Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, November 24, 2013

“Wakili wa Ibilisi” aliyepotea kwenye kioo

 Ahmed Rajab

Bibi Doris Lessing akionyesha tuzo yake
Bibi Doris Lessing akionesha tuzo yake

Ahmed Rajab
Toleo la 326
20 Nov 2013
Hivi karibuni walikufa watu wawili waliokuwa mashuhuri duniani, kila mmoja kwa kiasi chake. Wote hawakuwa Waafrika lakini ama walikulia Afrika au walikuwa na mahusiano makubwa na Wafrika.
Kukutana na watu wa sampuli zao — au kuzijua tu habari zao — kunayafanya maisha yazidi kuwa na ladha.
Mmoja kati ya wawili hao sikupata kamwe kumshuhudia. Lakini nimekuwa nikimsikia tangu ujana wangu na huyafananisha maisha yake na kitendawili. Aliishi kiajabu ajabu.
Mwengine nilikuwa sitoki kwake hasa katika siku zangu za ujana. Nimekula chakula chake, nimeosha sahani zake na nimewapapasa paka wake.
Sina hakika wala sijui iwapo wawili hao waliwahi kukutana. Lakini nadhani kama hawajakutana basi lazima kila mmojawao aliwahi kusikia habari za mwenziwe. Na kuna viungo vinavyowaunganisha.
Kiungo kimoja ni siasa za ukombozi.
Kingine kina umbo la binadamu: Abdul Rahman Babu, mwasisi na kiongozi wa chama cha Kimarx cha Umma Party huko Zanzibar na aliyewahi kuwa waziri Tanzania. Babu alikuwa rafiki wa chanda na pete na wote wawili.
Niliyekuwa sikuwahi kukutana naye ni wakili Jacques Vergès, aliyefariki dunia Paris, Ufaransa, Agosti 15 akiwa na umri wa miaka 88. Niliyekuwa nikimjua ni Doris Lessing mwandishi aliyefariki Jumapili iliyopita nyumbani kwake hapa London akiwa na umri wa miaka 94.
Wote wawili walikumbana na Babu walipokuwa wanaharakati wa mrengo wa kushoto miaka ya 1950.
Vergès, ambaye babake alikuwa Mfaransa na mamake Mvietnam, alikulia katika kisiwa cha Réunion kilicho mashariki mwa Madagascar.
Huko Réunion, inayotawaliwa na Ufaransa, Vergès ana nduguye pacha aitwaye Paul Vergès. Ni mwasisi wa Chama cha Kikoministi cha nchi hiyo alichokiongoza tangu 1959 hadi alipostaafu 1993. Paul aliwahi mara kadhaa kuwa Mbunge Ufaransa na Mbunge wa Bunge la Ulaya.
Jacques Vergès, kwa upande wake, alianza kujulikana miaka ya 1950 alipokuwa akivuma kama Mkomunisti aliyekuwa akipigania ukombozi wa makoloni ya wazungu. Wakati huo Babu alikuwa London, akiwa pia anapigania ukombozi wa Afrika.
Harakati hizo zilimfanya achaguliwe kuwa katibu wa Kamati ya Afrika ya Mashariki na ya Kati ya Vuguvugu la Uingereza la Kupigania Uhuru (Movement for Anti-Colonial Freedom).
Miongoni mwa aliokuwa akishirikiana nao Babu katika harakati hizo walikuwa Joseph Murumbi (ambaye baadaye alikuwa Makamu wa Rais wa Kenya chini ya Jomo Kenyatta), Mbiyu Koinange (mwakilishi wa Mau Mau na ambaye baadaye naye alikuwa waziri wa Kenyatta), mwandishi wa Afrika ya Kusini Peter Abraham, George Padmore (mwanamajumui wa Kiafrika) na Dk. Hastings Kamuzu Banda, aliyekuwa daktari wa Babu hapa London na baadaye alikuwa Rais wa Malawi.
Kulikuwako pia na mwanamke mmoja, Doris Lessing. Alikuwa mbichi, ndo kwanza amewasili London kutoka Rhodesia ya Kusini (Zimbabwe ya sasa).
Huyu ndiye Doris Lessing aliyefariki juzi na kuufanya ulimwengu wa fasihi uingiwe na majonzi. Huyu ndiye Doris Lessing aliyetunukiwa tuzo ya Nobel ya fasihi mwaka 2007 na ambaye amepewa tuzo nyingine nane.
Huyu ndiye Doris Lessing aliyeandika vitabu vipatavyo 70, vingine vikiwa vya muziki wa opera, vingine vya watoto, vingine vya riwaya, vingine vya hadithi fupi fupi, vingine vya kumbukumbu, vingine kuhusu paka kwani akipenda kufuga paka na vingine kuhusu nyanja mbalimbali za maisha.
Katika vitabu vyake viwili amemtaja Babu. Kwenye kimoja cha kumbukumbu zake amemtaja kwa uwazi, kwa jina; katika kingine cha riwaya amemficha kwenye wasifu wa mhusika mmoja katika riwaya hiyo.
Huyu ndiye yuleyule Doris Lessing aliyezaliwa Iran akakulia Rhodesia ya Kusini, akaja London akaandika mengi kuhusu Afrika na akajitolea kuitetea Afrika.
Muda mfupi baada ya kufariki nilipokea baruapepe kutoka kwa mama mmoja wa Kiingereza akiniarifu kuhusu kifo hicho. Aliandika: “Inahuzunisha kusikia kwamba punde hivi aliiaga dunia lakini 94 ni umri wa ajabu. Sitoisahau siku uliyonichukua mimi na Peter (mumewe) kwenda kula naye.”
Si umri wake tu uliokuwa wa ajabu. Yeye mwenyewe pia. Alikuwa mkarimu kupita kiasi. Hakupata kunialika nikajikuta peke yangu; daima akiwaalika na wengine. Wengi walikuwa wanawake wenzake kwani wakimhusudu, wakihisi kwamba maandishi yake yanaipigia vigelegele nadharia ya ukombozi na usawa wa wanawake. Mwenyewe akikanya.
Safari moja alinialika kwenye hafla katika kasri iliyo nje ya London ya mwandishi maarufu aitwaye Idries Shah, aliyekuwa rafikina mwalimuwake wa tasawwuf (Sufism).
Nilimwambia nitafuatana na rafiki yangu. Akasema: “Sawa”. Na huyo rafiki niliyeenda naye alikuwa Profesa Abdul Sheriff aliyekuwa London wakati huo.
Kabla ya kufunga safari Doris alinipigia simu na kunambia: “Itakuwa hafla ya saa 48 na tunaiita ‘Usiku wa Kiarabu’ kwa hivyo vaeni inavyostahiki.” Nilivaa tarbushi. Nikiandika tulioyashuhudia huko gazeti hili zima litajaa basi kheri tuyaache.
Doris Lessing niliyekutana naye miye hakuwa akitafautiana sana kimawazo na yule aliyekutana naye Babu miaka ya 1950. Wakati huo Babu alikuwa mmoja wa wahariri wa jaridala mwanzo la kimapiduzi lililokuwa la mrengo wa Mwenyekiti Mao wa China na lililokuwa likichapishwa Paris.Likiitwa Afro-Asian Latin American Revolution. Babu alikutana na Mao mara ya mwanzo alipoalikwa rasmi aizuru China mwishoni mwa 1954 na Vergès alikutana naye Mao Machi 1963.
Wahariri wengine wa jarida hilo walikuwa Profesa Samir Amin, Frene Ginwala aliyewahi huwa mhariri wa Daily News nchini Tanzania na baadaye Spika wa Bunge la Afrika ya Kusini. Mhariri mwengine alikuwa Jacques Vergès.
Babu pia aliliandikia gazeti jengine Révolution africaine alilokuwa akilihariri Vergès huko Algeria.
Jacques Verges
Jacques Verges
 
Wiki kadhaa kabla hajafariki rafiki yangu mmoja mjini Paris, Bwana Salim Hadji Himidi, waziri wa zamani mambo ya nje wa Comoro, alikutana na Vergès mjini humo. Alimzungumza sana Babu na akamwambia Bwana Himidi ampigie simu ili waonane amwonyeshe kumbukumbu za Babu alizokuwa nazo. Bahati mbaya rafiki yangu hakumpigia simu.
Miongoni wa wanafunzi wenzake alipokuwa Vergès akisoma Chuo Kikuu cha Paris alikuwa Pol Pot. Huyu atakuja kuwa kiongozi katili wa Kikomunisti nchini Cambodia.
Baada ya kumaliza masomo ya sheria Vergès alianza kuwatetea wakombozi wa Algeria mahakamani Ufaransa. Alimuoa mmojawao Djamila Bouhired na Ufaransa ilipoipa Algeria uhuru Vergès alihamia huko, akachukua uraia wa Algeria na kufanya kazi katika wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo.
Halafu mwaka 1970 Vergès akaupa ulimwegu kitendawili kikubwa. Alikopa mamilioni ya franga za Algeria kutoka Benki ya Algeria na akatoweka. Hakuna aliyejua alipotelea wapi. Alimkimbia mkewe, familia yake, marafiki zake na kazi yake. Alipoibuka miaka tisa baadaye alikuwa akisema tu kwamba alikuwa amekwenda“likizo”. Wakati mwingine akisema alivuka njia na alikwenda “upande wa pili wa kioo.”
Kuna uvumi mwingi lakini hadi leo hakuna ajuaye alikuwa wapi hasa. Wengine wakisema alikuwa Cambodia akimsaidia Pol Pot. Wengine kwamba alikuwa Urussi akifunzwa namna ya kuwa jasusi na KGB, shirika la ujasusi la Muungano wa Sovieti. Wengine wakisema alikuwa Damascus akimsaidia Walid Haddad aliyeunda kundi la ukombozi wa Palastina la PFLP. Ukweli ni kwamba hakuna ajuaye kweli ya kupotea kwa Vergès.
Halafu aliporudi Paris akiwa hana hata ndururu akaanza kuwatetea mahakamani wasiostahili kutetewa na magazeti ya Ufaransa yakambandika jina la ‘Wakili wa Ibilisi’. Alimtetea mhalifu wa Hitler, Klaus Berbie na Rais wa zamani wa Cambodia Khieu Samphan walioua halaiki ya watu; aliwatetea magaidi wawili wa Kijerumani; alimtetea Tariq Aziz aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Saddam Hussein huko Iraq. Aliwashauri pia akina Slobadan Milosevic aliyekuwa Rais wa Serbia na Saddam Hussein wa Iraq. Vergès akipenda kusema kwamba moja ya maadili yake ni kutokuwa na maadili.
Wakati mmoja Vergès alikuwa wakili wa gaidi Ilich Ramirez Sanchez maarufu kwa jina la ‘Carlos The Jackal’. Lakini baada ya muda Carlos akamkataa akiiambia Mahakama kwamba: “Wakili Vergès ni gaidi mkubwa kushinda mimi.”
Kuna mwandishi aliyewahi kumuuliza iwapo angemtetea Hitler. Vergès alimjibu: “Nitamtetea hata George Bush lakini yeye kwanza lazima akiri kuwa anayo hatia.”
Chanzo: Raia Mwema

No comments :

Post a Comment