Mkuu wa
Mkoa wa Tanga, Luteni mstaafu Chiku Gallawa, amesema watu waliomuua askari
mgambo Salum Mgonje na kumpiga risasi Mkuu wa Kituo cha Polisi Songe, wilayani
Kilindi Edward Lusekolo ni kikundi kilichokuwa kinaishi msituni.
Alisema
kikundi hicho kinaipinga Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na kudai ni ya
kikafiri kikiwa na mipango ya kutaka Tanzania isitawalike.Akizungumza na
waandishi wa habari Mjini Handeni, Bi. Gallawa alisema kikundi hicho kiliweka
kambi tatu wilayani humo kikifanya mafunzo mbalimbali yakiwemo ya kijeshi.
“Pia
kikundi hiki ndicho kilichokuwa kikipinga mchakato wa sensa mwaka 2012, kambi
zao tatu zilikuwa katika Kata ya Lwande na Negero kwenye Kijiji cha
Madina.“Katika kambi ya Madina, wafuasi wao wawili wameuawa baada ya kupinga
kitendo cha kukamatwa na askari Oktoba 26 mwaka huu wakijiita wafuasi wa
Sunni,” alisema.
Aliwataja
wafuasi waliouawa kuwa ni Ramadhan Hamis, ambaye ni mfanyabiashara wa madini na
mwingine jina lake halikufahamika mara moja lakini inasemekana ni mwalimu wa
dini ya Kiislamu (ustaadh) Kijiji cha Lwande.
Aliongeza
kuwa, kikundi hicho kimekutwa na bunduki tatu aina ya gobore, shortgun moja,
bastola mbili zilizotengenezwa kienyeji, mapanga 18 na visu 10. Bi.
Gallawa alisema wafuasi 46 wa kikundi hicho tayari wamekamatwa lakini jambo la
kushangaza wamo watumishi wa Serikali ambao ni walimu wa shule za msingi na
watafikishwa mahakamani wakati wowote.
Kamati ya
Ulinzi na Usalama Mkoa, ambayo inaongozwa na Bi. Gallawa, imeamua kuweka kambi
Kilindi kwani hivi sasa hali ya usalama si nzuri hadi
itakapotulia. Akizungumza na Majira hivi karibuni, Kamanda wa Polisi
mkoani humo, Constantine Masawe, alisema askari mgambo Salum Mgonje aliuawa
Oktoba 22 mwaka huu ambapo Edward alipigwa risasi za mbavu na mkononi Oktoba
23, saa mbili usiku.
Kikundi hicho
kinajumuisha wakazi wa vijiji mbalimbali wilayani humo ambao wamefukuzwa na
wenzao kutokana na tabia zao za kupinga mambo mbalimbali ya
maendeleo. Chanzo cha kuanzishwa kikundi hicho ni baada ya mwenzao mmoja
ambaye ni mfanyabiashara kutakiwa kulipa ushuru katika Kijiji cha Lwande na
kukataa hivyo mgambo waliingilia kati ndipo wafuasi wao walichukua uamuzi wa
kwenda kuwakata mapanga mgambo ambao mmoja alijeruhiwa na mwingine kuuawa.
No comments :
Post a Comment