alikuwa anatoa maelekezo yake baada ya kuambiwa kuwa Chama cha Ushirika cha Nyanza cha Mkoa wa Mwanza kilikuwa kinakamilisha mpango wa kukopa kiasi cha sh bilioni saba kutoka Benki ya Raslimali Tanzania (TIB) kwa ajili ya kununulia pamba.“Uamuzi wa kukopa ama kutokukopa ni wa kwenu.
Nyanza ni mali yenu, wezi waliopata kukibebesha madeni chama hicho mliwachagua nyie wenyewe. Fedha ni zenu lakini hatimaye athari za makosa yenu yanaiathiri Serikali na hata vyama vya siasa,”
“Kuna wakati viongozi wa Chama cha Nyanza walipata kuuza godown ya thamani ya Sh milioni 600 kwa sh milioni 50 tu…. Hawa ni wezi wa mchana wanaoiba kweupe. Wanaiba lakini wanataka Serikali iwasaidie.
Kwa nini? Nadhani kazi yetu kama viongozi ni kuwasaidia wananchi kupata viongozi adilifu na aminifu siyo wezi,” alisema Rais Kikwete.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment