NA MHARIRI
10th September 2013
Katika habari hiyo tulieleza kwamba Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mnero Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, Andrew Chiunguile, amejeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa kwa kupigwa kwa mawe na magongo na wanafunzi, ambao walimtuhumu kula fedha zao walizolipa kwa ajili ya mitihani ya majaribio (Mock) na michango mingine.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki baada ya wanafunzi hao kukusanyanyika na kuanza kurusha mawe kwenye majengo ya shule hiyo, ambayo mengine yalimjeruhi mwalimu huyo.
Ilielezwa kuwa baada ya kuona hali inakuwa mbaya, baadhi ya walimu waliokuwa shuleni hapo, walimchukua mwalimu mwenzao na kumficha kwenye moja ya vyumba vya shule hiyo hadi Polisi wa kituo cha Wilaya ya Nachingwe walipofika eneo hilo.
Uongozi wa shule hiyo ulichukua uamuzi wa kuwaita askari polisi baada ya jitihada ya kuzuia hasira za wanafunzi hao kugonga mwamba kutokana na kuzidiwa nguvu na wanafunzi hao.
Katika kutuliza ghasia za wanafunzi, polisi walilazimika kufyatua mabomu ya kutoa machozi na ndipo wanafunzi walipoanza kutawanyika kuondoka kwenye maeneo ya shule.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakanjinga, wanafunzi watatu walishikiliwa kwa muda na jeshi hilo na kuachiwa baada ya kuchukuliwa maelezo na kwamba upelelezi unaendelea ili kubaini chanzo cha vurugu hizo.
Licha ya kumjeruhi mwalimu huyo, vurugu za wanafunzi hao zimesababisha hasara kubwa kutokana na kuharibu samani mbalimbali zikiwemo viti, madawati na taa za umeme na kuvunjwa kwa milango.
Inadaiwa kuwa hasira za wanafunzi hao zilianza baada ya baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne kuzuiwa kufanya mtihani huo kwa madai ya kutolipa ada ya mtihani wakati wenyewe wakisema walishalipa kupitia kwa mwalimu huyo.
Wanafunzi wanadai mwalimu huyo alipewa jukumu la kukusanya michango hiyo lakini hakuziwasilisha fedha hizo kwa mkuu wa sekondari hiyo, hali iliyowafanya waathirike kwa kutoruhusiwa kufanya mitihani.
Kwanza tunachukua fursa hii kulaani vikali tukio zima ambalo limesababisha madhara na hata mali kuharibika.
Tunalaani wote waliohusika na hata kusababisha ghasia hizo kutokea kwa namna moja ama nyingine.
Kwa ujumla wake, tukio hilo limetuonyesha jinsi gani maadili yalivyoporomoko miongoni mwa wanafunzi na hata walimu.
Miaka ya hivi karibuni kumezuka tabia mbaya ya baadhi ya wanafunzi kufanya vurugu na kuharibu mali za shule pale wanapokuwa na malalamiko au kutoridhishwa na uamuzi fulani.
Tabia hii ni utovu wa nidhamu na inapaswa kukomeshwa mara moja na wanaofanya vitendo hivyo kuchukuliwa hatua kali ili liwe fundisho kwa wengine wasiendeleze vitendo hivyo.
Aidha, tulitegemea kuwa mwalimu anatakiwa kuwa mfano wa maadili mema na uadilifu mbele ya wanafunzi badala ya kuwa mfano mbaya kama ilivyo kwa mwalimu huyu.
Haiingii akilini kwamba mwalimu anaweza kutumia fedha za michango ya wanafunzi waliyotoa kwa ajili ya kufanya mitihani wakati akijua fika athari za kufanya hivyo.
Walimu wa namna hii nao wanapaswa kuchukuliwa hatua kali kwani wanaonyesha mfano mbaya kwa wanafunzi na hata wakati mwingine kuwa chanzo cha vurugu zinazotokea shuleni kama ilivyo kuwa kwa Shule hii ya Sekondari Mnero.
Wasimamizi wa elimu wilayani humo nao hawatakwepa lawama katika suala hilo. Kwani kuna taarifa kuwa kabla ya wanafunzi hao kufanya fujo, walitoa malalamiko kwa Ofisa Elimu ya Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Abdallah Membe, juu ya kuliwa fedha zao za mitihani.
Na hii inathibitishwa na Membe mwenyewe ambaye amekaririwa akisema ofisi yake inafahamu tatizo hilo lakini akajitetea kuwa ilikuwa imepanga siku hiyo ya tukio kukutana nao na kuwapa ufafanuzi.
Laiti kama wahusika wangechukua hatua za haraka kuingilia kati, hakika wanafunzi hao wasingefikia hatua waliyochukua.
Hii inaonyesha ni jinsi gani baadhi ya maofisa waliopewa dhamana na jamii wasivyowajibika na kuwa tayari kuchukua hatua za haraka pale yanapotokea matatizo.
Tunalaani na kusisitiza kuwa ni aibu kubwa kwa walimu kuwa chanzo cha machafuko shuleni.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment