Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, December 16, 2013

CUF:Serikali Umoja Kitaifa itanusuru Katiba Mpya

NA MUHIBU SAID

16th December 2013


Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
Chama  cha Wananchi (CUF) kimesema mchakato wa katiba mpya unakabiliwa na vikwazo vingi, ambavyo vinafanya isiweze kupatikana Aprili 26, mwakani, hivyo kimetahadharisha Tanzania kuwa mbioni kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa.

Kutokana na hali hiyo, kimemshauri Rais Jakaya Kikwete kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kusimamia vizuri upatikanaji wa katiba mpya na kuhakikisha maridhiano na mshikamano wa kitaifa katika kipindi hiki nyeti vinakuwapo nchini.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana na kushauri serikali hiyo iundwe baada ya Rais Kikwete kushauriana na wadau.

Pia ameshauri jukumu lingine la serikali hiyo liwe ni kupata daftari safi la wapigakura, kuunda tume huru ya uchaguzi na kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki mwaka 2015.

Pia iimarishe uwajibikaji wa vyombo vya dola na viongozi, ishughulikie kadhia ya matumizi mabaya ya fedha za umma na iimarishe ukusanyaji wa mapato ya serikali ili miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara na ufuaji wa umeme ikamilishwe.

“…Ni wazi katiba mpya haiwezi kupatikana ifikapo tarehe 26 Aprili 2014 wakati tunasherehekea miaka 50 ya Muungano,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema Watanzania wengi wangependa zoezi la kupata katiba mpya likamilike kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Lakini akasema kwa hali halisi ilivyo, zoezi hilo haliwezi kukamilika kwa ufanisi kabla ya mwaka huo.

Alisema sheria ya mabadiliko ya katiba inaeleza kuwa ikiwa katiba mpya haikupitishwa kwenye kura ya maoni, katiba ya sasa itaendelea kutumika.

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, katika mchakato wa kupata katiba mpya, maoni yaliyotolewa na wananchi na rasimu ya katiba inayotokana nayo imebainisha  Watanzania hawaitaki katiba ya sasa.

Hivyo, akasema kufanya uchaguzi kwa kutumia katiba ya sasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyopo hakutakubalika na wananchi na kunaweza kuwa chanzo cha mgogoro mkubwa wa kisiasa.

Pia alisema kura ya maoni inakabiliwa na kikwazo cha kutokuwapo kwa daftari la kudumu la wapigakura lililoandikisha wapigakura wote.

Vilevile, alisema daftari la wapigakura halijaboreshwa na kuandikisha wapigakura wapya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Alisema Februari, Rais Kikwetew alitangaza kuwa vitambulisho vya taifa, ambavyo vinatumia alama ya mwili ndivyo vitakavyotumiwa kwa kupiga kura ya maoni na uchaguzi mkuu.

Lipumba alisema katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete pia alisema Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) itashirikiana na NEC katika utoaji wa vitambulisho vya taifa, ambavyo pia vitatumika kupigia kura.

Hata hivyo, alisema zoezi la kuwapa wananchi vitambulisho vya taifa linaenda taratibu sana, huku Nida ikiwa haijakamilisha kuvitoa hata kwa Wilaya za Dar es Salaam.

“Kwa kasi hii ya uandikishaji na utoaji wa vitambulisho vya kitaifa, zoezi hili halitakamilika katika miaka miwili inayokuja. Itafika 2015 na wananchi wengi wenye umri wa miaka 18 watakuwa hawajapata vitambulisho vya taifa,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema zaidi ya hivyo, vitambulisho vya NEC havikidhi mahitaji na kwamba, vinaghushiwa kwa urahisi sana.

Lipumba alisema pia wadau wengi hawana imani na daftari la tume hiyo, hivyo akashauri vitambulisho vya Nida vyenye alama za mwili ndivyo vitumiwe kama vya kupigia kura.
Alisema kura ya maoni kuhusu katiba haiwezi kuendeshwa kwa ufanisi bila kuwa na daftari la wapigakura linaloaminika.

Lipumba alisema daftari la ZEC linawanyima wananchi wengi wa Zanzibar kuandikishwa kupiga kura kwa madai kuwa hawana vitambulisho vya ukaazi (Zan ID).

Alisema bila kuwapo kwa rasimu ya katiba ya Tanzania Bara na marekebisho ya katiba ya Zanzibar isikinzane na katiba ya Muungano, zoezi la kupata dira na mwongozo wa kusimamia utawala, uchumi na siasa za Watanzaniua haujakamilika.

Lipumba alisema Zanzibar wana katiba, lakini Tanganyika haina wala mchakato wa kuipata haujaanza.

Alisema rasimu ya katiba ya Muungano ina upungufu mkubwa, mambo mengi, ukiwamo mfumo wa Muungano, mambo ya Muungano, ukuu wa katiba ya Muungano, mapato ya kugharimia Muungano yanahitaji mjadala wa kina ili kufikia muafaka.

Aidha, alisema Bunge Maalumu la Katiba litakuwa na kazi kubwa ya kupata muafaka kuhusu mambo hayo muhimu na kwamba, hata wakifikia muafaka na kupata katiba mpya, mapendekezo yaliyomo katika rasimu ya katiba yatahitaji mabadiliko makubwa ya kisheria na kitaasisi ili kuitekeleza.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment