zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, September 3, 2013

Serikali yagongana sakata la Rwanda

NA WAANDISHI WETU

3rd September 2013


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Serikali imetoa kauli za kukinzana kuhusiana na usuluhishi wa mgogoro wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda.

Wiki iliyopita Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni kutoka kwa wabunge, alisema Rais Jakaya Kikwete, amemwomba Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kuwa msuluhishi wa mgogoro huo.

Wakati Pinda akitoa kauli hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema Tanzania haijamuomba Rais Museveni kusuluhisha mgogoro huo, bali Rais huyo (Museven) ameitisha Mkutano wa Kimataifa wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu  (ICGLR) ambao utafanyika jijini Kampala kesho.

Waziri Membe alisema moja ya ajenda katika mkutano wa kesho ni kujadili mgogoro kati ya  Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika  mgogoro huo, Rwanda inadaiwa kukisaidia kikundi cha waasi wa DRC cha M23 kinachoendesha mapigano Mashariki kwa DRC hususani katika mji wa Goma ulioko Jimbo la Kivu Kaskazini.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Waziri Membe alisema Rais Museveni ameitisha mkutano wa ICGLR utakaofanyika mjini Kampala na nchi 10 zinatarajiwa kushiriki ikiwamo Tanzania na kusisitiza kuwa vyombo vya habari vilipotosha suala la Tanzania kupatanishwa na Rwanda.

Membe alisema Tanzania imeombwa na Rais Museveni kushiriki  katika mkutano huo, na Rais Kikwete amekubali kushiriki. Hata hivyo, Waziri Membe hakutaka kueleza kama mkutano huo utakuwa na ajenda ya kujadili kuzorota kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Rwanda.

Alisema kabla ya kukutana kwa marais wa ICGLR kesho, leo watakutana mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo.

“Tanzania haijamwomba Museveni kusuluhisha mgogoro, bali kuna mkutano wa ICGLR ulioitishwa na Rais Museveni na Rais Kikwete amekubali kuhudhuria mkutano huo,” alisema Membe kwa njia ya simu.

Waziri Membe alisema nchi za Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi, DRC, Msumbiji, Zambia na Jamhuri ya Kati zitahudhuria mkutano huo na kueleza kuwa mojawapo ya ajenda itakayojadiliwa ni mgogoro wa Rwanda na Kongo.

Pinda alitoa majibu hayo Alhamisi iliyopita wakati akimjibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, aliyetaka kufahamu mikakati ya serikali ya kushughulikia mgogoro wa kidiplomasia unaoendelea kati ya Tanzania na Rwanda na kutishia kuitenga Tanzania katika EAC.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliongeza kuwa kinachoonekana katika mgogoro huo, Rwanda imezishawishi Uganda na  Kenya kusimama upande wake na miezi kadhaa iliyopita, viongozi wa Jumuiya hiyo, walikutana Uganda na Kenya bila Tanzania kuwapo katika kikao hicho.

Vile vile alizungumzia hatua ya nchi wanachama kadhaa wa EAC kupinga utaratibu wa vikao vya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kufanyika jijini Arusha ambako ni makao makuu ya jumuiya hiyo badala yake vifanyike kwa kuzunguka katika nchi zote wanachama.

Pinda alisema ni kweli katika siku za karibuni, kumekuwapo na hali ya kutoelewana kati ya  Tanzania na Rwanda na kuwa kiini cha yote hayo kimetokana na ushauri alioutoa Rais Kikwete kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame,  juu ya kumaliza mgogoro wa nchi yake na waasi wa kundi la FDLR.

Pinda alisisitiza kuwa ushauri alioutoa Rais Kikwete kwa Rais Kagame, ulikuwa na nia nzuri, lakini bahati mbaya nchi hiyo iliutafsiri tofauti.

Alifafanua kuwa ushauri huo wa Rais Kikwete ambao aliutoa wakati wa kikao cha viongozi wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia, ulikuwa na nia nzuri na wenye mazingira ya urafiki na kuwa Tanzania haina sababu yoyote ya kugombana na nchi jirani na inajitambua nafasi yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu.

Hata hivyo,  Pinda hakulieleza Bunge kama Rais Kikwete ameshawasilisha ombi hilo kwa Rais Museveni kwa ajili ya kuanzisha jitihada za kuzipatanisha Rwanda na Tanzania.

Kumekuwapo taarifa za kumshutumu Rais Kikwete katika vyombo vya habari vya Rwanda na kwenye mitandao ya kijamii.

Habari hizo zimetia chumvi kwamba ushauri wa kuitaka Rwanda kuzungumza na waasi wa FDLR wanaoendesha mapambano na Rwanda wakitokea DRC ni sawa na kutoyatambua mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini humo.

KAULI YA EAC
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Charles Njoroge, amesema, jumuiya hiyo haijapokea taarifa  rasmi zinazoelezea kuwapo uhasama wa kisiasa baina ya  Tanzania na Rwanda.

Alisema kwa msingi huo hakuna sababu ya wananchi kuhofia kuwa kuna ugomvi baina ya Rwanda na Tanzania, ambao unaweza kuvuruga mipango ya mtangamano.

Njoroge aliyasema hayo jana katika mahojiano na wanahabari jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa jumuiya inaliona suala hilo kuwa si mgogoro kama inavyodhaniwa na kuwataka wanachama wasiwe na wasiwasi kuwa Tanzania na Rwanda zinagombana.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment