zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, September 4, 2013

Watanzania kumiliki sekta ya gesi asilia ni haki yao

NA MHARIRI

4th September 2013


Katuni
Hakuna ubishi kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi chache sana duniani ambayo imejaliwa neema kubwa ya rasilimali asilia. Katika orodha hii kuna ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo, kuna maji ya mito na maziwa, yapo madini ya aina mbalimbali, kuna mbuga za wanyama, na sasa tunzungumzia gesi asilia na huenda tukazungumza pia mafuta ya petroli huko tuendako.

Hii ni neema ya bure kutoka kwa Muumba. Hakuna aliyechemsha bongo ili Tanzania iwe na vitu hivi na wala hakuna aliyezembea katika nchi nyingine hivyo watu wao wakakosa rasilimali hizi. Ni neema ya wote!

Rasilimali hizi ni urithi wa taifa. Hakuna hata mmoja anayeweza kusimama na kujipiga kifua kuwa ana hali za ziada juu ya rasilimali hizi zaidi ya Watanzania wengine. Huu ni urithi wetu sote.

Kwa bahati mbaya sana, katika miaka ya hivi karibuni ama kwa kutokujua au kwa makusudi wapo viongozi wetu wamemua kujitwalia mamlaka ya kuwa na hati miliki ya rasilimali hizi. 

Viongozi hawa wamekuwa na jeuri ya kusema lolote juu ya rasilimali hizi. Viongozi hawa wamekuwa na kebei na kiburi kinachoakisi shibe ya chakula na ulevi wa madaraka kiasi cha kushindwa kujua kuwa ofisi za umma wanazokalia ni dhamana walizopewa na umma.

Wenye dhamama hizi ni umma. Na ni kwa maana hiyo ni lazima wakati wote umma uone kazi inayofanywa ni kuwahakikishia kuwa wananufaika ndani ya taifa lao, kwamba rasilimali asilia katika taifa lao ni zao na ni lazima waone jinsi wanavyonufaika, jinsi wanavyoshiriki katika mchakato wa kuzimiliki na kuzitumia kwa ajili yao sasa na kwa vizazi vijavyo.

Wiki iliyopita Waziri wa Nishati na Madini alitangaza kuwa serikali haitarudi nyuma katika kuuza vitalu vya gesi katika mpango wake wa nne  wa uendelezaji wa sekta hiyo.

Waziri alisema hayo akipuuza na kutupilia mbali wito kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ya nchi hii kwamba kwa kuwa sera mpya ya gesi na hata sheria mpya bado haijawa tayari, ni vema serikali ikawa na subira kuliko kukimbizana na uuzaji wa vitalu hivyo kwa sasa.

Sera na sheria mpya ikishatoka, kwa hakika itaweza masharti na mzingira tofauti juu ya Watanzania kumuliki rasilimali hizi.

Nia ya wito kama huu ni kuepuka yale yaliyotokea kwenye sekta ya madini miaka ya mwishoni ya tisini na 2000 ambayo yalisababisha mvutano mkubwa kutoka kwa wadau wa madini kiasi cha kulazimisha haja ya kupitiwa upya kwa sheria husika.

Serikali imekuwa na tabia ya kuwa na kasi  kubwa katika kufanya maamuzi ya uvunaji wa rasilimali za  taifa ambayo aghalabu huwa na gharama kubwa kwa wananchi. Sekta ya madini ni mfano halisi katika hili.

Kwa maana hiyo, tunaungana na wito wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kwa serikali kwamba hakuna sababu ya kukimbizana kuuza vitalu vipya vya gesi wakati sera na sheria mpya ya  gesi havijawa tayari.

Tunaamini kwamba wito huu haulengi kuzuia wawekezaji kuja nchini, ila unataka kuwako kwa mazingira mazuri ya kuwawezesha Watanzania wawe wadau wa maana katika miliki ya sekta ya gesi. Tunasema wadau kwa maana kuu moja, kumiliki sekta hii.

Haya yanawezekana tu kupitia sera na sheria za gesi asilia.
Tatizo kubwa la viongozi wa taifa hili hasa wanasiasa ni kudhani kwamba kwa kuwa tu wamekabidhiwa ofisi ya umma, basi wamegeuka kuwa waelewa wa kila kitu, kuwa na majibu ya matatizo yote na kuishia kufanya maamuzi ambayo huligharimu taifa mara nyingi. Mifano mingi ipo wazi.

Hatuelewi ni kwa nini hasa viongozi wetu wamekuwa na tabia ya kufanya vitu kwa kasi hii bila kuchukua hadhari katika kulinda na kutetea maslahi ya wananchi. Hatuelewi pia ni kwa nini viongozi wetu wanadhani kwamba njia pekee ya kuvutia wawekezaji ni kupuuza kilio cha wananchi.

Ni kuwafanya watazamani katika miliki na matumzi ya rasilimali za taifa lao. Hatuelewi pia ni kwa nini hatujifunzi hata kwa makosa yetu wenyewe.

NIPASHE ni mali ya The Guardian Limited, chini yake linaongozwa na sera inayochagiza pamoja na mambo mengine kuhamasisha uhuru wa vyombo vya habari, maendeleo ya taifa, ulinzi wa mazingira na maliasili.

Chini ya kipengele cha maliasili ni wajibu wetu kuendeleza ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi wa taifa kwa kuunga mkono matumizi bora ya rasilimali ya watu na maliasili.

Chini ya mazingira ni wajibu wetu kuhimiza sera ya maendeleo ya kudumu hasa kwa rasilimali ambazo haziwezi kurudishwa baada ya kutumika na tunahamasisha tabia na utamaduni wa kujitegemea katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa maliasili ya nchi kwa kuwaelemisha wananchi njia bora za kufanya hivyo.

Misimamo hii ilisimikwa tangu mwanzo wa uhai wa vyombo vya habari vya The Guardian Limited, ni nguzo ambazo tunazisimamia hadi sasa. Ni kwa jinsi hii tunashindwa kuelewa Waziri anakuwa na maana gani anapopuuza kilio cha wadau katika kuhakikisha kuwa sekta ya gesi asilia inanufaisha umma kwa kuwafanya Watanzania kuwa siyo washiriki wa hivi hivi tu bali wamiliki katika sekta hii ambayo itaongoza taifa hili kwa takribani miaka mingine 100 ijayo.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment