NA MUHIBU SAID
20th December 2013
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alisema jana ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, kuwa Ikulu inaheshimu maoni na mawazo ya Profesa Lipumba na yeye kama kiongozi makini wa upinzani.
Lakini akasema haikubaliani na maoni na mawazo yake hayo kwa kuwa kwa sasa hakuna mazingira yanayoruhusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Rweyemamu alisema serikali iliyopo madarakani haijashindwa kusimamia na kuukamilisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ndiyo maana tangu uanze bado haujakwama.
Hivyo, amemshauri Profesa Lipumba kusubiri hadi tarehe iliyotangazwa na Rais Kikwete kama Katiba Mpya itakuwapo au la na haoni sababu kuwa na haraka na jambo hilo.
“Asubiri mpaka tarehe hiyo 26 Aprili, 2014 kama Katiba Mpya itakuwapo au la. Haraka ya nini?” alihoji Rweyemamu.
Alisema hoja ya mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya kuwa na vikwazo vingi vinavyosababisha isiweze kupatikana mwakani, haina msingi, kwa kuwa vikwazo ni sehemu ya maisha na mchakato.
“Hata kama unaoa utapata tu vikwazo. Tunamtaka (Profesa Lipumba) aendelee kuunga mkono mchakato, asiruhusu kuwa kikwazo,” alisema Rweyemamu.
Kauli hiyo imetolewa na Ikulu siku sita baada ya Profesa Lipumba kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema mchakato wa Katiba Mpya una vikwazo vingi na kwamba, haiwezi kupatikana mwakani kama Rais Kikwete alivyoahidi hivyo, kuna haja ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa Profesa Lipumba kutoa kauli hiyo.
Mei, mwaka huu, alitoa tamko kama hilo alipoonyesha wasiwasi wake kuhusu upatikanaji wa Katiba Mpya akadai ni janja ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumwongezea muda Rais Kikwete.
Profesa Lipumba alisema amekuwa akiutafakari kwa kina mchakato wa Katiba Mpya kama unaweza kukamilika mwakani, lakini jibu linalomjia, hakuna.
Alitaja baadhi ya vikwazo, ambavyo vinaweza kukwamisha kupatikana kwa Katiba Mpya kuwa ni Daftari la Kudumu la Wapigakura kuwa halijaboreshwa na kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho vya taifa, ambavyo vitatumika kupigia kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya.
Wakati Profesa Lipumba akisema hayo, tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeeleza kuwa haina mpango kwa sasa wa kuboresha Daftari la Kudumu Wapigakura kwa ajili ya kura za maoni kwa sababu muda uliobaki ni mfupi.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, alisema itakuwa vigumu kuboresha daftari hilo kwa ajili ya upigaji wa kura za maoni utakaofanyika mwanzoni mwa mwakani kwa sababu muda uliobaki ni mfupi na hakuna fedha za kufanya hivyo.
Pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alipoulizwa bungeni kuhusiana na kauli ya Jaji Lubuva alisema msimamo uliotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusiana na daftari hilo ndiyo msimamo hasa wa serikali.
Desemba 5, mwaka huu, Pinda alivihakikishia vyama vya siasa na Watanzania kwamba, daftari hulo litaboreshwa kabla ya upigaji kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya.
Pinda alisema hayo wakati akihitimisha hotuba yake ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013 baada ya suala la daftari hilo kuibua mvutano mkali baina ya wabunge na serikali.
Profesa Lipumba alisema kutokana na hali ilivyo sasa ni wazi Katiba Mpya haiwezi kupatikana kabla ya mwaka 2015, hivyo kuna haja ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kushughulikia mchakato wa Katiba na kuimarisha uwajibikaji wa vyombo vya dola.
Lipumba alisema: “Rasimu ya mwisho ya Tume ya Katiba itapatikana mwezi huu, huku na Rais anawajibika kukamilisha undaji wa Bunge la Katiba kwa kuteuwa wabunge 201 baada ya kupata mapendekezo, hivyo itakuwa bahati Bunge la Katiba kuanza mwisho wa mwezi Januari kitu ambacho kinarefusha mchakato huu.”
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment