Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, November 22, 2013

Hotuba ya Makamu wa Rais kwenye Mkutano wa Afro-Arab Kuwait

4133

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA TATU WA AFRIKA NA ARABIA, NCHINI KUWAIT, 20 NOVEMBA, 2013


Mfalme, Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah, Amiri wa nchi ya Kuwait na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa tatu wa Afrika na Arabia;
Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn,
Waziri Mkuu wa Ethiopia na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa tatu wa Afrika na Arabia;
Waheshimiwa Wafalme na Koo za Kifalme;
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali;
Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa nchi za Kiarabu;
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Mwanzo kabisa, nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe Mheshimiwa Mfalme Sheikh Sabah Al-Ahmad Sabah, Amiri wa nchi ya Kuwait, Serikali na wananchi wa Kuwait, kwa mapokezi mazuri na maandalizi makubwa mliyofanya ya kuandaa mkutano huu. Pili, niruhusu nitoe salamu kutoka kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye alipenda sana kuhudhuria mkutano huu, lakini hakuweza kufanya hivyo kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine ya kimataifa. Mheshimiwa Rais amenituma kuwasalimu na pia kuwaeleza kuwa anautakia mkutano huu mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Waheshimiwa Viongozi;
Nchi za Afrika na Arabia zinaunganishwa na mambo kadha wa kadha yakiwemo; historia, jiografia na utamaduni. Mahusiano yetu ya kihistoria na ukaribu wa kijiografia yametusaidia kuwasiliana kwa karne nyingi. Mawasiliano haya na mahusiano hayo, yamekuwa katika Nyanja za biashara, dini na tamaduni. Leo hii, theluthi mbili ya idadi ya wakazi wenye asili ya Arabia wanaishi Afrika. Nchini Tanzania, idadi kubwa ya wananchi wetu walio ughaibuni wanapatikana katika nchi za ukanda wa Arabia. Hakuna maeneo mengine nje ya Afrika ambapo lugha ya Kiswahili inazungumzwa kwa ufasaha kama ilivyo kwa nchi za Oman na Yemen. Hizi ni baadhi ya sababu zinazochangia kufanya ushirikiano baina yetu kuwa wa lazima.
Kama ambavyo tunaelewa, mkutano wa pili wa Afrika na Arabia uliofanyika Libya mwaka 2010 uliazimia mambo mengi ya msingi yaliyolenga kukuza na kutanua uhusiano baina ya kanda zetu hizi mbili. Kwa leo nitazungumzia kupitishwa kwa mkakati Kazi wa Afrika na Arabia yaani (Africa-Arab Strategic Framework and its Joint Plan of Action wa mwaka 2011 – 2016. Mkakati huu ulibainisha maeneo manne ya mashirikiano ambayo ni: ushirikiano wa kisiasa na uchumi, biashara na mtaji, kilimo na chakula na mahusiano ya kijamii na kitamaduni.
Ndugu Waheshimiwa;
Ni miaka mitatu sasa tangu tuanze kutekeleza mpango wa utekelezaji wa Pamoja kwa nchi za kanda hizi na ripoti zilizowasilishwa katika mkutano huu leo, zinaonesha bila kuficha yale tuliyofanikiwa kuyatekeleza. Miradi mingi ya Maendeleo iliyopitishwa haijaanza kutekelezwa na baadhi ndiyo iko katika hatua za awali ambapo hali hii imetokana na sababu mbalimbali. Ripoti ya pamoja ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) na ile ya Sekretarieti ya Umoja wa nchi za Kiarabu imeeleza kwa kina sababu zilizochangia kutotekelezwa kwa miradi mbalimbali iliyopangwa. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na; ukosefu wa fedha za uendeshaji, kutokuwepo mkakati wa ukaguzi na kushirikisha kwa kiwango cha chini sekta binafsi. Ukitazama changamoto hizi, nyingi ziko chini ya uwezo wetu na kupitia ushirikiano huu tunaweza kabisa kuzikabili katika kipindi tunachoweza kujiwekea.
Ndugu Waheshimiwa;
Wote tunafahamu kuwa dunia inapitia changamoto mbalimbali zikiwemo: athari za mdororo wa uchumi, upungufu wa chakula, majanga yanayotokana na hali ya hewa, kutokutangamaa kwa baadhi ya nchi sambamba na suala la ugaidi. Changamoto hizi ni kubwa na ngumu ambazo haziwezi kukabiliwa na taifa moja peke yake. Kutokana na hali hii, kunahitajika mashirikiano baina ya nchi za Afrika na Arabuni katika kipindi hiki kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Kwa kuwa na mashirikiano haya, kanda zetu hizi zitakuwa hazizungumzii tu changamoto zilizopo, bali pia zitaweza kukabiliana na changamoto hizo kwa kutumia fursa zilizopo na hivyo kufanikisha matakwa ya wananchi wa kanda hizi.
Nakushukuruni sana kwa Kunisikiliza!
 
Chanzo: ZanzibariYetu

No comments :

Post a Comment