Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, November 22, 2013

Serikali yapigwa chenga uuzaji wa gesi

Na Mwandishi wetu


Ni mauzo ya hisa za Sh. trilioni 2.09
Waziri wa Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo
 
Wakati taarifa za kampuni ya Ophir Energy PLC kuuza asilimia 20 ya hisa zake katika vitalu vitatu vya gesi asilia inavyomiliki nchini na kuingiza dola za Marekani bilioni 1.288 (sawa na Sh. trilioni 2.087), Tanzania haijui itakachopata katika mauzo hayo.

Ophir Energy ya Uingereza iliuza hisa hizo kwa kampuni ya Pavilion Energy ya Singapore, malipo ambayo yanalipwa kwa awamu hadi robo ya kwanza ya mwaka ujao.

Malipo hayo yanafanyika wakati Serikali imetengeneza sera mpya ya gesi asilia, lakini ikilenga tu shughuli za usindikaji, masoko, usafirishaji na usambazaji (down-stream activities), wa bidhaa zote zinazotokana na nishati hiyo bila kugusa utafiti, udhibiti na uchimbaji (up-stream activities).

Serikali katika sera yake mpya, imesema eneo la up-stream litashughulikiwa na sera ijayo ya mafuta ya petroli ambayo hata hivyo, haijulikani ni lini itakuwa tayari.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alipoulizwa kuhusiana na uuzaji huo, alijibu kwa kifupi: “Una uhakika kwamba hizo hisa zimeuzwa?”

Hata hivyo, NIPASHE ilipomwambia taarifa ya uuzaji wa hisa imewekwa kwenye tovuti ya kampuni ya Pavilion Energy na pia vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti, alisema: “Unauhakika? Soma matangazo yao.”

NIPASHE: Matangazo ya kampuni gani? Je, yametolewa wapi?
MASWI: Tafuta matangazo yao, wameeleza bayana kabisa.

NIPASHE: Sisi tulitaka kujua kama Taifa tumenufaika vipi na uuzaji huu?
MASWI: Tafuta matangazo yao.

Baada ya majibu hayo, Maswi alikata simu.

Wakati Maswi akijibu hivyo, mauzo ya hisa hizo yanahusu gesi yenye futi trilioni 15 za ujazo. Katika makubaliano hayo, kampuni ya Pavilion itaanza kupata gesi hiyo mwaka 2020.

Taarifa ya Pavilion Energy Pte Ltd ya Alhamisi iliyopita inaeleza kuwa tayari kampuni hizo mbili zimekwisha saini makubaliano ya kununua asilimia 20 ya hisa kwenye visima namba moja, tatu na nne nchini Tanzania kwa dola za Marekani bilioni 1.288.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa ununuzi wa hisa hizo kwenye visima Jodari, Mzia na Pweza, utatimiza lengo la kampuni ya Pavilion ya kusambaza nishati kwa nchi za Asia.

Taarifa ya kampuni ya Pavilion imemkariri Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Seah Moon Ming, akieleza kuwa malipo ya mwisho kwenye biashara hiyo yanatazamiwa kumalizika robo ya kwanza ya mwaka ujao na kwamba itaanza kuchukua gesi mwaka 2020.

“Uwekezaji huu katika vitalu 1, 3 na 4 nchini Tanzania ni hatua muhimu kwa Pavilion Energy kujenga mkakati wetu wa kudumu kwenye usambazaji wa gesi kwa muda mrefu na kwa bei ya ushindani ili kukidhi mahitaji ya nishati safi Asia na kwa bei ya ushindani,” alikaririwa Ming kwenye taarifa hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa ugunduzi wa gesi nchini utaifanya Tanzania kuwa muuzaji mkubwa wa gesi nje ya nchi na Mwenyekiti wa kampuni ya Pavilion Energy, Tan Sri Mohd Hassan Marican, anaiangalia Tanzania kama mdau muhimu wa kupeleka nishati hiyo katika soko la Singapore na Asia kwa ujumla.

Mauzo hayo yanakuja huku kukiwa na kesi kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kampuni ya Mantra ya Australia iliyouza hisa kwa kampuni UraniumOne ya Urusi, kwa dola za Marekani milioni 980, bila kulipa kodi yoyote.

Kampuni hizo zinamiliki leseni ya kutafuta uranium Selous, Mkuju River Project.

Katika mauziano hayo, TRA ilitaka ilipwe kodi ya ongezeko la mtaji (capital gains tax), lakini kampuni hiyo ilikataa jambo lililopelekea TRA kwenda mahakamani kudai malipo ya kodi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 116.

Kwa mujibu wa sheria, kampuni zinapouziana leseni, lazima Waziri wa Nishati na Madini atoe idhini ya mauzo hayo, lakini Profesa Sospeter Muhongo, aliwahi kujibu bungeni kuwa kilichokuwa kimeuzwa siyo kampuni ya Tanzania bali Australia na hivyo hakuna kodi, jambo ambalo liliibua mvutano bungeni kati yake na mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, aliyekuwa ameuliza swali.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment