zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, November 11, 2013

Maadui wa uhuru wa habari

NA WAANDISHI WETU

11th November 2013


Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),Jaji Frederick Werema
Uamuzi wa Bunge wa kukataa mapendekezo ya serikali ya kuongezea makali sheria ya mgazeti namba tatu ya mwaka 1976 ambayo inajulikana kuwa ni kandamizi dhidi ya uhuru wa habari nchini, huku ikiungwa mkono na wabunge wachache imethibisha kuwa bado kuna wanasiasa maadui wa uhuru wa habari nchini.

Wabunge hao walidhihirika kutokana na kauli walizozitoa wakati wakichangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2013, kwa nyakati tofauti bungeni wiki iliyopita. 

Muswada huo, ambao ulirekebisha sheria 14 zilizopendekezwa na serikali bungeni, ulipendekeza pia Sheria ya Magazeti Namba Tatu ya Mwaka 1976, irekebishwe katika kifungu chake cha 36 na 37 kinachotoa adhabu ya faini ya Sh. 150,000 au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja kwa gazeti litakalofanya makosa ya kuchapisha habari ya uchochezi au inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuingeza faini hadi Sh. milioni tano.

 Muswada huo uliwasilishwa bungeni Jumatano wiki iliyopita, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, na kupendekeza kifungu hicho kirekebishwe kwa kuongeza adhabu ya faini hiyo kufikia Sh. milioni tano.
Walioonyesha nia kukaba koo uhuru wa habari ni pamoja na:

JAJI WEREMA
Awali, akiwasilisha muswada huo bungeni, Jaji Werema alisema serikali imepitia Sheria ya Magazeti na kuona kuwa inazuia uchapishaji wa habari inayoweza kusababisha uchochezi au uvunjifu wa amani kama inavyoelezwa katika vifungu vya 36 na 37.

“Aidha, adhabu ya faini kwa makosa ya kuchapisha habari ya uchochezi au habari inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani chini ya vifungu hivyo ni Sh. 150,000,” alisema Jaji Werema na kuongeza:

 “Kwa kuzingatia kuwa adhabu hiyo ni ndogo kulinganisha na madhara ya kosa husika katika jamii, muswada unapendekeza katika Ibara ya 40 na 41 kuwa vifungu hivyo virekebishwe kwa lengo kwa lengo la kuongeza adhabu ya faini kwa makosa hayo ili adhabu hiyo isizidi Sh. milioni tano.”

Akijibu hoja za wabunge waliochangia muswada huo, Jaji Werema alisema marekebisho hayo hayana nia ya kuwakanamiza waandishi wa habari.  “Taifa kubwa la Amerika, marekebisho ya kwanza ya katiba ya nchi hiyo, ambayo inafanana na katiba yetu, inahusu uhuru wa habari,” alisema Jaji Werema na kuongeza:

“Mahakama kubwa imeshaweka mipaka ya uhuru kama ambayo iko kwenye katiba yetu, kwa sababu uhuru bila mipaka ni vurugu. Lazima uwe na control (udhibiti).”

“Kama watu wenye nguvu, akina Tyson, kama wangekuwa wakiona mtu mwenye mwili mdogo wanampiga kama Chiza na Kafulila ingekuwaje?”

“Niliona kwenye magazeti, maofisa usalama wanaandikwa habari zao na picha zao zinawekwa kwenye gazeti. Kwa hiyo, unapokuwa na haki linda wajibu wako,” alisema Jaji Werema.

Alisema lengo la kuwekwa adhabu ni kufundisha, hivyo adhabu inayotolewa kwenye sheria hiyo kwa sasa imelenga iwe kali kwa mwovu, kwa sababu haiwezekani kumwadhibu mtu safi na kwamba, mtu mwovu ni yule anayekiuka wajibu wake kwa Taifa.

 “Hili Taifa halikujiunda, hili Taifa limeundwa, ni lazima tulilinde kwa sheria,” alisema Jaji Werema na kuongeza:  “Kwa hiyo kama mtu unatumia kalamu, unaanza kuandika maandishi ambayo yanalenga kuleta vurugu, kifungu hiki kinakuhusu wewe.”

 Alisema serikali imefikia hatua hiyo baada ya kuona pamoja na mambo mengine, baadhi ya waandishi wa habari kuanza kuandika mambo yanayohusu majeshi ya nchi yaliyoko kwenye operesheni katika nchi mbalimbali.  Alisema kwa kuwa hategemei magazeti kuwa mbunge, kamwe hawezi kumung’unya maneno kuhusu marekebisho yaliyofanywa kwenye sheria hiyo.

“Kama unasema ili magazeti ya kulinde get out (nenda nje), wewe uwe ni CCM uwe Chadema,” alisema Jaji Werema na kuongeza:

 “Marekebisho hayo niliyoyaleta siyaondoi, ondoeni nyinyi. Kwa kiapo nilichoapa haya siyaondoi. Hili halina hila wala hatumlengi mtu, wala halihusiani na kumfungia mtu, katiba iko wazi, nendeni mahakamani. Kama nchi tuogope kalamu ambazo hazifikirii maslahi ya taifa nchi hii.”

“Tutaleta hiyo sheria. Ila kifungu hicho kibaki kama serikali inavyopendekeza. Sitamwangukia mtu miguuni, lakini kwa maslahi ya Taifa hiki kifungu sitakiondoa,” alisema Jaji Werema.

KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Fakharia Khamis Shomar, akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pindi Chana, kuhusu muswada huo, alisema kamati inaunga mkono pendekezo la nyongeza ya adhabu katika sheria hiyo.

Alisema adhabu hiyo ni kwa wale wanaokutwa na hatia ya kutumia lugha za matusi na uchochezi unaoweza kusababisha machafuko nchini.

 “Ni ukweli usiopingika kwamba misingi ya uanzishwaji wa vyombo vya habari kama magazeti si kutumia lugha za matusi na kuandika habari za uchochezi zinazoweza kusababisha mchafuko. Bali ni kuhabarisha jamii kuhusu taarifa na matukio mbalimbali yanayoihusu jamii,” alisema Fakharia.

PINDI CHANA

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana, aliwaomba wabunge, wahariri na wadau wa masuala ya habari nchini kumpa majibu nini kifanyike pale magazeti yanapotumika kuchochea mambo kwa kuandika habari za kupendelea upande mmoja au za kuvuruga amani.

Alitoa ombi hilo kwa maelezo kuwa yeye hana majibu.

“Wametuambia lengo la marekebisho ya sheria hii ya magazeti ni kuongeza adhabu ili kulinda matumizi ya lugha ya matusi yanayoweza kusababisha ukosefu wa amani,” alisema Chana.  Aliongeza: “Sasa nauliza pale magazeti yanapotumika kuchochea mambo na kuvunja amani, ndiyo uhuru wa habari. Nauliza na sina majibu. Wahariri, wabunge niambieni.”

Alisema hana matatizo na vyombo vya habari wala waandishi au wahariri, lakini akasema wapo baadhi yao wananunuliwa na kikundi cha watu kupotosha ukweli au kupendelea upande fulani na kuhoji wachache hao wafanyweje?

 “Wale wanaotumika ndivyo sivyo, leo Bunge hili lisema nini kifanyike, Watanzania wenzangu tusaidiane pale kikundi cha watu kinatumia vyombo vya habari kubeba kikundi kimoja na hususan kwa wanasiasa. (magazeti) yanatumika sana tufanyeje?” alihoji Chana. 

Alisema kuna nchi leo zinashindwa kurudisha amani, na kutolea mfano wa nchi ya Misri ambayo alisema imeshindwa kurejesha amani yao na kutaka Watanzania na wadau nchi kusaidiana kupata jibu la swali hilo.

Alitoa mfano akisema kichwa cha habari kinaandikwa mtu fulani ni jangili halafu kesho akaombwa radhi wakati hata mahakama haijathibitisha tuhuma zilizoandikwa dhidi ya mtu huyo na kusema kitendo hicho kinamshushia heshima mtuhumiwa.

GODFREY ZAMBI

 Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, alisifu hatua hiyo ya serikali kuyabana magazeti, akidai wapinzani wanapinga kwa vile ndio wanayatumia kutoa kauli za kichochezi.

Alisema ni muhimu kwa waandishi wa habari kuwa wazalendo na nchi yao na kutetea taifa lao katika uandishi wao.

Zambi alisema pamoja na kuweka sheria hiyo, lazima kuweka sheria kali dhidi ya lugha za uchochezi zinazoandikwa katika baadhi ya vyombo vya habari.

“Bado kuna umuhimu kwa serikali kuweka adhabu juu ya masuala ya kuandika habari za uchochezi na kama wapo watu wanaona kuwa kuweka adhabu hizo ni kuwanyima haki waandishi, basi hao wanataka kuvitumia vibaya vyombo hivyo kwa maslahi yao,” alisema Zambi.

MWIGULU NCHEMBA.
 Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba, alisema habari nzuri zimekuwa si habari, ila zile mbaya ndiyo biashara.

Hivyo, akasema ni lazima Bunge litunge sheria itakayobana tabia ya watu aliyoiita ya kuuza sana taarifa mbaya wakati zipo nzuri nyingi za Taifa, ambazo magazeti hazizichapishi.

 “Lazima tukubali kwamba taarifa mbaya ni hatari kwa Taifa. Sioni shida kwa upinzani kuona taarifa mbaya ni mtaji kwao, kwa sababu hawana dhamana na hawana uzalendo na Taifa hili. Adui yetu mkubwa ni yule aliye adui wa Taifa letu,” alisema Nchemba. Alisema kuna wabunge wanamiliki vyombo vya habari, hasa magazeti, ambao kazi yao ni kuuza taarifa.

Pia alisema kuna watu wana pasi mbilimbili za kusafiria ndani ya vyama vyao na pia wanamiliki majumba nje ya nchi, ambao wapo tayari kuvuruga amani ya nchi na kukimbilia nchini Dubai yaliko majumba yao.

“Wanamiliki vyombo vya habari kwa ajili ya kuchafua amani ya nchi. Ni wachochezi sana na wanatekeleza azma yao kuwa nchi hii haitatawalika. Kikishanuka hapa wao wanajua wanamiliki nyumba nyingi nje ya nchi watakimbilia huko,” alisema Nchemba.

Aliongeza: “Misri na nchi nyingine zimepoteza amani kwa sababu ya vyombo vya habari, ambavyo vilikuwa vinachochea mambo ya uongo ndani ya nchi yao. Leo hii wapo wapi? Lazima sheria ziwe kali sana.”

Alisema pia kuna viongozi wa vyama bungeni, ambao wamezoea kuongoza kwa mabavu, wanaruka vichwa na kuwapiga viongozi wao ndani ya chama.

“Yaani Kikwete aruke kichwa kumpiga mwenyekiti wa mkoa wa Dar es Salaam wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kweli huu ndiyo uongozi?” alihoji Nchemba.

Aliongeza: “Yaani lazima sheria ziwe kali sana. Watu wanapenda kulaumu mambo yapo ovyo wakati hawataki sheria ziwe kali juu yao na juu ya utaifa wetu. Naomba sheria ya magazeti iendee juu zaidi, iwe kali zaidi, kwani watu wananufaika na sheria hii kuwa butu.”

WADAU WA HABARI WANENA
Wadau wa habari wamepongeza hatua ya wabunge kupinga marekebisho ya sheria ya magazeti ya mwaka 1976 na kutaka muswada wa sheria ya habari  ulioandaliwa na kujadiliwa na wadau mwaka 2006 kufikishwa bungeni.

Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwandishi mwandamizi, Dk. Ayoub Rioba, alisema maamuzi ya wabunge wachache waliopinga marekebisho ya sheria hiyo ni ya kiungwana na kizalendo.

Alisema haiwezekani leo serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya sheria ambayo ni mbovu inayotakiwa kubadilishwa kwani haifai katika kipindi cha demokrasia ya vyama vingi.

“Kama wabunge wangepitisha mapendekezo yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa serikali, ningewashangaa sana…wanaachaje kuhoji muswada uliojadiliwa na wadau tangu mwaka 2006 haujafika Bungeni na badala yake warekebishe vipengele?”alihoji.

Dk. Rioba alisema si wakati wa kutafuta namna ya kuweka viraka kwenye sheria ili kuweza kukamata watu na kuwabana washindwe kufanya kazi na badala yake muswada ujadiliwe kwa manufaa ya umma.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (Misa-Tan), Mohammed Tibanyendera, alisema marekebisho ambayo yangefanyika yangekwenda kinyume cha ibara ya 18 ya Katiba kwa kuminya uhuru wa habari.

“Naamini wabunge walifanya hivi kwa maslahi ya umma na si kisiasa, na hata muswada wa sheria ukifikishwa kwao wataujadili kwa maslahi ya wananchi na wasikubali kutumika kisiasa na kuingiza vifungu vya kukandamiza uhuru wa habari,” alisema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (Jet), Chrysostom Rweyemamu, alisema anashanzwa na haraka ya serikali kufanya marekebisho ya sheria hiyo, badala ya kusubiri Katiba mpya ambayo ni sheria mama.

“Naishangaa serikali, mambo inayofanya na Mwanasheria Mkuu naye simuelewe, tungesubiri Katiba mpya na si kwenda mbele na kurudi nyuma kwani baada ya kupatikana Katiba sheria nyingine zitahitaji marekebisho kwenda sambamba nayo,” alisema.

Rais wa Muungano wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Keneth Simbaya, alisema ni hatua nzuri kwa wabunge kukataa kwa kuwa itatoa fursa kwa wadau na jamii kujadili kwa kina.

Alisema wadau wa habari na waandishi wa habari nchini walishapiga kelele kuwa sheria hiyo si rafiki kwa habari na ndiyo maana muswada uliandaliwa ulibaki kufikishwa bungeni.

Alisema sheria kandamizi inatisha watu kufanya kazi kwa uhuru na badala yake kuwa na hofu kila wakati.

Hata hivyo Bunge lilikataa kuifanyia fanya marekebisho sheria hiyo na kuiagiza serikali kupeleka Bungeni Muswada wa Sheria ya Habari.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment