NA MUHIBU SAID
31st December 2013
Uraia mmoja
Spika, naibu spika wasitokane na chama
Mbunge kuwajibishwa na wananchi
Usalama wa taifa, polisi moja
Ofisi ya msajili wa vyama kujitegemea
Haki za binadamu zaboreshwa zaidi
Spika, naibu spika wasitokane na chama
Mbunge kuwajibishwa na wananchi
Usalama wa taifa, polisi moja
Ofisi ya msajili wa vyama kujitegemea
Haki za binadamu zaboreshwa zaidi
Pendekezo hilo limesisitizwa kutokana na maoni ya Tume kuhusu ugumu uliopo katika mahitaji ya ukarabati wa yaliyomo kwenye orodha ya mambo ya Muungano ili kuendelea na muundo wa Muungano wa serikali mbili.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, alisema hayo katika hafla ya kukabidhi ripoti ya Tume kwa Rais Kikwete na Dk. Shein, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema tathmini ya Tume ni kwamba, ukarabati mkubwa unahitajika ili kuendelea na muundo wa serikali mbili na kwamba, maeneo mawili makubwa yanahitaji mabadiliko.
Jaji Warioba alisema jambo la kwanza ni kuwa na mambo ya kutosha kwenye orodha ya Muungano, ikiwa ni pamoja na mambo ya maendeleo na kiuchumi.
Hata hivyo, alisema jambo hilo likifanyika, litazidisha malalamiko kwa upande wa Zanzibar kuwa hadhi na madaraka yake yanazidi kupotea.
Pia alisema mambo ya Muungano yakipunguzwa sana, serikali ya Muungano itakuwa inashughulika zaidi na mambo ya Tanganyika na Zanzibar itaona Tanganyika ndiyo Muungano.
“Lakini kwa upande mwingine, Tanganyika nayo itaona si haki nayo isiwe na uhuru wa kuendesha mambo yake kama ilivyo kwa Zanzibar,” alisema Jaji Warioba.
Alisema jambo la pili ni kuondoa mgongano na mgogoro wa Kikatiba, ikiwa na maana Zanzibar kubadili katiba yake ili Zanzibar na Tanganyika ziwe ni sehemu za nchi moja badala ya kuwa nchi kamili.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kama Zanzibar na Tanganyika zikiwa nchi kamili, haitawezekana nchi moja ikawa na hadhi na uhuru wake na nchi nyingine isiwe na hadhi na uhuru wake.
“Kwa tathmini ya Tume, kwa hali halisi, tunaona ukarabati huo ni mgumu. Hii ndiyo sababu kubwa ya kupendekeza muundo wa serikali tatu ili pande zote mbili ziwe na hadhi sawa. Kila upande utashughulikia mambo yasiyo ya Muungano na serikali ya Muungano itabaki na mambo machache ya msingi na ambayo yanaunganisha taifa,” alisema Jaji Warioba.
Alisema wakati Tume inazindua rasimu ya kwanza ya katiba mpya, walisema hawakupendekeza kuendelea kuwa na muundo wa serikali mbili kwa sababu mbalimbali.
Jaji Warioba alisema walichokisema ni kuwa kuendelea kwa serikali mbili kulihitaji ukarabati mkubwa ambao walifikiri hautawezekana.
Alisema mabaraza ya katiba yalitoa maoni mengi ambayo yalilazimu Tume kufanya tena uchambuzi wa kina.
Jaji Warioba alisema kama ilivyokuwa katika rasimu ya kwanza ya katiba mpya, suala la Muungano ndilo lililochukua muda mwingi wa Tume.
Alisema wananchi wengi walitoa maoni kuhusu Muungano, lakini wengi wao walijikita kwenye muundo wake.
Jaji Warioba alisema kwa Tanzania Bara, wananchi zaidi ya 39,000 walitoa maoni kuhusu Muungano na kati ya hao, karibu 27,000 walizungumzia muundo.
Alisema kwa Zanzibar, wananchi karibu wote walitoa maoni walijikita kwenye suala la Muungano na kwamba, kati ya wananchi karibu 38,000 waliotoa maoni, 19,000 walitoa maoni kuhusu muundo wa Muungano.
Akielezea mchanganuo wa takwimu hizo, alisema kwa upande wa Tanzania Bara, asilimia 13 walitaka serikali moja, wakati asilimia 24 serikali mbili na asilimia 61 serikali tatu.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, asilimia 34 walipendekeza serikali mbili, asilimia 60 Muungano wa Mkataba na asilimia 0.1 (watu 25) serikali moja.
Aidha, alisema taasisi nyingi kama vile vyama vya siasa, asasi za kiraia na jumuiya za kidini zilipendekeza muundo wa serikali tatu.
Alisema baadhi ya taasisi za kiserikali, ama moja kwa moja au kwa tafsiri ya mapendekezo yao, pia zilipendekeza serikali tatu.
“Kwa mfano, Baraza la Wawakilishi Zanzibar lilipendekeza kuwapo kwa mamlaka huru ya Zanzibar, mamlaka huru ya Tanganyika na mamlaka ya Muungano na iwekwe wazi maeneo, uwezo, nguvu, utendaji na mipaka ya kila mamlaka,” alisema Jaji Warioba.
Alisema pia Ofisi ya Waziri Mkuu imependekeza mfumo wa serikali tatu ili kuondoa kero za Muungano.
Pia alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imependekeza kuwapo kwa serikali tatu ili kutoa majibu ya kero zilizopo na kuleta utulivu zaidi ilimradi upangiliwe vizuri.
Jaji Warioba alisema baada ya kuona takwimu hiza na kuchanganua sababu zilizotolewa na makundi mbalimbali, Tume iliamua kufanya utafiti kuhusu muundo wa Muungano.
Alisema suala hilo lilijitokeza kwa nguvu na hisia kali mara ya kwanza mwaka 1984 katika kipindi kilichoitwa “kuchafuka kwa hali ya hewa kisiasa Zanzibar”.
Vilevile, alisema mwaka 1991 Tume ya Jaji Francis Nyalali ilipendekeza muundo wa serikali tatu na kwamba, miaka miwili baadaye, yaani mwaka 1993, kikundi cha wabunge wa Tanzania Bara katika Bunge la Jamhuri ya Muungano (G55), kilipendekeza kuwa na muundo wa serikali tatu na Bunge likaridhia.
Alisema pia mwaka 1999 Kamati ya Jaji Kisanga ilipendekeza muundo wa serikali tatu na kwamba Tume pia imepitia taarifa ya kamati nyingi zilizoundwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kama vile, Kamati ya Amina Salum Ali na Kamati ya Shelukindo ya mwaka 1994.
“Sababu zilizotolewa katika matukio hayo ya mwanzo kwa kiwango kikubwa, zinafanana na zile ambazo zimetolewa kipindi hiki. Kila upande wa Muungano una malalamiko mengi kuhusu muundo wa Muungano,” alisema Jaji Warioba.
Alisema kuna malalamiko 10 kwa upande wa Zanzibar na manane kwa upande wa Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kwa upande wa Zanzibar, malalamiko matatu makubwa ni pamoja na kwamba, Serikali ya Tanganyika imevaa koti la Serikali ya Muungano, ambalo linaisaidia Tanganyika zaidi kuliko Zanzibar na kwamba, koti hilo limeifanya Tanganyika kuwa ndiyo Tanzania.
Alisema la pili, mambo ya Muungano yamekuwa yakiongezeka na hivyo kuathiri madaraka ya Zanzibar na kufifisha hadhi ya Zanzibar na kwamba, Zanzibar inaendelea kumezwa.
La tatu, alisema ni kumwondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jaji Warioba alisema kwa upande wa Tanzania Bara, malalamiko makubwa ni kwamba, Zanzibar imekuwa nchi huru, ina bendera yake, ina wimbo wake wa Taifa ina serikiali yake na imebadili katiba yake ili ijitambue kama nchi, wakati Tanzania Bara imepoteza utambulisho wake na kwamba, Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema Tanzania ni nchi moja lakini katiba ya Zanzibar inasema ni mbili.
La pili, Zanzibar imebadili katiba yake na kuchukua madaraka ya Jamhuri ya Muungano, kama vile kuelekeza sheria za Muungano zilizopitishwa na Bunge la Muungano zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi ikimaanisha kwamba, Zanzibar Katiba yake sasa ipo juu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano.
La tatu, wananchi wa Tanzania Bara kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa Zanzibar wana haki hiyo Tanzania Bara.
Jaji Warioba alisema katika kuchambua malalamiko ya Zanzibar kwamba Tanganyika imevaa koti la Muungano, Tume imebaini kwamba muundo wa Muungano wa serikali mbili umeifanya serikali ya Muungano kwa kiwango kikubwa kushughulikia zaidi ya mambo ya Tanzania Bara, hasa mambo ya maendeleo.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, serikali ya Muungano ina mamlaka ya kusimamia mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara.
Kwa msingi huo, alisema serikali ya Muungano inashughulikia sana mambo ya kilimo, elimu, afya, maji, nishati na madini, ujenzi, uchukuzi, maliasili na utalii na mengine ya Tanzania Bara, ambayo siyo ya mambo ya Muungano.
Alisema wakati wa kikao cha Bajeti, Bunge la Muungano hutenga siku mbili au tatu za majadiliano kwa wizara zinazosimamia mambo hayo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara wakati mambo ya Muungano kama ulinzi, mambo ya nje na mambo ya ndani hutengewa siku moja au nusu siku.
Jaji Warioba alisema maswali ya wabunge kuhusu mambo ya maendeleo pia yanahusu Tanzania Bara na ziara za wabunge kukagua miradi ya maendeleo zinahusu Tanzania Bara katika mambo yasiyo ya Muungano.
Alisema mambo hayo bungeni yanasimamiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, ambaye kihalisia hana mamlaka wala madaraka yoyote kuhusu Zanzibar.
Aidha, alisema muundo huo wa Muungano pia umesababisha kuwapo kwa wizara au taasisi zenye sura au zinazotekeleza mambo ya Muungano pekee, mambo ya Tanzania Bara na mambo mchanganyiko.
“Kwa maana ya mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano, hali ambayo inasababisha ugumu wa kutofautisha gharama za Muungano na zisizo za Muungano katika wizara au taasisi hizo. Kundi la pili na la tatu ndilo limekuwa chanzo cha kero za Muungano,” alisema Jaji Warioba.
Kutokana na hali hiyo, alisema hakuna njia ya kubadili hali hiyo kwa sababu serikali ya Muungano haina mamlaka ya kutosha juu ya mambo ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar.
Alisema mawaziri wengi na serikali kwa jumla inalazimika kupanga maendeleo na kutafuta rasilimali kwa ajili ya Tanzania Bara zaidi kuliko kwa Zanzibar.
Jaji Warioba alisema Zanzibar hufanya mipango yake ya maendeleo, lakini ili kupata rasilimali kama mikopo na misaada, ni lazima ipitie serikali ya Muungano, jambo ambalo utekelezaji wake umesababisha matatizo mengi.
Alisema utatuzi wa matatizo hayo umekuwa mgumu, umechukua muda mrefu au umeshindikana na kwamba, njia pekee, ambayo ingefanya maendeleo ya Zanzibar yapewe uzito sawa na mambo ya Tanzania Bara ni kuyaweka mambo hayo chini ya serikali ya Muungano, yaani kuwa na serikali moja.
“Hata hivyo, hilo likifanyika kuna hofu ya Zanzibar kumezwa,” alisema Jaji Warioba.
Alisema Tume pia imefanya uchambuzi wa ndani kuhusu malalamiko ya Zanzibar kwamba kuongezeka kwa mambo ya Muungano kumeathiri madaraka ya Zanzibar.
Jaji Waroba alisema tangu mwanzo wa Muungano, ilikubalika kwamba Zanzibar ibaki na hadhi yake na iwe na madaraka kuhusu mambo yasiyo ya Muungano.
Alisema Tume ilifanya uchambuzi wa mambo ya Muungano ili kubaini kama yanaingilia hadhi na uhuru wa Zanzibar.
Jaji Warioba alisema kati ya mambo 22 ya Muungano, Tume imebaini kuwa siyo mambo yote yanatekelezwa kikamilifu kimuungano na kwamba, mambo mengi yamebadilishwa bila ya kubadili katiba, ama kwa makubaliano kati ya pande zote mbili za Muungano au kwa hatua zilizochukuliwa na upande mmoja.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kodi, bandari, leseni za viwanda, usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, posta na simu, uraia, takwimu, mafuta na gesi na Mahakama ya Rufani.
Alisema kwa hali halisi ilionekana hakuna uwezekano kuyarudisha kwenye orodha ya Muungano mambo ambayo yameondolewa kiutekelezaji.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita, kamati nyingi zimeundwa na kutoa mapendekezo ya kuondoa mambo mengi zaidi kutoka kwenye orodha ya mambo ya Muungano, ikiwa ni pamoja na elimu ya juu, biashara ya nje, uhusiano wa kimataifa, mikopo, misaada ya nje na mafuta na gesi.
Alisema wakati Tume inakusanya maoni, wananchi wengi wa Zanzibar kutoka makundi mawili makubwa; waliotaka Muungano wa serikali mbili na waliotaka Muungano wa mkataba, wote walipendekeza mambo hayo yaondolewe kwenye orodha ya mambo ya Muungano.
“Kwa tathmini ya Tume baadhi ya mambo haya hakuna budi yaondolewa kutoka orodha ya Muungano la sivyo kero za Muungano zitaendelea. Kwa mfano, suala la uhusiano wa kimataifa likiendelea kuwa ni jambo la Muungano Zanzibar haitaweza kujiunga na mashirika kama OIC na Fifa,” alisema Jaji Warioba.
Aliongeza: “Kwa msingi huo, Tume imependekeza kuliondoa suala la uhusiano wa kimataifa katika mambo ya Muungano na kubakisha suala la mambo ya nje.” Alisema eneo lingine ni mgongano kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka masharti kwamba sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano hazitatumika Zanzibar hadi zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi.
Aidha, alisema kodi itakayoamuliwa na Bunge kutozwa na serikali ya Muungano lazima ipate ridhaa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Alisema mambo hayo yameleta mgongano wa katiba na kwamba, juhudi zilizofanywa pande zote mbili hazikufanikiwa kuondoa mgongano huo.
“Zaidi ya hapo, mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanywa mwaka 2010 yametamka wazi kwamba Zanzibar ni nchi kati ya nchi mbili za Muungano wakati Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaelekeza kwamba Tanzania ni nchi moja,” alisema Jaji Warioba.
Alisema mabadiliko katika Katiba ya Zanzibar pia yamehamisha baadhi ya madaraka ya serikali ya Muungano kwenda Zanzibar.
Hata hivyo, alisema wakati muundo wa serikali tatu unaonekana kukidhi matakwa ya Watanzania wengi na pia kushughulikia ipasavyo matatizo mengi au malalamiko au kero za Muungano, Tume imetambua kuwa muundo huo nao una changamoto zake.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment