NA MHARIRI
27th September 2013
Katika uzinduzi uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, pamoja na mambo mengine ilielezwa kuwa kundi la vijana linaongoza kwa idadi kubwa ya watu sawa na asilimia 26.
Takwimu hizo zilibainisha kuwa watu milioni 19.7 sawa na 44% ya watu wote nchini ni watoto wenye umri chini ya miaka 15, vijana kuanzia miaka 15 hadi 35 wakiwa milioni 15.6 sawa na 35%, pamoja na wazee ambao ni milioni 2.5 sawa na 6%.
Kwa vyovyote itakavyoelezwa takwimu hizi ni moja ya nyenzo za kupanga mipango ya maendeleo ya nchi, iwe kwenye huduma za elimu, afya na hata kujiandaa kwa ajili ya uwekezaji mdogo na mkubwa.
Kama alivyosema Balozi Iddi mwenyewe, kwamba ni vema takwimu hizo zikatumika vizuri kwa maana ya kusaidia watendaji ndani ya serikali kupanga vizuri mipango ya maendeleo, sisi hatuna tunachoweza kuongeza zaidi ya hapo isipokuwa ni kueleza tu kwamba kushindwa katika kupanga, kubashiri na kukabiliana na jambo lolote ambalo limo ndani ya uwezo wa watalaam wetu wa uchumi na mipango bora ya ardhi, miji na upatikanaji wa huduma bora za kijamii, siyo kutia mambo chumvi kusema utakuwa ni uzembe wa makusudi.
Kwa mfano katika takwimu zilizotolewa zinaeleza kuwa mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya vijana ambao ni 46.8% wakiwa kati ya umri wa miaka 15-35 huku mkoa wa Singida ukishika nafasi ya mwisho ukiwa na 30.7%.
Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na asilimia kubwa zaidi ya watu wenye umri wa kufanya kazi, 66.3% huku mkoa wa Simiyu ukishika nafasi ya mwisho ukiwa na 45.5%.
Mchanganuo huo pia unaonyesha kuwa idadi ya wazee imepungua kutoka asilimia 6.2 mwaka 1988 hadi kufikia asilimia 5.6 mwaka jana, yawezekana kuwa Watanzania wanakufa mapema zaidi ndiyo maana hawako wengi, kwa maana hiyo kuna haja ya kutafiti na kutafakari sababu zake na kupata tiba.
Takwimu hizi zikitazamwa vizuri serikali itagundua nini kifanyike wapi katika kuimarisha sekta ya huduma za kijamii, itatambua nguvu zaidi zilekezwe wapi katika kutatua matatizo ya huduma za afya, elimu, mipango bora ya mkazi na ardhi, lakini la muhimu zaidi kujua ni kwa kiasi gani huduma kwa kundi ambalo haliwezi tena kuzalisha mali linaweza kuhudumiwa chini ya mfumo wa hifadhi ya jamii.
Mathalani, katika takwimu zilizotolewa asilimia 6 ya watu wote ni wazee kuanzia miaka 60, hawa wanaelezwa kufikia watu milioni 2 .5. Ukilitazama kundi hili peke yake mtu anaweza kujiuliza swali, hivi sera ya taifa ya huduma za afya bure kwa wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea inawezekana? Kwamba Tanzania kama taifa linaweza kutoa huduma za afya bure kwa wazee hawa ambao ni milioni 2.5 tu?
Lakini pia takwimu hizi zinaipa serikali changamoto nyingine kwamba kama kundi la vijana kuanzia miaka 18-35 likiwakilisha watu milioni 11.8 sawa na 26%, ambalo linakuwa na umuhimu wa kipekee nchini kisiasa na kiuchumi, linatazamwa vipi?
Hivi katika kundi hili la vijana ni kiasi gani kimetengwa kuwawesha kupata elimu ya kutosha, kutengeneza fursa za ajira, kuwashirikisha katika nafasi na vyombo vya maamuzi vya taifa lao, maswali yanaweza kuwa mengi, lakini cha msingi ni kujiuliza kwa ujumla wale ni kwa kiwango gani serikali sasa inafurahi kwamba ina nyenzo muhimu ya kuamua ifanye nini katika kupanga mipango yake yote ya maendeleo?
Tunaungana tena na Balozi Iddi kwamba takwimu hizi siyo takwimu tu za kukaa kwenye makabrasha na mashubaka ya serikali, bali ni nyenzo muhimu kwa watendaji wa serikali katika kutikiza majukumu yao.
Tunataraji zitafanya kazi hiyo ili tuachane na tabia ya kufanya vitu kwa kubuni, lakini pia zitusaidie kutibu matatizo ya nchi hii yanayozidi kuongezeka ya vijana wengi kukimbilia mijini wakati hawakuna wanachokifanya na kuacha vijiji vikiwa na wazee tu bila uzalishaji wowote wa maana mashambani. Takwimu za sensa zitukomboe kujipanga vema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment