NA MHARIRI
1st November 2013
Tukio hilo lilitokea baada ya majambazi kuvamia gari na kumteka Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni ya Ujenzi ya Dott, Shuresh Bab (45), na kutokomea na fedha hizo.
Katika tukio hilo lililotokea juzi asubuhi, liliacha maswali mengi ambayo hata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, hakuwa na majibu.
Hiyo ni kutokana na uamuzi wa kampuni hiyo kuhamisha kwa gari lisilo na aina yoyote ya ulinzi kiasi hicho cha fedha kutoka Benki ya Standard Chartered Tawi la Moshi kuzipeleka Benki ya NMB Tawi la Mandela.
Waporaji hao wanaodaiwa kuwa wawili, wanaelezwa kuwa walikuwa na silaha za moto.
Hata hivyo, katika tukio zima la uporaji hadi majambazi hayo kufanikiwa kuondoka na fedha hizo, hakuna risasi hata moja iliyofyatuliwa katika makutano ya barabara ya Arusha na Old Boma mjini Moshi.
Taarifa zilieleza kwamba majambazi hayo yaliyokuwa kwenye pikipiki, yaliteka gari la Bab lililokuwa limechukua fedha hizo.
Ilielezwa kwamba baada ya majambazi hayo kuliteka gari hilo, Bab aliwazidi nguvu na kuruka kutoka katika gari hilo kisha akakimbia kuelekea barabara kuu inayopita mkabala na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na kutoa taarifa. Hata hivyo, taarifa zilisema hakuna risasi hata moja iliyofyatuliwa wakati Bab akifurukuta kuwatoroka majambazi hayo na kukimbia.
Baada ya kutoa taarifa, polisi walifika eneo la tukio na kulikuta gari alilokuwa mkurugenzi huyo likiwa limetelekezwa katika Mto Karanga ndani yake kukiwa na wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya Dott waliokuwa wametekwa pamoja na mkurugenzi wao.Wafanyakazi hao walikuwa salama, hakuna aliyejeruhiwa.
Kamanda Boaz alisema polisi walifanikiwa kuokoa zaidi ya Sh. milioni 80 kati ya Sh. milioni 220 ikimaanisha kwamba majambazi hayo yalifanikiwa kutoroka na Sh. milioni 140.
Kamanda Boaz alifafanua kuwa Mkurugenzi na wafanyakazi wa kampuni ya Dott walitekwa na kuporwa fedha hizo wakiwa njiani kuelekea katika benki ya NMB tawi la Mandela wakiwa katika gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin yenye namba za usajili T 864 AZM.
Alisema wakiwa njiani kuelekea katika benki hiyo, ghafla ilipita pikipiki ikiwa na watu wawili na kusimama mbele na kumwamuru dereva wa gari hilo, Wenslaus Mambo (32), asimame na baadaye wakamwamuru abadili mwelekeo.
Kufuatia tukio hilo, watu wawili wanashikiliwa na uchunguzi wa Sh. milioni 140 ambazo hazijapatikana unaendelea kufanyika.
Kamanda huyo alipoulizwa sababu za mkurugenzi huyo kuchukua kiasi kikubwa cha fedha taslim benki kinyume cha sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayoelekeza kwamba malipo yoyote yanayozidi Sh. milioni 10, lazima yafanyike kwa njia ya benki (interbank money transfer), alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi.
Pia alipoulizwa sababu za kutokukamatwa kwa mkurugenzi huyo kwa kukiuka sheria hiyo, alisisitiza kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi.
Kinachotushangaza sisi, ni taratibu zilizotumika za kuhamisha kiasi hicho kikubwa cha fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine tena pasipo ulinzi wa aina yoyote. Lakini pia BoT ilikwishatoa mwongozo wa namna ya uhamishaji wa fedha, njia tunayoamini kwamba kama ingetumika, fedha hizo zingekuwa salama.
Tunapoliangalia tukio hili la ujambazi, kwa hakika tunajiuliza maswali mengi yasiyo na majibu kama ilivyokuwa kwa Kamanda Boaz mwenyewe.
Tukio hili pia linafanana na matukio mengine yaliyokwisha kutokea siku za nyuma ya kampuni, taasisi ama watu binafsi kuporwa fedha na majambazi wanapopeleka benki ama wanapotoka kuchukua kutoka benki.
Mara kdhaa, Makamanda wa Polisi, wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa taasisi, kampuni ama watu binafsi, kuomba ulinzi wa polisi pale wanapoleka benki kiasi kikubwa cha fedha ama wanapokwenda benki kuchukua fedha nyingi.
Hata hivyo, licha ya msisitizo wa makamanda hao wa polisi, bado baadhi ya kampuni, taasisi ama watu binafsi hupuuza ama kwa makusudi au kwa sababu wanazozijua wenyewe.
Tunazidi kusisitiza kwamba kampuni, taasisi na watu binafsi wanapotaka kuchukua kiasi kikubwa cha fedha ama kupeleka benki, wazingatie maagizo ya makamanda wa polisi pamoja na BoT.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment