NA MWANDISHI WETU
31st October 2013
Maslahi hayo ni pamoja na mishahara, posho na mengine yanayohusisha wasaidizi wa wabunge.
Pia wanadaiwa kuilalamikia kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, ya kuzungumzia hadharani hali mbaya ya maisha ambayo huwakabili wabunge wanapostaafu au vipindi vyao vya ubunge vinapokoma na kushindwa kuchaguliwa tena kuwa wabunge.
Walifikia hatua hiyo katika kikao cha wabunge cha kupewa taarifa za shughuli za Mkutano wa 13 wa Bunge unaoendelea hivi sasa.
Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa, mjini hapa juzi jioni chini ya uenyekiti wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha, anayemwakilisha Waziri Mkuu, ambaye kikanuni za Bunge ndiye Kiongozi Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya kikao hicho kililieleza NIPASHE kuwa aliyeibua hoja kuhusu uduni wa maslahi ya wabunge, ni Mbunge mmoja wa Viti Maalumu (Chadema).
Kwa mujibu wa chanzo hicho, mbunge huyo katika hoja yake, pamoja na mambo mengine, alisema umefika wakati kwa serikali kutafakari upya kuhusu maslahi duni wanayopata wabunge na kuangalia uwezekano wa kuyaboresha.
Alisema maslahi wanayopata wabunge wa Tanzania ni duni kulinganisha na yale wanayopata wabunge wenzao wa mabunge mengine duniani.
Chanzo hicho kilisema hoja ya mbunge huyo iliibua madukuduku yaliyoonekana kuwa kwa wabunge wengi muda mrefu kuhusiana na suala hilo.
Kilisema sehemu kubwa ya wabunge waliopata fursa ya kuchangia katika kikao hicho, waliunga mkono hoja hiyo mkono kwa uzito mkubwa.
“Hali hiyo ilifanya kikao chote kutawaliwa na mjadala kuhusu kuboreshwa kwa maslahi ya wabunge,” kilieleza chanzo chetu kutoka ndani ya kikao hicho.
Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa hadi kikao hicho kinafungwa, hakuna kilichoeleweka kutoka kwa serikali kama itatekeleza madai ya kuhusu kuboresha maslahi yao au la.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, jambo lingine lililolalamikiwa na wabunge katika kikao hicho ni kauli ya Spika Makinda ya kuzungumzia hadharani hali mbaya ya maisha, ambayo huwakabili wabunge wanapostaafu au vipindi vyao vya ubunge vinapokoma na kushindwa kuchaguliwa tena kuwa wabunge.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, katika malalamiko yao, wabunge walisema kauli hiyo ya Spika Makinda imewadhalilisha wabunge.
Makinda mwenyewe hakuwapo katika kikao hicho, kutokana na kuwa mkoani Njombe katika mazishi ya Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Njombe, Mhashamu Raymond Mwanyika. Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alihudhuria.
Hoja kuhusu maslahi duni wanayopata wabunge, imetolewa siku nane baada ya Spika Makinda kutamka kwamba mishahara wanayolipwa wabunge wa Tanzania siyo mikubwa kulinganisha na ile wanayolipwa wabunge wa mabunge mengine duniani.
Spika Makinda alitoa kauli hiyo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka ufafanuzi kuhusu kauli yake juu ya mpango wa Bunge wa kuwaokoa wabunge dhidi ya hali mbaya ya maisha, ambayo huwakabili wanapokuwa wamestaafu ubunge.
Kauli kuhusu mpango wa Bunge kuwaokoa wabunge wastaafu dhidi ya hali mbaya ya maisha, ambayo huwakabili, ilitolewa na Spika Makinda, wakati wa mazungumzo kati yake na Spika Rais wa Bunge la Uswisi, Maya Graf, alipotembelea ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, Oktoba 23, mwaka huu.
Katika ufafanuzi wake, Spika Makinda aliitaja mishahara wanayolipwa wabunge katika orodha ya sababu zinazochangia hali mbaya ya maisha kuwakabili wanapostaafu ubunge.
Sababu mojawapo aliitaja kuwa ni mabadiliko ya malipo kwa wabunge baada ya kumaliza kipindi chao cha ubunge au kustaafu kazi hiyo, yaliyofanywa katika kipindi cha Bunge lililoshirikisha vyama vingi vya siasa nchini, kuanzia mwaka 1995.
Alisema katika kipindi chote cha Bunge lililokuwa na wabunge kutoka chama kimoja cha siasa (CCM), kulikuwa na utaratibu wa kuwalipa pensheni wabunge wanaostaafu ubunge.
Lakini alisema utaratibu huo uliondolewa baadaye baada ya Bunge la vyama vingi vya siasa kuanza mwaka 1995.
Alisema baada ya Bunge hilo kuanza, uliwekwa utaratibu mpya, ambao wabunge wanaomaliza kipindi chao cha ubunge au kustaafu kazi hiyo hulipwa kiinua mgongo au bahashishi (gratuity).
Alitaja sababu nyingine inayochangia wabunge wastaafu kukabiliwa na hali mbaya ya maisha kuwa ni mishahara midogo wanayolipwa wakati wakiwa kazini.
Alisema licha ya mishahara ya wabunge kutokuwa mikubwa kulinganisha na ile wanayolipwa wabunge wa mabunge mengine duniani, pia hutakiwa katika kile kidogo wanacholipwa wachangie majimboni.
Wakati wabunge hao wakilalamikia maslahi madogo, mbunge mmoja hulipwa mshahara wa Sh. milioni 11 kwa mwezi.
Hiyo ni mbali na posho ya Sh. 330,000 anayolipwa mbunge kwa kuhudhuria kikao kimoja kwa siku. Posho ni Sh. 80,000 za kujikimu akiwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao Sh. 200,000 kwa siku na mafuta ya gari Sh. 50,000, jumla kuwa Sh. 330,000 kwa siku.
Aidha, mbunge mmoja hulipwa ‘gratuity’ (kiinua mgongo au bahashishi) ya Sh. milioni 72 baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka mitano cha ubunge.
Posho ya Sh. 330,000 anayolipwa mbunge kwa siku inazidi kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa serikali wa Sh. 150,000 kwa mwezi.
Aidha, wabunge hupewa fedha za Mfuko wa Jimbo Sh. milioni 30 kila mwaka kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo katika majimbo yao.
Serikali hadi sasa imeshindwa kuongeza kima cha chini kufikia Sh. 350,000
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment