NA MWANDISHI WETU
21st November 2013
Ni kauli ya Kinana
Waziri Mgimwa anaungana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima.
Mawaziri hao watahojiwa katika kikao cha CC kitakachofanyika mwezi ujao.
Kuongezeka kwa Dk. Mgimwa katika orodha hiyo kulitangazwa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, mkoani Ruvuma, baada ya kupokea malalamiko ya wakulima wa mahindi wa Wilaya ya Songea ya kutolipwa fedha za mahindi yao zaidi ya tani 50,000 ambayo yalichukuliwa na serikali.
Akizungumza jana na wananchi wa kijiji cha Masangu, kata ya Magagula wilayani Songea, Kinana alisema Dk. Mgimwa ndiye Waziri wa Fedha, hivyo malalamiko ya wakulima ya kutolipwa fedha yanamhusu na kwamba lazima aitwe CC kuhojiwa.
”Kikao kinachokuja cha Kamati Kuu, Waziri wa Fedha, Dk. Mgimwa anatakiwa kutoa maelezo ya kina, naye ataitwa kuhojiwa na kwa hili sitanii, lazima aitwe na atoe maelezo kuhusu malalamiko hayo,” alisema Kinana aliyeonekana kuchukia kutokana na malalamiko ya wananchi.
Kinana alisema chama chake hakiwezi kukaa kimya wakati wananchi wakilalamika na kwamba madai yao ni ya msingi kwa serikali, hivyo akiwa mtendaji mkuu wa CCM, lazima apate majibu ya kuridhisha kutoka kwa mawaziri hao wenye dhamana ya kuutumikia umma.
”Waziri wa Fedha hawezi kuachwa huku wakulima na wadau mbalimbali wa mahindi wakiwamo waliosafirisha wakiwa hawajalipwa fedha zao. Ninasimamia maagizo ya mkutano mkuu wa nane ulioagiza Chama kusimamia serikali zake mbili ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar. Hivyo sifanyi mimi binafsi na haya yote sijaja nayo kwenye ziara bali nimeyakuta,” alisema.
Kwa mujibu wa Kinana, Dk. Mgimwa anatakiwa kujiandaa na mambo kadhaa ya kuijibu CC ikiwamo kujibu kwanini wakulima hawalipwi fedha zao wakati bajeti ya fedha imepitishwa mapema ili fedha zitumike kwa wakati ikiwamo wakulima kulipwa fedha zao baada ya kuliuzia mahindi Ghala laTaifa.
Alisema pia Dk. Mgimwa atatakiwa kujibu kwanini fedha za pembejeo hazilipwi kwa wakati, hali inayosababisha malalamiko katika maeneo yote ambayo amepita, wakati fedha hizo zilishatolewa.
”Atujibu kwanini bajeti ya serikali ilichelewa kutekelezwa licha ya kusomwa Aprili badala ya Julai kwa lengo la kuanza kutekelezwa mapema,” alisema Kinana, ambaye ameongozana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje, Dk. Asha-Rose Migiro.
Hata hivyo, Kinana alisema umefika wakati kila mtendaji wa serikali pamoja na mawaziri kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi badala ya kulalamika.
”Viongozi wote walipoteuliwa kushika nafasi mbalimbali hawakukataa, bali walifurahi na kuahidi kuwahudumia wananchi, hivyo hilo ndilo tunalolisubiri na kulitarajia,” alisema.
Kinana alisema CCM ndiyo iliyopewa dhamana na wananchi ili iwatumikie na kuunda serikali, hivyo lazima waisimamie kufanikisha matumaini ya Chama kwa Watanzania.
Jumatatu wiki hii, CCM kupitia Nape kiliwataja Dk. Kawambwa, Christopher Chiza na Adam Malima,kuwa wameshindwa kazi na kupendekeza wang’olewe.
Nape alitoa kauli hiyo mbele ya Kinana, akisema kuwa mawaziri hao wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.
Alisema anasikitishwa na kitendo cha mawaziri hao waliopewa dhamana kushindwa kutambua wajibu wao na kwamba umefika wakati wa kuhojiwa na CC ili wachukuliwe hatua kwani bila kufanya hivyo aibu itarudi kwa chama chake.
Nape alitoa kauli hiyo katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wakati akielezea changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania, huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Alisema kuwa Waziri Chiza na Malima, wamebaki wakifunga tai na kuvaa suti mjini wakati wakulima wa Ruvuma na mikoa mingine ya Tanzania wakiteseka.
Alisema Waziri Kawambwa naye anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kuingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya Progressive iliyopewa zabuni ya kutengeza barabara ya Natumbo hadi Tunduru wakati mkandarasi huyo hana uwezo wa kuijenga na matokeo yake amefukuzwa kazi.
Nape alisema inasikitisha kuona wakulima wakiteseka, lakini waliopewa dhamana ya kuwasaidia wakishindwa kuwasikiliza na kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao.
Alisema atahakikisha mawaziri hao wanachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuwajibishwa na Chama na ikishindikana watawatumia wabunge wao kufanya kazi hiyo.
Nape alisema akiwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kila eneo wananchi walikuwa wakiwalalamikia Chiza na Malima kwa mambo mbalimbali hivyo suala hilo linapaswa kufikia mwisho wake maana chama hakiwezi kuwavumilia.
Alimweleza Kinana kuwa alimuuliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, kama Chiza na Malima wamefika lini kusikiliza matatizo ya wakulima wa tumbaku, korosho na mahindi, lakini alimjibu kuwa hakumbuki kama wamefika mkoani hapa.
Nape aliongeza kuwa alifuatilia na kugundua kuwa hata Waziri aliyetangulia kuongoza Wizara hiyo, Profesa Jumanne Maghembe, naye hakuwahi kufika.
Alisema Dk. Kawambwa amekuwa akiikwamisha CCM katika kutimiza wajibu wake na kwamba pia ameshindwa kushughulikia matatizo ya walimu nchini na kumkumbusha kuwa alipewa muda wa miezi sita na CCM na inakaribia kumalizika.
Naye Kinana alisema katika kikao cha CC kitakachofanyika mwezi ujao, kitamuandikia barua Rais Jakaya Kikwete, ili mawaziri wake waende mbele ya kikao na kueleza kwa nini wasifukuzwe kwa kushindwa kazi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment