Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
anaondoka Nchini leo jioni kuelekea Washington kuhudhuria Mkutano wa
15 wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye asili ya Afrika ya Kaskazini
Magharibi mwa Picific unaotarajiwa kufanyika katika Jimbo la Seattle Nchini
Marekani.
Balozi Seif amepata heshima hiyo kufuatia ujumbe wa Jumuiya ya
Wafanyabiashara wenye asili ya Afrika kutoka Marekani uliowahi
kufanya ziara hapa Zanzibar kati kati ya mwezi wa April Mwaka huu na kujionea
mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo Zanzibar imepatiwa fursa ya kwenda
kujitangaza Nchini humo.
Mtandao wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye asili ya Afrika
Nchini Marekani umeamua kufungua ukurasa mpya katika kuona inaendeleza
mashirikiano na Nchi rafiki ikilenga kusaidia taaluma na hata uwezeshaji kwa
Taasisi na Mashirika Barani Afrika ili yajinyanyue kiuchumi.
Katika ziara hiyo ya wiki moja ya Kiserikali itakayotoa pia
fursa ya kutembelea baadhi ya Makampuni na Taasisi za Umma, Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar anauongoza ujumbe wa Viongozi saba wa Serikaliwakiwamo
Mawaziri, Watendaji wa serikali na Maafisa waandamizi.
Viongozi anaofuatana nao ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud
Mohammed, Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Mh. Nassor Ahmed Mazrui pamoja
na Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Mh. Hamza Hassan Juma.
Wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha wafanyabiashara Zanzibar
Abdulla Abass, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na
Nishati Ali Khalil Mirza, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Abdulla
Mzee Abdulla,Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bahari Kuu Zahor Mohammed El-
Kharousy pamoja na timu ya wafanyabiashara wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake
akiambatana na baadhi ya wafanyabaiashara maarufu hapa Zanzibar atapata fursa
ya kutembelea Kampuni ya utengenezaji wa ndege za Abiria na mizigo ya Boeing
Mjini Seattle, kukutana na Uongozi wa Mfuko wa misaada wa Melinda Gates na ule
wa Microsoft pamoja na jumuiya ndogo ndogo za wafanyabiashara.
Maeneo mengine watakayopata fursa ya kutembelea ni ni baadhi ya
Taasisi za Serikali, Meya wa Jiji la Seattle ziara iakayoambatana pia na vikao
na Mikutano ya Wafanyabiashara wa Zanzibar na Mji huo katika kubadilishana
mawazo na kuanza kupanga mikakati ya ushirikiano.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amepanga kukutana na
Wanachama wa Jumuiya ya Wazanzibari na Watanzania wanaoishi Mjini Seattle na
Washington kwenye Tafrija maalum waliyojipanga kumuandalia yeye na ujumbe wake
aliofuatana nao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif anatarajiwa
kukamilisha ziara yake Mjini Seattle Nchini Marekani Mnamo Tarehe 14 Novemba
2013 na kurejea nyumbani kwa kupitia Dubai.
Mapema asubuhi kabla ya kuondoka Nchini kuelekea Marekani
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Balozi
Mdogo mpya wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Bwana Xie Yunliang ambae
alifika kujitambuluisha rasmi.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar Viongozi hao walielezea haja ya pande hizo
mbili kuendelea kushirikiana katika miradi ya maendeleo China ikiwa mshirika
mkubwa wa Zanzibar katika uimarishaji uchumi na ustawi wa Jamii.
Balozi Xie Yungliang alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba China itaendelea kuunga mkono harakati z maendeleo za Zanzibar
katika kujiletea maendeleo na kupunguza umaskini.
Alisema China ilitenga zaidi ya Yuan Milioni Mia moja katika
kuunga mkono miradi ya Skuli, awamu ya Pili ya ujenzi wa uwanja wa ndege bwa
Kimataifa wa Zanzibar Kisauni pamoja na ile awamu ya Pili ya mradi wa Mkongo wa
Mawasiliano hapa Zanzibar.
Naye akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif aliipongeza Jamuhuri ya Watu wa China kwa jitihada
zake za makusudi za kuona Zanzibar inajikwamua kutoka katika wimbi
la umaskini.
Balozi Seif alimuahidi Balozi huyo Mdogo mpya wa Jamuhuri ya
Watu wa China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kumpa
ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa majuku yake aliyopamngiwa na Nchi
yake.
Baadaye Balozi Seif pia alifanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa
Oman hapa Zanzibar Bwana Saleh Suleiman Al - Harith ambae naye
alifika kujitambulisha bada ya kuteuliwa na Nchi yake kufanya kazi ya
Kidiplomasia hapa Zanzibar.
Mazungumzo yao yalijikita zaidi katika kuendeleza uhusiano na
ushirikiano uliopo kati ya Nchi hizo ambao ni wa kihistoria kutokana na
maingiliano ya kidamu ya wananchi wa pande hizo mbili.
Balozi Seif alimueleza Balozi Mdogo wa Oman Nchini kwamba
Zanzibar Zanzibar inahitaji kuwa na viwanda vidogo vidogo hasa vya matunda
ilikuweza kusaidia uchumi wake.
Alisema wananchi wengi hasa wakulima wamekuwa wakizalisha idadi kubwa
ya matunda ambayo baadaye hupotea na kuleta hasara kutokana na wakulima hao
kukosa utaalamu wa hifadhi ya matunda hayo.
Aliipongeza Oman kwa misaada yake mikubnwa inayoendelea kutoa
kwa Zanzibar katika Nyanja za za maendeleo ambayo inazidi kuimarisha uhusiano
uliopo kati ya mataifa hayo mawili.
Naye kwa upande wake Balozi mdogo wa Oman hapa Zanzibar
Bwana Saleh Suleiman Al –Harith amewapongeza Viongozi na Wananchi wa Zanzibar
kwa ushirikiano waliompa uliomuwezesha kutekeleza majukumu yake
vizuri katika kipindi kifupi cha utumishi wake.
Balozi Saleh
alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
kwamba lile ombi la Zanzibar la kutaka mkutano wa ushirikiano wa
wafanyabiashara wa Nchi za Ghuba Oman ikiwa mratibu atalifikisha katika ngazi
zinazohusika wakati ataporejea Nchini mwake.
Chanzo: ZanziNews
No comments :
Post a Comment