Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, January 13, 2014

Ni `Golden Jubilee` ya Mapinduzi ya Zanzibar

NA MHARIRI

12th January 2014


Maoni ya Katuni
Leo ni kilele cha maadhimisho ya 'Golden jubilee' ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo yalitokea tarehe kama ya leo, 12 Januari 1964.
Siku hiyo wananchi wa Zanzibar wakiongozwa na hayati mzee Abeid Aman Karume waliamua kwa dhati kuutokomeza utawala wa kikoloni wa Sultani uliokuwa umedumu kwa miaka mingi visiwani humo.
Kilele cha maadhimisho haya kilitanguliwa na mlolongo wa matukio mengi visiwani humo ambapo viongozi mbalimbali walishiriki katika uzinduzi wa miradi ya maendeleo zaidi ya 150 ikiwa ni pamoja na uwekaji wa mawe ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa jamii.
Matukio ya shamrashamra za kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa visiwa vya Unguja na Pemba, yamekuwa yakihusisha ngoma za utamaduni pamoja na magwaride yaliyojulikana kama 'fensi'.
Vyote kwa pamoja vikiashiria kukomaa kwa umoja na mshikamano wa wananchi wa visiwa hivyo, ambavyo kwa pamoja ndivyo vinavyoifanya Zanzibar.
Mitaa pamoja na vitongoji vingi vya Zanzibar vinaonekana kung'ara vikiwa vimepambwa kwa bendera za serikali ya Muungano na ya Zanzibar, pamoja na picha za Marais waliowahi kuiongoza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu Mapinduzi hayo yalipofanyika kwa mafanikio makubwa Januari 12, 1964.
Kimsingi, wananchi wa Zanzibar kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja wamekuwa wakisherehekea matukio mawili muhimu katika ustawi wa Zanzibar, la kwanza la Mapinduzi yenyewe kufikia umri wa miaka 50, na suala la pili ni la maridhiano yaliyofikiwa kati ya vyama vilivyosuguana kwa muda mrefu vya CCM na CUF.
Mahusiano ya kisiasa kati ya vyama hivyo yalianza kuwa mabaya tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1972. Makubaliano yaliyofanyika kwa usimamizi na uongozi wa Rais mstaafu Dk. Aman Abeid Karume akishirikiana na viongozi wa CUF walioongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad yalifanikiwa na kufikia muafaka wa kuunda serikali ya umoja.
Mwishoni mwa wiki hii, katika hali ya kufikia kilele cha maadhimisho hayo, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad alizindua kitabu chenye picha zinazoonesha safari ndefu ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo wasanii, wasomi, pamoja na wawakilishi wa mabalozi walioko nchini walialikwa kushuhudia uzinduzi huo wa kihistoria ulioshuhudiwa pia na Rais mstaafu Dk. Aman Abeid Karume.
Wakati wananchi wa Zanzibar pamoja na Watanzania wote wakisherehekea kwa nderemo na vifijo 'Golden Jubilee' ya Mapinduzi ya Zanzibar, suala la hatima ya Katiba Mpya inasubiriwa kwa hamu na wananchi wengi. 
Kinachosubiriwa zaidi ni kujua muundo wa Muungano utakavyoamriwa, maamuzi ambayo yatajulikana baada ya kupigwa kura za maoni.
Rais Kikwete, katika hotuba yake ya kukaribisha mwaka mpya kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, alisema kufikia mwezi Mei mwaka huu, maamuzi ya mwisho ya Rasimu ya Katiba Mpya yatakuwa yamefikiwa na kwamba itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kura za maoni.
Rais Kikwete aliwaambia mabalozi hao kuwa kama ratiba ya mchakato wa kupata Katiba Mpya itakwenda kama ilivyopangwa, inawezekana Katiba hiyo ikapatikana ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, na kuongeza kuwa Watanzania wanaendelea kufurahia amani na uhusiano mzuri na majirani ingawa alisema kuna changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Ni wajibu wetu kwa pamoja kuunga mkono jitihada za serikali ya Zanzibar katika kutafsiri mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 ya tangu Mapinduzi yafanyike visiwani humo. 
Mafanikio ya wananchi wa Zanzibar ni mafanikio ya Watanzania wote, kwani sisi tu wamoja tunaoamini kuwa umoja, mshikamano, amani pamoja na upendo ni nguzo kuu za kuendeleza Muungano ulioasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Aman Abeid Karume.
Tunaweza kutofautiana kwa itikadi zetu, lakini tukawa na malengo ya kufikia katika matumaini ya aina moja, hata kama Katiba Mpya itafanya mabadiliko katika vipengele vya masuala ya Muungano, bado Watanzania tutabaki kuwa wamoja na kuendeleza upendo, mshikamano, amani na umoja. 
Tunaipongeza serikali ya Zanzibar kwa maadhimisho hayo na kuwaombea waendeleze mshikaano uliopo ili wafikie miaka mingine 50 wakiwa wamoja na wenye upendo na amani. 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment