Ahmed Rajab
Toleo la 323
30 Oct 2013
Toleo la 323
30 Oct 2013
HAMNA shaka kwamba Rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya iliyopendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba ni hatua kubwa kwa Wazanzibari, hasa tukilizingatia pendekezo lake kuhusu muundo wa Muungano wa Tanzania. Hata hivyo Rasimu hiyo bado haikuwafikisha kule watakako kwenda.
Pendekezo kuhusu muundo wa Muungano linataka pawepo serikali tatu — ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya tatu itayokuwa serikali ya aina ya Shirikisho. Kuna wakati, lakini wakati huo sasa umepitwa na wakati, ambapo wengi wa Wazanzibari wangelifurahia pendekezo hilo la Muungano wa Serikali Tatu. Si leo.
Leo ukizungumza na wengi wa Wazanzibari, hususan vijana, wa vyama vyote vya siasa na wasio na vyama, utathibitisha kwamba wanataka Zanzibar irejeshewe mamlaka yake kamili.
Je, hili litapatikana katika Rasimu ya pili ya Katiba?
Tukiangalia Rasimu ya kwanza tutaona ya kwamba mambo saba yaliyopendekezwa yawe ‘Mambo ya Muungano’ hayatoufanya Muungano wetu uwe Muungano wa Mkataba.
Miongoni mwa mambo hayo ni mambo ya nje, ulinzi na usalama, uraia na uhamiaji, usajili wa vyama vya siasa, sarafu na mabenki, na kodi.Mambo hayo, kama nilivyokwishagusia, hayatoleta Muungano wa Mkataba, uliopendekezwa na zaidi ya asilimia 65 ya Wazanzibari katika vikao mbalimbali vya mchakato wa kuandika Katiba mpya, vikiwemo vile vya mabaraza ya Katiba.
Inavyoonekana ni kwamba pendekezo hili halikubaliwi na viongozi wa Tanganyika. Kwa hivyo, Rasimu ya pili kama haitofanyiwa mabadiliko ya msingi katika Bunge la Katiba ili kukidhi madai ya Wazanzibari itasababisha kupatikana kwa Katiba ya mpito tu ya kufikia matilaba ya Wazanzibari. Kwa hali hii itabidi kampeni za uteteziwa mamlaka kamili kwa Zanzibar ziendelee ili Zanzibar iweze hatimaye kupata mamlaka yake yote chini ya Muungano wa Mkataba.
Hata hivyo, hatuwezi kusema ya kwamba kazi iliyofanywa na Tume ya Marekebisho ya Katiba haina maana. Lakini kwa upande wa Zanzibar kazi hiyo haitoshi. Ni dhahiri ya kwamba suala hili la kuipatia Jamhuri ya Muungano Katiba mpya bado halijamalizika kwani hivi sasa kuna mazungumzo yanayoendelea ndani ya Tume ya Katiba yenyewe, kati ya vyama vya siasa na miongoni mwa wananchi.
Kwa hivyo, Tume ina fursa kubwa katika kuitayarisha Rasimu ya Pili kuifanya iwe na mfumo muwafaka utakaoleta Muungano wa kudumu.
Mfumo unaopendekezwa hivi sasa wa serikali tatu ni muhimu sana. Lakini lililo muhimu zaidi ni madaraka ya serikali hizo tatu kuliko idadi ya serikali zenyewe. Kwanza, si sawa kuiita serikali ya tatu ‘Serikali’. Haistahili kuitwa ‘Serikali’ kwa sababu itashughulikia mambo saba tu ambayo yanaweza kupunguzwa katika Rasimu ya pili yakawa manne au matano. Kwa hivyo, muundo unaofaa zaidi ni kama ule wa Muungano wa Ulaya ambao hauna Serikali inayozisimamia serikali zote za Muungano lakini una ‘Tume’.
Tukiichambua zaidi Rasimu ya Kwanza tutaona kuwa kimsingi Serikali ya Muungano, kisheria na kimuundo, itakuwa na mamlaka katika mambo yake kuliko Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar. Hali hii inathibitisha msemo wa watu wengi Zanzibar ya kwamba maoni yao ya kutaka mamlaka kamili ya Zanzibar hayakutiwa maanani na Tume ya Katiba katika kuitayarisha Rasimu iliyoiwasilisha kwa wananchi.
Kwa hali hii Bunge la Katiba, hasa wawakilishi wake kutoka Zanzibar, lina jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba madaraka kamili yanarejeshwa Zanzibar na Katiba mpya au tuseme Mkataba mpya kwa sababu zoezi la kuandika katiba linavyokwenda inaonyesha kinachoandikwa ni ‘Mkataba’ na si ‘Katiba’.
Tukichambua zaidi tutaona ya kwamba Serikali ya Muungano ndiyo itayoiwakilisha Tanzania – yaani Tanganyika na Zanzibar — kwenye ukumbi wa kimataifa. Kwa hali hii, ni wazi ya kwamba serikali za nchi hizo mbili hazitokuwa na mamlaka ya dola huru hasa ukichukulia kwamba marais wote watatu — wa Muungano, wa Tanganyika na wa Zanzibar —watachaguliwa moja kwa moja na wapiga kura.
Utaratibu huo ni kinyume cha taratibu za Miungano ya nchi huru ambapo serikali ya shirikisho huwa haiitwi serikali yenye mamlaka na madaraka kamili bali huwa Tume inayoongozwa na nchi wanachama wa shirikisho. Na Rais wake huwa hachaguliwi bali huteuliwa na nchi zilizo katika shirikisho hilo.
Katika kipindi hiki cha mpito mpaka Tanganyika na Zanzibar zitapopata mamlaka yao kamili ni wazi kwamba kunaweza kukazuka migogoro ya kikatiba. Kwa mujibu wa mfumo unaopendekezwa na Rasimu ya kwanza ya Katiba serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa ndiyo yenye uamuzi wa mwisho.
Je, serikali hiyo katika kuendeleza shughuli zake itasimamia kikamilifu maslahi ya Zanzibar kinyume na uzoefu wake wa miaka 50 ya mfumo wa hivi sasa wa ‘serikali mbili, nchi moja’? Tusisahau kuwa mfumo huo umeleta madhara makubwa kwa Zanzibar kiasi ya kwamba Zanzibar ni moja ya visiwa duniani ambapo wananchi wake wengi wao hawana ajira na ijapokuwa hakuna njaa inayosababisha vifo lakini ipo njaa iliyoenea chini kwa chini na shida zisizokwisha.
Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyowafanya Wazanzibari wa itikadi zote za kisiasa wasimame imara katika mchakato huu wa kutafuta Katiba mpya katika kugombania haki ya Zanzibar na uhuru wake.
Huko usoni twendako itabidi uwepo ushirikiano wa dhati baina ya Tanganyika na Zanzibar hasa kuhusu maendeleo ya watu wa nchi hizi mbili na uwiano wa sera mbalimbali ili pasizuke mushkil na migogoro ambayo hayatomsaidia mtu yeyote bali italeta balaa na shida kwa nchi hizi mbili.
Kwa mantiki hii, ukichukulia uchumi wa Tanganyika na uchumi wa Zanzibar katika miaka 50 ya Muungano utaona wazi kwamba ule wa Zanzibar umedhoofika na wa Tanganyika umeendelea. Haya ni matokeo ya mfumo wa Muungano wa ‘Mambo 22’ au ‘Mambo 38’, kama wanavyoyahesabu wengine, ambayo mengi yao yanahusiana na uchumi na ustawi wa jamii.
Kwa karne nyingi Zanzibar imekuwa taifa la wafanya biashara. Kwanza ilikuwa na biashara ya karafuu na nazi. Leo haina kitu. Ijapokuwa kuna matumaini ya mafuta na gesi asili kupatikana, itachukua muda mrefu sana kabla ya natija kupatikana Zanzibar kutokana na rasilmali hiyo. Kwa hali hiyo itategemea zaidi, mipango na sera za serikali ya Zanzibar katika nyanja za uchumi hasa katika sekta ya biashara, viwanda, teknlojia ya habari na mawasiliano (ICT).
Swali ni kwamba, je, Rasimu ya Pili itaipa Zanzibar mamlaka na madaraka ya kujiandaa kama soko huru au visiwa huru kiuchumu ambalo ni suluhisho pekee kwa matatizo yake ya kiuchumi na ustawi wa kijamii.
Ni wazi kwamba Tume na wadau wote wanaohusika na mchakato huu bado wana kazi kubwa ya kuifanya. Na itakuwa makosa makubwa kuliharakisha jambo muhimu kama hili ambalo linatokea kwa mara ya mwanzo baada ya miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano.
Nilisema hapo awali kwamba Katiba itayoibuka inawezekana ikawa Katiba ya mpito. Swali linaloibuka hapa ni hili, je, mpito huo utakuwa mpito wa miaka mingapi? Au utakuwa mpito wa miaka mingine 50 kama wanavyosema baadhi ya watu kwamba wanataka Katiba ya kudumu kwa muda huo.
La muhimu zaidi ni iwapo Tume ya Katiba, hasa wawakilishi wake 15 kutoka Zanzibar, watafanya kazi kuhakikisha kwamba Zanzibar baada ya 2015 inaweza kuweka mikakati ya kujiibua kutoka dhiki zisizokwisha wanazozikabili wananchi wake kila siku katika hali ambayo huduma zote za serikali za Zanzibar haziridhishi.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/rasimu-ya-katiba-si-kwamba-haina-maana-lakini-haitoshi#sthash.91p1zJSf.dpuf
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/rasimu-ya-katiba-si-kwamba-haina-maana-lakini-haitoshi#sthash.91p1zJSf.dpuf
No comments :
Post a Comment