NA MUHIBU SAID
9th November 2013
Wakijadili Muswada wa Sheria hiyo jana, Wabunge walikataa mapendekezo ya serikali yaliyotaka adhabu ya faini kwa makosa ya kuchapisha habari ya uchochezi na uvunjifu wa amani, iongezwe kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. milioni tano.
Badala yake, limeitaka serikali kupeleka bungeni marekebisho ya kipengele kimoja tu cha Sheria ya Magazeti Namba Tatu ya Mwaka 1976, ipeleke Muswada mzima wa Sheria ya Vyombo vya Habari ili ujadiliwe na kupitishwa na Bunge.
Mapendekezo ya nyongeza ya adhabu hiyo, yaliingizwa na serikali kwenye sheria hiyo, ambayo ni kati ya sheria 14, zilizokuwamo kwenye Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2013.
Muswada huo uliwasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, bungeni Jumatano wiki hii na kupitishwa na Bunge jana.
Uamuzi wa kuyakataa mapendekezo hayo ya serikali, ulifikiwa na Bunge wakati lilipokaa kama Kamati ya Bunge zima kupitia vifungu mbalimbali vya muswada huo kwa ajili ya kuupitisha muswada huo.
Kabla ya Bunge kupiga kura ya sauti na kuamua hilo, wa mwisho ‘kumpiga mweleka na kumwangusha chali’ Jaji Werema, alikuwa ni Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Makinda akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge zima, alikataa ushauri uliotolewa na Jaji Werema aliyetaka zipigwe kura za vidole badala ya sauti ili kuamua ama kuyakubali mapendekezo hayo au kuyakataa.
Alisema hakuna haja ya kupiga kura ya vidole, kwa kuwa ni muda mrefu sasa serikali imekuwa ikifanya utani kupeleka Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari bungeni.
“Eneo tunalofanya utani ni katika eneo hili (la vyombo vya habari). Kila siku tumeambiwa leteni muswada (wa sheria ya vyombo vya habari),” alisema Makinda.
Awali, Makinda alisema hata yeye pia anataka muswada huo upelekwe bungeni.
Alitoa kauli hiyo akiunga mkono hoja zilizotolewa kwa nyakati tofauti Jumatano wiki hii na jana na Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, ambaye aliomba pia wabunge wamuunge mkono.
Hoja hiyo ya Serukamba iliungwa mkono na wabunge wenzake; Jenista Mhagama (Peramiho-CCM), Ester Bulaya (Viti Maalumu-CCM) na Martha Mlata (Viti Maalumu-CCM).
Awali, mapendekezo hayo ya serikali yalipingwa vikali na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kupitia maoni yake kuhusu muswada huo, yaliyowasilishwa bungeni Jumatano wiki hii na Msemaji wake wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu.
Serukamba alisema haungi mkono mapendekezo hayo ya serikali kwa kuwa inalenga kuukandamiza upande mmoja wa waandishi wa habari.
Alisema haoni sababu kwa serikali kupeleka kipengele kimoja badala ya kupeleka muswada mzima ambao umekuwa ukidaiwa kupelekwa bungeni zaidi ya miaka minane sasa, lakini haijawahi kufanya hivyo.
Naye Mhagama alipigilia msumari wa mwisho kwa kusema inasikitisha kuona serikali inakuja na mapendekezo ya kuweka adhabu kwa wana habari wakati Bunge limekuwa likipiga kelele kutaka muswada huo upelekwe, lakini haijafanyika hivyo.
“Naishangaa serikali kuna tatizo gani la kuwa na kigugumizi katika kuleta muswada wa sheria bungeni,” alisema Mhagama.
Alisema wamepita mawaziri; George Mkuchika na Dk. Emmanuel Nchimbi, katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa miaka mingi, lakini muswada huo haujawahi kupelekwa bungeni.
“Mimi sikubaliani na marekebisho ya sheria hiyo, bali nataka iondolewe ili muswada wa sheria ya habari uletwe hapa bungeni,” alisema Muhagama.
Awali, Lissu akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu muswada huo, alisema mapendekezo hayo hayana msingi kwa kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha adhabu zilizoko katika baadhi ya vifungu vyake vilivyopendekezwa na serikali kuongezwa, kama vimeshindwa kudhibiti makosa ya uchochezi.
Pia alisema ni aibu kwa serikali kuendeleza Sheria ya Magazeti, ambayo ilitumika kumtia hatiani Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere zaidi ya nusu karne iliyopita, huku ikijidai kumuenzi.
Muswada huo wa Sheria ya Magazeti, pamoja na mambo mengine ulipendekeza kufanya marekebisho ya vifungu vyake vya 36 (1) na 37(1) (b) kwa lengo la kuongeza adhabu ya faini kwa makosa ya kuchapisha habari, uvumi au taarifa za uongo zinazoweza kusababisha taharuki au hofu kwa wananchi, au zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani; au kuchapisha, kusambaza au kutoa taarifa ya uchochezi.
Katika marekebisho hayo, muswada huo ulipendekeza kuongezwa adhabu ya makosa hayo kutozwa faini kutoka Sh. 150,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja hadi Sh. 5,000,000.
Mbali na Sheria ya Magazeti, Jaji Werema alisema pia kuwa katika marekebisho ya Sheria ya Filamu na Michezo ya Maigizo, adhabu kwa mtu atakayetenda kosa ikiwamo kutoa filamu au mchezo wa kuigiza wenye lugha ya uchochezi imeongezwa kutoka faini ya Sh. 5,000 hadi Sh. 5,000,000.
Hata hivyo, Lissu alisema wanapinga marekebisho ya Sheria ya Magazeti kwa sababu kadri ya ufahamu wa kambi ya upinzani, tangu sheria hiyo ilipotungwa miaka zaidi ya 37 iliyopita, hakuna mwandishi wa habari au mchapishaji wa gazeti lolote aliyewahi kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia ya makosa hayo.
Alisema badala ya kuwapeleka wakosaji wa aina hiyo mahakamani wakaadhibiwe kwa mujibu wa sheria hiyo, serikali imejenga utamaduni wa kufungia magazeti na kutisha waandishi wa habari.
Lissu alisema hiyo peke yake inathibitisha hoja kwamba sheria hiyo ilitungwa kwa malengo ya kisiasa ya kudhibiti wakosoaji na wapinzani wa serikali na watawala na siyo kuzuia makosa ya jinai.
“Katika hili, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kwa Bunge lako tukufu, taarifa ya kesi zote– kama zipo- zilizofunguliwa mahakamani kuhusu ukiukwaji wa masharti ya vifungu vya 36 (1) na 37 (1) (b) vya Sheria ya Magazeti tangu Sheria hiyo ilipotungwa mwaka 1976,” alisema Lissu.
Pia aliitaka serikali itoe bungeni taarifa ya adhabu zozote za faini, kama zipo, zilizotozwa kwa mujibu wa vifungu hivyo ili Bunge lipime ukweli wa kauli yake kwamba adhabu hizo ni ndogo kulingana na ukubwa wa makosa yenyewe.
Alisema taarifa hizo zitaliwezesha Bunge kujadili na kufanya maamuzi ya busara kuhusu mapendekezo ya muswada huo, badala ya kufanya maamuzi kwa hisia na taarifa au kauli potofu kama za AG.
Lissu alisema miaka 22 iliyopita, Tume ya Jaji Francis Nyalali, iliwahi kusema kuwa sheria hiyo na ile ya Magazeti ya Zanzibar 1988 kwamba, zinakwenda kinyume cha Ibara ya 18 (1) ya Katiba zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar.
Alisema Tume hiyo pia ilisema sheria hizo zinawapa mawaziri mamlaka mengi na makubwa mno na kutolea mfano, namna mawaziri walivyo na uwezo wa kuagiza gazeti lisichapishwe tena.
Lissu alisema Tume hiyo iliendelea kusema kuwa sheria hizo pia hazitilii maanani umuhimu wa magazeti katika jamii kwamba ni moja ya vyombo muhimu vinavyotoa msukumo wa shughuli za umma.
Alisema hatimaye Tume hiyo ikapendekeza kuwapo sheria, ambazo zitayapa magazeti uhuru kamili bila ya kubanwa na chombo chochote cha dola.
“Tunapendekeza kuwa sheria inayohusu uhuru wa magazeti itengenezwe haraka iwezekanavyo, ikitilia maanani vilevile hali iliyopo sasa ya teknolojia ya magazeti,” aliinukuu Lissu Tume hiyo.
Hata hivyo, Lissu alisema kwa kipindi chote hicho, serikali imekataa kutekeleza mapendekezo ya Tume hiyo, badala yake, Tanzania imegeuka kuwa taifa lisilotaka watu kuhabarishwa vizuri juu ya matendo ya watawala.
“Tanzania imegeuka kuwa taifa linalofungia magazeti yanayofichua ufisadi, uchafu na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa viongozi, watendaji na watumishi wa Serikali hii ya CCM. Tanzania imegeuka, chini ya usimamizi wa Wizara na Serikali hii ya CCM, kuwa taifa linaloteka nyara wanahabari, kuwatesa kwa kuwang’oa kucha na meno, kuwatoboa macho, kuwamwagia tindikali na hata kuwaua,” alisema Lissu.
Alisema maneno hayo waliwahi kuyasema katika maoni yao kuhusu Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo na Vijana katika Mkutano wa Bunge la Bajeti, mwaka huu.
“Miezi mitatu haikupita tangu tuseme maneno haya kabla ya Serikali hii ya CCM kuthibitisha ukweli wake kwa kutumia Sheria ya Magazeti kuyafungia magazeti ya Mtanzania na Mwananchi,” alisema Lissu.
Mbali na Spika Makinda na wabunge hao, baadhi ya wabunge waliyaunga mkono mapendekezo hayo ya serikali, kwa madai kwamba, yanazingatia maslahi ya Taifa dhidi ya uchochezi unaofanywa na baadhi ya magazeti.
Wabunge hao ni Pindi Chana (Viti Maalumu-CCM), Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki-CCM), Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi-CCM) na Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala.
Awali, akiwasilisha muswada huo, Jaji Werema alisema marekebisho hayo ya sheria hiyo yanalenga kutekeleza azimio la Bunge katika Mkutano wake wa 11, kikao cha 21.
Alisema katika kikao hicho, Bunge liliazimia, pamoja na mambo mengine, kwamba serikali ipitie sheria zilizopo ili kuona kama zinatosheleza kuzuia lugha au kauli za uchochezi.
Alisema serikali imepitia Sheria ya Magazeti na kuona kuwa inazuia uchapishaji wa habari inayoweza kusababisha uchochezi au uvunjifu wa amani kama inavyoelezwa katika vifungu vya 36 na 37.
“Aidha, adhabu ya faini kwa makosa ya kuchapisha habari ya uchochezi au habari inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani chini ya vifungu hivyo ni Sh. 150,000,” alisema Jaji Werema na kuongeza:
“Kwa kuzingatia kuwa adhabu hiyo ni ndogo kulinganisha na madhara ya kosa husika katika jamii, muswada unapendekeza katika Ibara ya 40 na 41 kuwa vifungu hivyo virekebishwe kwa lengo kwa lengo la kuongeza adhabu ya faini kwa makosa hayo ili adhabu hiyo isizidi Sh. milioni tano.”
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment