airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, November 23, 2013

Zitto ang'olewa, Kitila, Mwigamba nao nje

Na Romana Mallya


Wamo pia Kitila Mkumbo, Samson Mwigamba
Makamu Mwenyekiti Bara Said Arif ajiuzulu
 

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lisu.
PICHA: OMAR FUNGO
 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewang’oa nafasi ya uongozi viongozi wanne wa chama hicho akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe.
Wakati viongozi hao wakivuliwa nyadhifa zao, Makamu Mwenyekiti (Bara) wa Chama hicho, Said Arfi, ametangaza kujiuzulu wadhifa wake.

Wengine waliovuliwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitilla Mkumbo, anayetambulika kama M1 kwenye Waraka wa mkakati wa Mabadiliko 2013.

Mwingine ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha aliyesimamishwa uongozi, Samson Mwigamba, ambaye katika waraka huo anajulikana kama M3 na mwingine anayetambulika kama M2 jina lake halijajulikana.

Aidha, M2 anatajwa na waraka huo kuwa yuko ukingoni kupigwa nje katika mageuzi ya kiutendaji yanayoendelea katika sekretarieti cha chama makao makuu.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati Kuu (CC) ya Chadema iliyokaa kwa siku mbili kuanzia Jumatano ya wiki hii, Tundu Lissu ambaye kwa sasa anatambuliwa na chama hicho kama Mwanasheria Mkuu, alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kubaini mkakati huo uliolenga kukiangamiza chama.

Akisoma maamuzi hayo ambayo yamesainiwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Wilbroad Slaa, mwanasheria huyo alisema kikao hicho ambacho kimemalizika jana alfajiri, kilijadili kwa kina taarifa mbalimbali kuhusu hali ya kisiasa ndani ya chama baada ya kugubikwa na tuhuma za viongozi na Chadema yenyewe.

Alisema tuhuma hizo zenye lengo la kuwachafua na kuwapaka matope zilielekezwa moja kwa moja kwa Mwenyekiti Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Slaa.

Pia alisema zililenga kutengeneza mtandao wa siri ndani na nje ya chama ambao hatimaye ungefanikisha sio tu lengo la kufanya mapinduzi nje ya utaratibu wa kikatiba wa chama, bali ungekipasua vipande na kuua matumaini ya Watanzania kuhusu kuleta mabadiliko ya kisisasa, kiuchumi na kijamii.

UCHUNGUZI WA KAMATI KUU

Lissu alisema umebaini kuwepo kwa mkakati huo wa kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka wa ‘Mkakati wa mabadiliko 2013’ ambao umeandaliwa na kikundi hicho kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’.

Alisema Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, katika waraka huo anajulikana kama MM au ‘Mhusika Mkuu’.

Kwa mujibu wa waraka huo, ‘mkakati huu umeandaliwa kwa pamoja na M2 na M3 na kupitiwa na marekebisho na M1 ili upelekwe kwa MM kwa maoni ya mwisho na kuanza utekelezaji.’
Alisema, Dk. Mkumbo alikiri mbele ya Kamati Kuu kuwa MM ni Kabwe, M1 ni yeye na M3 ni Mwigamba.

Alisema Dk. Mkumbo alikataa kumfahamu M2 na kukiri kuwa yote yaliyoandikwa katika mkakati huo yametoka kwenye ‘Mtandao wa Ushindi na hayajabadilishwa.
Akifafanua kuhusu mkakati huo, Lissu alisema ni mpango wa kuipasua Chadema na kuiangamiza kabisa kwenye uso wa siasa hapa nchini.

“Huu sio mkakati wa kufanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya chama kwa njia ya demokrasia na za kikatiba, bali ni mpango wa kukiteka nyara Chadema na kukiua,” alisema na kuongeza:

“Ndio maana watunzi wa waraka huu wanasema, wanahitaji kutekeleza mkakati huu kwa siri kubwa ili mkuu aliyepo aendelee kubweteka na ndio maana hata lugha iliyotumika ndani ni ya pekee,” alisema.

Alisema Kamati Kuu inaamini mkakati wenye malengo halali ya kikatiba ya kufanya mabadiliko ndani ya chama usingependekezwa kwamba ‘Vikao vyetu na yeye (MM) vitafanyika mara chache na mahali pa faragha kupita kiasi ikiwezekana hata nchi jirani,’ mwisho wa nukuu.

Alisema Kamati Kuu inaamini kuwa kama ungekuwa na malengo mazuri ya kukijenga chama, wanamtandao hao wasingependekeza utaratibu kuwa Dk Mkumbo ndiye atakayekuwa anawasiliana na wanayemtaka (MM).

Kwa mujibu wa waraka huo watu hao walipanga wasiwe na mawasiliano mengi kati ya kamati na Kabwe, lengo likiwa ni kuepuka mwingiliano wa mawasiliano na wapinzani wao.

Alisema M1 ni mtu wa karibu na MM kwa hiyo mawasiliano yao hayataweza kutiliwa shaka na mtu yeyote hata wangewasiliana mara nyingi kiasi gani.

MAWASILIANO YAWE USO KWA USO
Lissu alisema watu hao walikubaliana mawasiliano yao yawe kwa kuonana uso kwa uso ama kwa simu na ujumbe mfupi na kwamba Dk Mkumbo (M1) na Kabwe (MM) wanapotaka kukutana na kamati ya kitaifa, mipango itafanywa na M1 kwa siri.

“Mkakati wa mabadiliko 2013 ni mpango haramu na ambao unaichana chana katiba ya chama.. ni mkakati wa vita dhidi ya chama chetu na utaratibu wetu wa kikatiba,” alisema.

Alisema kuwa ibara ya 10.1 (iv) ya kanuni za uendeshaji kazi za chama ambazo ni sehemu ya katiba ya mwaka 2006 inamkataza kiongozi wa Chadema kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana.

Alibainisha kuwa, wanamtandao hao wanaendekeza siasa za udini kwa kusema ‘mtu tunayemtaka (Zitto) kwa kuwa ni muislam, hii ni fursa katika kupata kuungwa mkono na wanachama waislamu ambao wamekuwa na kigugumizi wakidhani waislamu hawatakiwi katika uongozi wa taasisi yetu.’

Alisema wakati ibara ya 10.1 (viii) ya kanuni za uendeshaji inamtaka kila kiongozi wa chama kuwa mkweli na muwazi na kuachana na vikundi, majungu na wadanganyifu, wanamtandao hao wanaeleza utekelezaji wa mkakati wao utafanyika kwa siri.

Pia alisema ibara ya 10.1 (ix) inamtaka kiongozi wa chama asijihusishe na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro, mtandao wao wamesambaza tuhuma za uongo dhidi ya Mbowe huku wakimwelezea kuwa hana mahusiano mema na viongozi wa ngazi za chini.

Kwa mujibu wa ibara ya 10.1 (x) inamtaka kiongozi asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye kanuni.

UAMUZI WA KUWAVUA NYADHIFA
Alisema tuhuma zilizotolewa dhidi ya viongozi wa juu wa chama hazijawahi kutolewa na yeyote kati yao kwenye vikao halali vya chama.

“Wanamtandao hawa wamemtuhumu Mbowe kuwa ni mtu mwenye uzalendo unaotia shaka, mwenye elimu ya ‘magumashi’, mzito kujieleza na mtu mwenye akili ndogo,’ alisema na kuongeza:

“Kama ilivyo kwa binadamu au taasisi yoyote ile, uvumilivu wa chama chetu na viongozi wake wakuu umefika kikomo, kamati kuu kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba ya dharura chini ya ibara ya 6.5.2 (d) imeazimia mambo sita ikiwemo hilo la kuwavua nyadhifa watu hao,” alisema.

Alitaja mengine kuwa ni timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa sekretarieti ya Makao Makuu ya chama na wajumbe wa kamati kuu ifanye uchunguzi wa haraka ili kumtambua M2 ili hatua zichukuliwe dhidi yake.

Pia alisema kamati ya chama ya wabunge imeelekezwa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha Kabwe anavuliwa madaraka yake yote kama Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi Bungeni mapema iwezekanavyo,

HATI ZA TUHUMA NA KUJIELEZA
Alitaja pendekezo lingine kuwa ni viongozi waliotajwa waandikiwe hati zenye tuhuma dhidi yao haraka iwezekanavyo na watakiwe kujieleza kwa nini wasifukuzwe kwenye chama kwa vitendo vyao na wapatiwe fursa za kujitetea.

Mara baada ya utekelezaji wa azimio hilo, Kamati Kuu ikutane kwa dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatma ya watuhumiwa na hatua nyingine zichukuliwe.

Aidha, waraka wa wanaojiita wana-mtandao wa ushindi uwekwe haradhani na usambazwe kwa vyombo vya habari ili Watanzania na wanachama waweze kupima uzito wa mkakati wa umtandao huo na maamuzi ya kamati.

ZITTO NA KITILLA WAOMBA KUJIUZULU
Lissu alisema katika kikao hicho watu hao waliiomba Kamati Kuu iwaruhusu kujiuzulu nyadhifa zao baada ya mkakati wao kukiteka nyara na kukiangamiza chama kujulikanai.

Aidha alisema kwa kuzingatia uzito wa makosa waliyokifanyia chama, kwa kuzingatia nyadhifa zao, uzoefu na katiba, Kamati Kuu iliwakatalia kwa kuwa ingekuwa ni sawa na kuwaruhusu wajiondoe kwenye uongozi wa chama wakiwa na heshima wasiostahili.

Akimwelezea Zitto, mwanasheria huyo alisema mara nyingi amekuwa akisema hadharani kuwa hachukui posho na kuhoji fedha za kutekeleza mkakati huo anazitoa wapi.

Akieleza msimamo wa chama , Mbowe alisema awe yeye au yeyote ndani ya chama hawatakubali mtu, kikundi au mbinu chafu zenye lengo la kukiyumbisha chama.

Alipoulizwa endapo uchunguzi wao ukabaini M2 ni Dk. Slaa watamchukulia hatua, Mbowe alisema wa mujibu wa katiba yao hata akiwa huyo atatimuliwa.

KUNG’ATUKA MADARAKANI DK SLAA NA MBOWE
Mbowe alisema utumishi wa chama cha upinzani ni adhabu na kwamba kama kuna mtu anafikiri ni fursa na starehe hajafahamu.

“Chadema hakuna ukomo katika uongozi sio tu kwa nafasi ya taifa hata wilaya na mkoa, kama mtu ni mtendaji haitaamuliwa aondolewe eti kwa sababu amekaa sana, halafu tukampa mtu mwenye nia ovu,” alisema na kuongeza:

“Kuwa kiongozi wa upinzani sio starehe, kama kupigwa mabomu ni starehe, kama kufungwa na kupata kashfa mnaona ni starehe basi huyo mtu atafakari mara mbili, tunaishi kwa visasi, kama kuna mtu mwenye sifa na mapenzi mema anayetaka cheo hatutasita kumpigia debe, lakini hatutaweza kugawa vyeo eti kwa sababu tu mtu anamalengo maovu,” alisema.

Alisema kutafuta uongozi ndani ya Chadema au taasisi haimaanishi akipasue au kukigawa.

“Ngoja niwaambie leo ukikiua Chadema nchi itachukua zaidi ya miaka 20 kukiunda chama kingine cha upinzani kama Chadema, kama hamjui hili waulizeni wapinzani wengine,” alisema.

MSIMAMO WA MBOWE
Amesema ataendelea kuwa mwenyekiti wa chama hicho mpaka hapo wanachama wake wakitaka akae pembeni na kuwataka wanaotaka uongozi wafuate njia ya wazi ya katiba na sio njia za kihuni.

Mbowe alibainisha kuwa, mikakati ya wanamtandao huo inafadhiliwa na watu wa ndani na wa vyama vingine.

Alisema Chadema ni mpango wa Mungu na kwamba yeyote anayetaka kuibomoa amepotea.
“Watu hubadilika walikuwa wazuri lakini leo hii sio, hii ni hatari unakaa nao unafikiri mna malengo ya aina moja kumbe wanataka kukuangamiza, kuna watu walikuwa wema jana, lakini leo ni hatari, ila bora tumjue yupo CCM kuliko ndani ya chama,” alisema.

Alisema kuna watu (bila kuwataja) wamekataa kufika bei ndio maana sasa wanapigwa vita.

Mbowe alisema waraka wa siri uliopo kwenye mitandao ya kijamii ambao unamzungumzia Zitto hautokani na chama na kwamba Chadema haiwezi kumhukumu.
Alisema Zitto aliwaeleza kuwa na waraka unaomhusu kwa sababu umemtaja lakini hajawahi kuuona.


ARFI AJIUZULU

Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda, amejiuzulu nafasi hiyo kuanzia jana.
Arfi ametangaza kujiuzulu muda mfupi baada ya Mbowe kuulizwa na mmoja wa waandishi kutokwepo kwa makamu huyo kwenye kikao hicho.

Akijibu, Mbowe alisema kikao hicho ni cha mwenyekiti hivyo haikuwa na ulazima kila mtu awepo.

Katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii, Arfi ameeleza sababu ya kuchukua uamuzi huo kuwa kuwa ni kuchoshwa na unafiki unaoendelea ndani ya Chadema. Alisema kuwa hayupo tayari kuchaguliwa marafiki.

“Kwa kipindi kirefu zimekuwepo shutma dhidi yangu na kutiliwa mashaka mahusiano yangu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na kulijadili katika vikao kadhaa Mpanda na Dar es Salaam, bado yapo mashaka kwa nini alipita bila kupingwa hayo yalikua maamuzi ya Wanampanda, kwenu imekuwa ni tatizo,” imesema sehemu ya taaifa hiyo na kuongeza:

“Lakini hamsemi kwa nini majimbo mengine 16 nchini yalipita bila kupingwa, mlikua wapi na nani alaumiwe huu ni unafiki wa kupindukia.”
Alisema Chadema imechukizwa kwa nini alihoji kauli ya Muasisi wa Chama, Edwin Mtei kuwachagulia viongozi.

“Naomba ifahamike wazi kwamba huu ni mtazamo wangu na utabakia hivyo siku zote kwa chama cha demokrasia kutoruhusu uongozi wa kiimla kwa kukidhi matakwa ya Waasisi ambao huvigeuza vyama kuwa mali binafsi,” imesema.

Katika taarifa hiyo Arfi ameeleza kuwa kwa kusema na kusimamia ukweli daima itabakia kuwa lengo lake katika maisha yake siku zote hata kama itamgharimu maisha.

Akizungumza na NIPASHE, Mkumbo alisema sasa hivi ni mapema mno kuzungumzia suala hilo kwa kuwa huo ni muda wa kutafakari.
Alisema kwa mujibu wa taratibu za chama ni vyema kuheshimu maamuzi. Hata hivyo aliahidi kuzungumzia suala hilo leo.

Zitto na Mwigamba, hawakuweza kupatikana baada ya simu zao kuita bila kupokelewa.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment