NA WAANDISHI WETU
23rd December 2013
Miaka minane mawaziri watano, ajaye wa sita
Wadau wasema cha msingi ni mifumo sera, sheria
Wadau wasema cha msingi ni mifumo sera, sheria
Idadi hiyo kubwa ya mawaziri wanaokaa kwa muda mfupi bila kutekeleza majukumu yao waliyojipangia ni ishara dhahiri kwamba wizara hiyo ina changamoto kubwa.
Tangu Rais Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, wizara hiyo imeshaongozwa na mawaziri watano, Anthony Diallo, Profesa Jumanne Maghembe, Shamsa Mwangunga, Ezekiel Maige na Balozi Khamis Kagasheki wakati makatibu wakuu ni wanne Saleh Pamba, Blandina Nyoni, Balozi Dk. Ladslaus Komba na Maimuna Tarishi.
Waziri wa kwanza kuteuliwa na Rais Kikwete katika baraza lake la kwanza la mawaziri ni Diallo kuanzia mwaka 2006/2008, akafuatiwa na Profesa Maghembe 2008/2009, Mwangunga 2009/2010, Ezekiel Maige 2011/2012 na kurithiwa na Balozi Kagasheki.
Sababu za kuondolewa Diallo hazikuelezwa, lakini alipondolewa ni Rais alipolivunja na kuliunda upya Baraza la mawaziri baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa mwaka 2008. Alijiuzulu sambamba na Dk Ibarahim Msabaha (Ushirikiano Afrika Mashariki) na Nazir Karamagi (Nishati na Madini).
Profesa Maghembe naye aliondolewa wizarani hapo na kupelekwa katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na nafasi yake kujazwa na Mwangunga.
Mwangunga hakukaa baada ya mwaka 2010 kushindwa katika kura za maoni ndani ya CCM na hivyo kukosa sifa ya kuwa mbunge.
Baada ya uchaguzi mkuu wa 2010, Maige akiwa Naibu waziri wa wizara hiyo, aliteuliwa kuwa waziri kamili, lakini aliondolewa mwaka 2012 Rais alipofanya mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri kufuatia mawaziri kadhaa kuandamwa na tuhuma za kushindwa kuwajibika zilizobainishwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na kamati za Bunge.
Maige alituhumiwa na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji.
Ripoti ya CAG ilibaini kuwa Wizara hiyo ilipoteza kiasi kikubwa cha fedha baada ya kufanya uamuzi wa upendeleo wa kutoa kiwango cha chini cha mrahaba kwamauzo ya misitu. Maige pia alituhumiwa kushindwa kuwajibika katika kashfa ya utoroshaji wa wanyama hai kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia)
Mawaziri wengine ambao waliondolewa sambamba na Maige ni William Ngeleja (Nishati na Madini), Omar Nundu (Uchukuzi), Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) na Mustafa Mkulo (Fedha).
Maige baada ya kuondolewa, nafasi yake ilichukuliwa na Balozi Kagasheki ambaye alikuwa Naibu wake, ambaye alijipatia sifa kubwa kutoka kwa wananchi na wadau wengine kutokana na jitihada zake za kupambana na vitendo vya ujangili hususani mauaji ya kasi kubwa ya tembo katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Ni jitihada hizo za Kagasheki zilizochangia kwa kiasi kikubwa uamuzi wa serikali wa kuanzisha Operesheni Tokomeza Majangili ili kunusuru tembo hao kutoweka nchini baada ya takwimu zilizotokana na tafiti kuonyesha kuwa takribani tembo 30 wanauawa nchini kila siku.
Ni operesheni hiyo iliyomuondoa Balozi Kagasheki katika wizara hiyo kutokana na kulalamikiwa na wananchi, makundi ya watetezi wa haki za binadamu na wabunge kwamba ilitekelezwa kinyume cha haki za binadamu.
Operesheni hiyo haikumwondoa Kagasheki peke yake bali pia iliwang’oa mawaziri wengine watatu ambao ni wa Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Mathayo David Mathayo; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Hatua ya kung’oka kwa mawaziri hao wanne sasa ni dhahiri kuwa Rais Jakaya Kikwete atalazimika kikatiba kuwateua watu wengine wenye nyadhifa za ubunge kujaza nafasi hizo wakati wowote kuanzia sasa.
Hata hivyo, kazi kubwa itakuwa kwa atakayeteuliwa kuiongoza wizara hiyo ambayo imeonyesha kuwa ngumu kuiongoza.
Kama ilivyotokea kwa Kagasheki akamrithi Maige, yanaweza kutokea maajabu Naibu wa sasa wa wizara hiyo, Lazaro Nyalandu, kupandishwa kuwa waziri kamili wa wizara hiyo.
Bado changamoto za kuiongoza wizara hiyo zikiwamo za usimamizi wa vitalu, utoroshaji wa magogo kwenda nje ya nchi, utoroshaji wanyama hai pamoja na ujangili hususani wa tembo zitamsubiri waziri wa sita kuiongoza wizara hiyo.
Kama atashindwa kukabiliana nazo, yanaweza kutokea mazingira mengine ya kuwa na waziri mwingine wa saba kabla ya serikali ya awamu ya nne kumaliza muda wake mwaka 2015.
WADAU WAZUNGUMZA
Katika hatua nyingine; wadau wa utalii wamezungumzia changamoto zinazowapata mawaziri wanaoiongoza wizara hiyo na kulazimika kuondoka baada ya muda mfupi.
Aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo na mfanyabiashara ya utalii, Aloyce Kimaro, alisema wizara hiyo ni ngumu kutokana na kuwa na vishawishi vingi.
Alisema inahitaji mtu ambaye ameshiba kwa maana ya kujitosheleza kimaisha na asiye na tamaa wala papara na kwamba kwa sasa ni mtihani mgumu kubashiri atakayeteuliwa atakuwa ni mtu wa aina gani.
“Balozi Khamis Kagasheki aliimudu wizara hiyo na ni mtu aliyetosheka, hana tamaa za ovyo, lakini imekuwa bahati mbaya kwa waliopewa jukumu la kuendesha Operesheni Tokomeza wamekwenda kinyume na malengo husika,” alisema.
Alisema tatizo kubwa kwa sasa ni kukosekana kwa nidhamu ya kazi na kila mtu aliyemtumishi wa serijkali kujifanyia atakavyo na anapowekwa Waziri muajibikaji huambiwa wamepita wengi nawe utaondoka na kujikuta watu wazuri wakiwekwa kando kila wakati.
Alisema kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni kubadili mfumo zima wa serikali kwani uliopo umeshusha nidhamu ya serikali na kwamba kubadili mawaziri kila wakati si suluhisho la matatizo ya Watanzania.
Paul Mgana, mdau wa utalii mkoani Kilimanjaro, alisema kubadili mawaziri kila mara ni kuweka utalii rehani.
Alisema kila waziri anayekuja anahitaji muda wa kuifahamu wizara na kujifunza jinsi ya kufanyakazi kwa kuwa wengi si wataalamu katika eneo husika, hivyo muda unapotea na pale anapoanza kumudu naye huondolewa na kuwekwa mwingine.
Nao wasomi wamesema kuna umuhimu wa kuwa na mfumo mpya wa uendeshaji wa wizara hiyo.
Wamesema kuvunja kwa mifumo iliyopo sasa ya uendeshaji wa wizara nyeti, ndiyo suluhisho pekee.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema, kitendo cha wizara hiyo kuendeshwa na mawaziri watano mpaka sasa kinaonyesha unyeti wa wizara yenyewe.
“Ni wizara nyeti inayogusa maslahi ya watu wengi na tatizo lililopo pale, ni la wizara kutoendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni, ila kwa maslahi ya watu wachache,” alisema.
Dk. Bana alisema namna mambo yanavyoendeshwa katika wizara hiyo, kunazua maswali ambayo yanahitaji mfumo unaoeleweka kuweza kuyadhibiti.
Alisema, balozi Hamis Kagasheki alijitahidi kufanya kazi kwa maslahi ya nchi, ikiwa ni pamoja na kukamata nyara za serikali, lakini hakuungwa mkono na viongozi wenzake wakiwemo wabunge waliosimama kupiga kelele ya kumtaka awajibike.
“Hatukuona mbunge aliyesimama na kusema atakavyosaidia kuupiga vita mtandao unaoihujumu wizara hiyo, iliyogubikwa na mitandao ya rushwa na ufisadi, na ilionekana dhahiri kuwa kila mtu alikuwa anakwepa kuuingia mtandao huo,” alisema.
Dk. Bana alisema rushwa na ufisadi uliojengwa kwa miaka mingi kwenye maeneo ya maliasili, vitalu vya uwindaji na utoroshwaji wa wanyama kwenda uarabuni, ni kansa iliyowatisha wengi, kiasi cha kutomuunga mkono balozi Kagasheki.
Alisema, muarobaini wa mtandao wa ufisadi uliopo katika wizara hiyo, utapatikana kwa kufumua mifumo, sera, sheria na kanuni mbalimbali zinazotoa fursa kwa mitandao ya rushwa kuendelea kuwepo, katika wizara hiyo.
“Na ndiyo maana ninaunga mkono hatua ya serikali ya kuunda tume ya kimahakama ya kufanyika uchunguzi mwingine, kwa kuwa kinachoonekana kufanywa na tume hii, ilikuwa ni kukomoa watu, baada ya fursa kupatikana,” alisema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala UDSM, Bashiru Ally, alisema tatizo la kimfumo ndilo linasababisha na litaendelea kusababisha mabadiliko si katika wizara hiyo tu, bali kwenye wizara zote zenye kuchangia maendeleo makubwa ya watu.
“Mabadiliko hayajafanyika katika wizara hiyo pekee, bali angalia wizara zote zinazogusa maslahi ya watu, kama vile ardhi, na ile ya madini na nishati, utaona mabadiliko ya mawaziri yamefanyika karibu mara mbili au tatu,” alisema.
Alisema tatizo hili litamalizika kwa kufanyia kazi tatizo la kimfumo na hasa kwa kuzifanya sekta za ndani za binafsi au za serikali kuwa na uwezo wa kushiriki moja kwa moja (Domestic private Capital, Public Capital ) kuwekeza kwenye sekta zote zinazogusa maendeleo ya nchi.
Alisema kutokuwepo kwa udhibiti wa rasilimali katika sekta muhimu kwa maendeleo ya nchi kunazalisha kundi la watu wenye fedha, ambao wanaweza kutuchagulia siku moja rais, waziri mkuu au mtu wa kusimamia wizara nyeti kwa maslahi yao.
Imeandikwa na Gwamaka Alipipi, Salome Kitomari na Raphael Kibiriti.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment