Aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mansour Yusuf Himid akisisitiza kitu alipokuwa akizungumza na wananchi mbalimbali (hawapo pichani) kuhusu msimamo wake baada ya kufukuzwa Uanachama CCM , katika ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar
TANGU mwanzoni mwa sakata la Mansour Yussuf Himid, nilijua fika hatimaye atabaki Mzanzibari zaidi kuliko mwana-CCM, kwa uamuzi wowote uliochukuliwa katika kushughulikia suala lake.
Lakini lililo muhimu zaidi kwa watu kulifahamu kwa hatua iliyofikiwa, ni ukweli kuwa Mansour amehukumiwa “vikali” bila ya kusikilizwa. Amepewa hukumu ya kiwango cha mwisho juu – kuvuliwa uanachama au kufukuzwa chama.
Wakati aliitwa ilipoketi Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (KM-NEC) ya Zanzibar, hakuitwa kupata uhakika wa maelezo yake suala lake lilipofika Kamati Kuu au NEC.
Kwa mujibu wa taarifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma, Mansour amefukuzwa kwa kushindwa kutekeleza kazi kwa ufasaha, kukiuka na kukaidi katiba ya CCM na kuisaliti Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.
Hakuna hata “shitaka” moja kati ya yale yaliyoelezwa kwenye pendekezo la Kamati Maalum ya NEC ya Zanzibar lililofafanuliwa vizuri.
Kwa kuwa tuhuma zake zinahusu utendaji kazi ya siasa, ilitarajiwa aelezwe bayana. Asomewe tuhuma; na asikilizwe kama ana neno la kusema hata kabla ya mjadala wa tuhuma hizo.
Kwa kuwa tuhuma zake zinahusu utendaji kazi ya siasa, ilitarajiwa aelezwe bayana. Asomewe tuhuma; na asikilizwe kama ana neno la kusema hata kabla ya mjadala wa tuhuma hizo.
Njia nyingine. Mkuu wa vikao vya Dodoma angeagiza Mansour aitwe na kusomewa tuhuma zinazomkabili. Angekuja, na kama asingependa kuwepo, ingejulikana alikataa kutumia haki hiyo.
Iwapo angekuwa ameitwa na kufika mbele ya kikao, angesomewa tuhuma. Angezisikia. Labda mjadala wa tuhuma ungefanywa yeye akiwa nje ya kikao. Ni sawa.
Lakini baada ya mjadala, ingetarajiwa mkuu wa kikao aagize kwa mara nyingine Mansour aitwe. Apewe au asipewe taarifa ya majadiliano. Mwisho angesomewa mtizamo wa kikao baada ya tuhuma zake kujadiliwa.
Mansour angetakiwa kusema jambo lolote kama angependa. Hatua ya mwisho angetakiwa kusikiliza uamuzi baada ya tuhuma kujadiliwa. Angesikiliza uamuzi ukisomwa.
Pale ambapo uamuzi umeshasomwa na Mansour akiwa amesikia uamuzi, ingetarajiwa kuwa atakiwe kutoa kauli. Hapo, labda angetoa utetezi.
Utetezi ungekubalika ingejulikana. Laa, ungekataliwa pia ingejulikana. Mkuu wa kikao angeagiza Mansour aelezwe haki zake za msingi baada ya kusomewa uamuzi wa kikao juu ya tuhuma zilizomkabili. Angekuwa amesikiliza haki zake zikiorodheshwa moja baada ya nyingine.
Kufikia hapo, Mansour angekuwa amepewa haki zote tangu mwanzo wa usikilizaji mashitaka mpaka mwisho uamuzi unapotolewa.
Inasikitisha Mansour ambaye si mjumbe wa kikao cha ngazi yoyote ndani ya chama, alichukuliwa tu yale aliyoyatoa mbele ya Kamati Maalum. Lakini hao wakuu wa Kamati si ndio waliomtungia tuhuma? angekuwa na imani kiasi gani ya kutendewa haki?
Mbele ya Kamati Maalum imeelezwa kuwa alisema maneno machache mno. “Nimesikia, nifukuzeni leo, nifukuzeni kesho, lakini huo ndio msimamo wangu.”
Kumbe angesemaje kwa kikao ambacho amekosa imani nacho? Hicho ndio kikao kilichompa tuhuma. wapo walimotetea Mansour kuwa hakuna kosa alolifanya.
Nje ya kikao, wapo wanaosema wazi kuwa kwa kutoa maoni yake, ametumia haki yake ya kikatiba kama raia kutoa anachokiamini. Unamsakama vipi?
Hivi inakuaje chama kinachojinasibu kuwa na nguvu kubwa, wafuasi wengi, mtandao ulio imara, kikiwa ndicho kinachoshika serikali, kinajadili tuhuma na kufikia uamuzi wa kumfukuza uanachama mtu pasina kumpa fursa ya kujieleza?
Kwa hivyo, baada ya hukumu iliyotolewa dhidi yake, Mansour amebakiwa na haki ipi? Mtu hatakuwa ametenda kosa lolote akisema hakutendewa haki.
Ninataka kuamini hapa ndipo chama kinapoonekana kuchukua uamuzi usiokuwa wa busara wala hekima. Kimechukua uamuzi usiozingatia maslahi ya Mansour kama mwanachama wala akiwa kama mwananchi tu.
Pengine macho ya viongozi wa CCM waliohudhuria vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, yaliamini kuwa kwa vile tayari zipo tuhuma dhidi ya Mansour, basi hakukuwa na sababu ya kumpa nafasi ya kusema, bali asubiri tu hukumu.
Kama hivyo ndivyo, basi pia si dhambi kwa mtu kusema chama chenyewe kimefanya kosa kubwa kiuwajibikaji. Kutokana na hatua kiliyoichukua ya kumjadili, kufikia uamuzi wa kumfukuza chama, kitakuwa kimemkandamiza.
Wapi sakata lilianzia? Mwanzo wake ni mbali. Katika hatua za awali, baadhi ya viongozi wenye ushawishi walitumika kujenga mazingira ya kumfitini. Yapo mambo yakifanywa kwa siri.
Walio ndani wanasema kwa muda mrefu ulisukwa mpango wa kummaliza. Na hii ilitokana na alipoanza kutoa kauli hadharani akitamka kuwa ingawa haungi mkono Uamsho, anavutiwa na kaulimbiu yao isemayo, “Tuachiwe Tupumue.”
Kaulimbiu hii iliyotoholewa na viongozi wa Uamsho, ilikusudiwa kuwaamsha Wazanzibari watanabahi kuwa wanayo haki ya kujiongoza lakini kwanza sharti watoke kwenye minyororo ya kubanwa. Wamefungwa shemere mfano wa ng’ombe anayekusudiwa kuvuta mizigo.
Ng’ombe akishafungwa shemere, hawezi kukaidi amri ya mchunga wake. Anajua kama akijaribu kukaidi amri, anapata machungu kutokana na kidonda. Hathubutu kuvuta kwa nguvu kamba ya shemere kwa sababu anajua atajimaliza mwenyewe.
Wazanzibari wamefungwa shemere kutokana na mfumo wa Muungano. Hawapiki hawapakui. Hawachumi wala hawalishi. Wapowapo tu.
Wazanzibari wameaminishwa kuwa hawanufaiki na Muungano kwa mfumo uliopo. Wameshaamua kutaka mabadiliko ya mfumo. Wanataka Zanzibar yenye mamlaka kamili chini ya Muungano wa Mkataba.
Hili limewajaa kama lilivyomjaa Mansour. Matamshi yake ya mapema katika Baraza la Wawakilishi, na mengine aliyokwishayatamka akiwa kwenye shughuli za Kamati ya Maridhiano inayoongozwa na mwanasiasa mkongwe Hassan Nassor Moyo, yanaakisi ukweli huu.
Alikotoka
Hakuwa katika siasa za majukwaani. Akifanya shughuli za biashara. Ghafla baada ya uchaguzi mwaka 2000, aliteuliwa mjumbe wa baraza la wawakilishi. Akateuliwa waziri wa nchi Maji, Ujenzi, Nishati, Ardhi na Mazingira.
Baada ya uchaguzi wa 2005, aliteuliwa tena waziri baada ya kuwa mwakilishi wa kuteuliwa na rais. Katika uchaguzi wa 2007 wa CCM, alishinda ujumbe wa NEC.
Katika uchaguzi mkuu wa 2010, alishinda uwakilishi jimbo la Kiembesamaki. Akateuliwa Waziri wa Kilimo, Maliasili na Mazingira. Akateuliwa mkuu wa idara ya fedha na uchumi wa chama. Nafasi hizo alivuliwa baada ya uchaguzi wa CCM 2012
Chanzo: Mawio
No comments :
Post a Comment