LAITI kama wanasiasa wetu wangekuwa wanatumia uhuru na haki yao ya kujieleza kwa kusema ukweli mtupu, matatizo mengi yanayolalamikiwa kila siku na wananchi, yasingekuwepo.
Wale wenye wajibu wa kuwapatia huduma wananchi wasingekuwa na popote pa kujificha. Watake wasitake wangewajibika.
Hatufikii hapo – ambapo ni kipimo kizuri cha kiongozi muadilifu – kwa sababu wapo wanasiasa wanaoujua ukweli wa jambo, lakini kwa maslahi binafsi, wanauficha.
Nimeliona hili niliposikiliza mjadala wa muswada wa sheria ya Kura ya Maoni uliofanyika bungeni wiki iliyopita.
Shamsi Vuai Nahodha, ambaye sasa ni kiongozi mkubwa aliyeanzia kuwa msaidizi mkuu wa Rais wa Zanzibar, kwenye awamu ya uongozi ya Amani Abeid Karume, naye alijadili muswada huo ambao hatimaye ulipitishwa na Bunge.
Kwa miaka kumi mfululizo, kutoka Novemba 2000 hadi Novemba 2010, alikuwa waziri kiongozi Zanzibar.
Alishika nafasi muhimu ya kumshauri rais kuleta mabadiliko. Angeweza kumshauri kutunga sheria za maana kwa maendeleo ya jamii.
Angejua kuwa kukitendeka mambo ya ovyo, watabeba pamoja lawama na likitendwa lililo jema, watasifiwa pamoja.
Chini ya uongozi wao, waliridhia sheria ya kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi ambayo ilipitishwa na Baraza la Wawakilishi mwaka 2005.
Sheria hii ilipingwa. Wakati huo hapakuwa na kuaminiana kati ya viongozi wa serikali na hasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na chama kikuu cha upinzani – Chama cha Wananchi (CUF).
Siasa zilikuwa za chuki na fitina, zilizojaa ubaguzi, dhulma na utamaduni wa watawala kupotosha mambo kwa maslahi ya kisiasa.
Viongozi wa CUF walipoipinga, walisema japo inawezekana sheria hiyo kuwa nzuri, hofu yao ni kuja kutumiwa vibaya; kukandamiza haki za watu wasioaminika kwa CCM.
Viongozi wa serikali na CCM wakajitetea wakisema haitatumika vibaya. Kinyume chake, itasaidia kumaliza matatizo yanayosababishwa na kutokuwepo kwake. Wananchi watatambuliwa, kusajiliwa na kupewa kitambulisho (ZAN-ID).
Ni maelezo yaliyonyooka. Unaona namna viongozi wa serikali walivyo makini katika kutatua matatizo.
Sheria ilitaka kila Mzanzibari aliyefikia umri wa miaka 18 kuendelea, atambuliwe, kusajiliwa na kupatiwa kitambulisho. Sheria ikaelekeza kuwa ni kosa la jinai kwa mtu kutokuwa na kitambulisho hicho wakati amefikia umri.
Akikamatwa, na kushitakiwa, na akithibitika ametenda kosa kwa kutokuwa na ZAN-ID, atastahili kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini, au adhabu zote mbili kwa pamoja.
Harakaharaka serikali ilifungamanisha ZAN-ID na haki ya mwananchi kuwa mpigakura. Awe nacho kwanza ndipo aandikishwe na kuingizwa kwenye Daftari la Kudumu la WapigaKura (DKWK).
Mfungamano huu ulipingwa. Serikali ikalazimisha. Ukaleta matatizo wakati Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilipoanza kuandikisha wapigakura. Tume wakasema kazi yao inatatizwa. Hatimaye serikali iliondoa sharti lile. Uandikishaji ukaendelea.
Ulikuwa ni mwaka mbaya katika historia ya ukuzaji wa demokrasia Zanzibar. Ulizuka mgogoro mkubwa katika kupata daftari la wapigakura. Serikali haikutaka lihakikiwe. Ikasingizia eti haina fedha za kugharamia uhakiki.
Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Mpango wa Maendeleo (UNDP) ukashawishi nchi wahisani za magharibi kusaidia. Fedha zikapatikana. Kazi ya kuhakiki ikakumbwa na mizengwe mingi.
Tatizo kubwa CCM waliona dhamira zao za kupandikiza wapigakura mamluki kwenye daftari zitashindwa. Wataadhirika. Itaharibu mipango yao ya kulazimisha ushindi kwenye uchaguzi.
Uhakiki ulifanyika kwa mazingira magumu. Vitisho viliwatia hofu wataalamu waliokuja kutoka Afrika Kusini. Waligundua kuwa waliitwa kufanya kazi isiyoipendeza serikali.
Tume katika ripoti yake ilithibitisha kuwa zaidi ya watu 3,000 waliandikishwa zaidi ya mara moja. Bado hakuna aliyeshitakiwa licha ya uthibitisho huo.
Maandalizi ya uchaguzi wa 2010 yalipoanza, serikali ilitangaza kuwa ZAN-ID itakuwa kiingilio cha mtu kuandikishwa kuwa mpigakura.
Wakahalalisha uchafu. Kufikia uchaguzi, wengi wa wale waliopiga kura 2005, wakawa wamenyongwa. Walikosa kitambulisho, wakashindwa kuandikishwa. Kwa hiyo? Hawakupiga kura.
Yote haya Shamsi anayajua. Alitetea kitambulisho. Akahakikishia wananchi watapewa. Alipoambiwa hata wenye sifa wananyimwa akaendelea kuahidi kila mwenye haki atapata. Hata jimboni kwake tulikuta mamia ya wananchi hawakupiga kura 2010. Hakujali.
Kaka yangu ni mpigakura Mwanakwerekwe, jimbo la Shamsi. Kwa kuwa alikuwa mgonjwa wa mguu, nililazimika kumsaidia kufika kituoni akapige kura. Tulifika nusu saa kabla ya muda wa kupiga kura kwisha. Uchafu mtupu. Watu wanapiga kura bila ya shahada. Wasimamizi hawajali kama walishapiga kura kwingine.
Niliyoyaona uchaguzi wa 2000, nikayaona Mwanakwerekwe. Mtu mmoja kura mia. Makundi ya watu wanaingizwa kituoni chini ya ulinzi wa polisi wa serikali. Wanapiga kura.
Ni jimboni kwa Waziri Kiongozi na Mjumbe wa Kamati Kuu CCM. Anatafuta kura. Ilipothibitika zake hazikutosha, akazira. Wakaitwa askari wa kutuliza ghasia – naona wanazianzisha wao. Wananchi walio karibu wakafukuzwa na kukimbilia msikitini, karibu na kituo.
FFU wakafyatua risasi za mipira kuwafukuza. Hali ilipotulia, Shamsi akatangazwa ameshinda uwakilishi.
Haya yatamchukiza Shamsi. Hawezi kuyasema haya, wala kusikia yakisemwa. Yanaumiza. Kwake yanamuanika. Na hii ndiyo kadhia ya kweli ya kitambulisho. Kinatumika kuzuia haki za wananchi kuchagua viongozi wawatakao.
Shamsi na CCM hawajali. Yao yanatimia. Ushindi wa kishindo unapatikana. Wanatoa visingizio mbalimbali kwa lugha tamu kuhalalisha uchafu. Wanachokifanya ni kuuficha ukweli.
Wabunge wenzao wa CUF wanataka mabadiliko. Wao wanataka uchafu huo urithiwe katika Kura ya Maoni ya kuamua hatima ya Katiba ya Muungano. Kusibadilike chochote. Utaratibu uwe uleule – kulitegemea daftari la Zanzibar wanalojua li chafu.
Shamsi anaungana na wabunge Abdalla Sharia Ame wa Dimani, Yahya Kassim Issa (Chwaka), Jadi Simai Jadi (Mkwajuni) kutetea kitambulisho. Wanasema hakina tatizo. Wanatetea sheria ya ukaazi ya miaka mitatu jimboni. Wanasema tatizo watu hawataki kufuata sheria.
Kwa demokrasia ya Zanzibar na Afrika ambayo inakandamiza wasioridhia watawala, ni dhambi kuruhusu Wazanzibari walioko nje, kupiga kura kwao. Haishangazi. Kama hata waliomo ndani ya nchi wanatafutiwa sababu wasipige kura, itakuwa hao?
Kwa kuyajua haya, Mussa Haji Kombo (Chake Chake) akasema daftari la Zanzibar lisitumike kwa kura ya maoni. Tume iandikishe wapigakura kwa utaratibu wake ili asibakie mwenye haki nje ya kufanya uamuzi wa katiba mpya.
Shamsi anataka mfumo mpya wa uchaguzi. Anaomba aungwe mkono na wawakilishi – maana yeye ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi – atakapopeleka hoja binafsi kutaka mfumo wa uwakilishi.
Kwamba akishachaguliwa rais, wawakilishi wapatikane kwa kuangalia kura za urais. Kiasi cha kura ndio kiamue idadi ya wawakilishi kwa kila chama.
Kwa heshima na taadhima, hili lina maana gani wakati wa Kura ya Maoni? Hili si ni jambo la kujadiliwa barazani kule Chukwani?
Kura ya maoni ya Tanzania nzima kama alivyosema mbunge mpya wa Chambani, Yussuf Salim Hussein.
Anasema “enyi mnaoficha ukweli, mjue mtajibu mbele ya haki. Katiba si ya vyama, si ya Zanzibar wala Bara. Ni ya jamhuri. Kila mtu ashiriki kuiamua.
Chanzo: Mawio
No comments :
Post a Comment