NA MHARIRI
13th November 2013
Changamoto hii ni ya kweli kwa sababu aghalab uhalifu hufanywa na watu waliofuzu vizuri mambo ya usalama na pengine walipata kufanya kazi katika vyombo vya usalama na kwa maana hiyo wana ujuzi wa kujipanga na kutekeleza uhalifu wao kwa makini kiasi cha kukwepa kuacha kielelezo chochote cha kuwaunganisha na uhalifu wao.
Ni kwa maana hiyo kwa wale wanaofuatilia taarifa mbalimbali za kiusalama duniani wanaelewa kuwa zipo kesi mbalimbali za jinai zimechukua miaka na miaka kwa wahusika kupatikana.
Kazi ya kupeleleza uhalifu kimsingi siyo nyepesi na inajulikana hivyo. Uhalifu ni changamoto kwa mataifa yote, masikini na tajiri. Vyombo vya usalama vinatumia gharama kubwa kusomesha wataalamu wa kukabiliana na changamoto hizo; hata hivyo, maendeleo ya sayansi na teknolojia yamefanikisha upatikanaji wa zana muhimu za kusaidia katika upelelezi wa uhalifu.
Tukiwa tunatambua ukweli huu, tumeguswa na kauli iliyotolewa juzi na viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi kwamba vyombo vya habari vimekuwa kikwazo cha polisi kufanikisha uchunguzi wa matukio kadhaa ya uhalifu hususan yaliyohusu kutekwa na kuteswa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka na tukio linalofanana nalo la kutekwa kupigwa, kung’olewa kucha, kukatwa kidole, kung’olewa meno na kutobolewa jicho, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea mafanikio yaliyofikiwa na vyombo vya usalama katika uchunguzi wa janga lililomkuta Mjumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, lakini wakajitetea sababu za kushindwa kufanikiwa katika kukamatwa kwa wahalifu wengine aliohusika na majanga ya Kibanda na Dk. Ulimboka.
Kwa utetezi wa viongozi hao, mojawapo ya sababu za kushindwa kukamatwa kwa yeyote kati ya wahusika wa matukio hayo mawili ya kutisha ni vyombo vya habari kuingilia upelelezi. Kuingilia upelelezi kunakoelezwa ni vyombo vya habari kuandika mno kuhusu habari za Kibanda na Dk. Ulimboka!
Kwa mawazo na msimamo wa viongozi hao wawili, kitendo cha kuandikwa mno kwa habari za matukio hayo mawili ambayo kimsingi yaliwafikisha wahusika kuzimu kama siyo tu mkono wa Mungu kuwaokoa kwa jinsi walivyoumizwa, ndiko eti kumewafanya polisi na wote waliokuwa wanapeleleza matukio hayo kushindwa kukamata mtuhumiwa yeyote hadi leo.
Ni kwa maana hiyo, viongozi hao wanataka vyombo vya habari viache kufuatilia mambo ambayo yanafanyiwa upelelezi na polisi kwa madai kuwa watavuruga upelelezi kwa kuandika sana! Kwamba tukio la Dk. Mvungi halikuandikwa sana ndiyo maana polisi wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa tisa hadi ilipofika juzi.
Tunatambua kwamba upelelezi wa kesi hasa za kusaka watu waliotenda mambo maovu kama waliotendewa Kibanda na Dk. Ulimboka siyo jambo rahisi hata kidogo, tumesema tangu awali, lakini kwa polisi kufikia hatua ya kutaka kuaminisha umma kwamba eti kukwama huko kunatokana na waandishi wa habari kuandika mno mambo hayo ni kutokuwatendea haki wananchi kwa kuwataka kuwaweka gizani katika mambo ambayo yanahusu usalama wao.
Tunasema wazi kwamba vyombo vya habari siyo idara ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama, wala siyo kazi ya vyombo vya habari kujua nini maofisa wa vyombo vya ulinzi wanafanya katika kuchunguza matukio ya uhalifu, kwa kawaida vinapewa taarifa kama zimekamilika au bado uchunguzi unafanyika.
Vyombo vya habari navyo vina wajibu wa kufanya kazi zake kwa mujibu wa maadili yake; habari za uchunguzi wa matukio kama ya kushambuliwa Kibanda na Dk. Ulimboka ni sehemu ya wajibu wa lazima kabisa kuchunguzwa hata kama vyombo vya usalama vinachunguza au kinyume chake.
Kwa msingi huo, siyo sahihi kusingizia vyombo vya habari kuwa ni kikwazo cha vyombo vya ulinzi na usalama kutimiza wajibu wake.
Tunatambua vyombo vya ulinzi na usalama vipo kisheria, vina nguvu ya kutimiza wajibu wake kisheria, hakuna mwenye uwezo wa kuvizuia kutimiza wajibu wake, vina zana, vina wataalam waliofuzu kwa kazi hizo, lakini zaidi vinapatiwa fungu la fedha za walipa kodi kutimiza wajibu huo muhimu kwa ajili ya ulinzi wa maisha na mali za raia wa nchi hii.
Vyombo vya habari vinafanya kazi zake kwa kujituma tu, havilindwi na sheria yoyote, havina uwezo wa kumshurutisha yeyote asema au atoe taarifa fulani.
Katika mazingira hayo, ni kuvionea vyombo vya habari kuwa ni sababu ya kushindwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kutimiza wajibu wake kwa umma.
Katika mazingira yanayozingatia weledi, taarifa za vyombo vya habari siyo tu zimesaidia vyombo vya ulinzi na usalama kufanikisha upelelezi wake, bali ni nyenzo muhimu katika kufanikisha kazi zao; vyombo vya habari vinavyokaa kitako kusubiri kuletewa habari zilizokwisha kukamilishwa na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama bila vyenyewe kuwa mstari wa mbele kudadisi na kuchunguza kwa kuzingatia maadili yake, havistahili kuitumikia jamii yake.
Ni vema watendaji wa umma wakaepuka tabia ya kusaka visingizio pale wanaposhindwa kutimiza wajibu wake, badala yake wawajibike kwa udhaifu wao wa kushindwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment