NA MWANDISHI WETU
14th January 2014.
Mjumbe huyo Maalum ambaye ni Waziri wa Makazi na Maendeleo wa Miji na Vijiji, Jiang Weixin alifika Zanzibar kumwakilisha Rais Xi Jinping katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya visiwa hivyo.
Katika mazungumzo yao ambayo yalihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, Dk. Shein alisema kitendo cha Rais Xi Jinping kumtuma mjumbe wake maalum kushiriki katika maadhimisho hayo ni uthibitisho wa urafiki wa kweli uliodumu kwa miongo mingi kati ya serikali na wananchi wa nchi hizo mbili.
Alimueleza mjumbe huyo kuwa, wananchi wa Zanzibar wamefarijika kupokea salamu za kuwatakia heri katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi kutoka kwa Rais wa China , Xi Jinping.
Dk. Shein alirejea usemi wa Rais Xi Jinping kuwa, urafiki wa wananchi wa Zanzibar na wenzao wa China si wa msimu bali wa wakati wote na kwamba historia imedhihirisha hivyo katika miaka 50 ya mapinduzi.
Alisema kitendo cha Jamhuri ya Watu wa China kuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar kitabaki katika kumbukumbu za historia ya ukombozi wa watu wa Zanzibar.
Alisema miaka 50 iliyopita wananchi wa Zanzibar walipokataa kutawaliwa na kuamua kujitawala wenyewe hivyo walihitaji kuungwa mkono na wananchi wenzao kote ulimwenguni na ndipo China bila ya ajizi ikayatambua mapinduzi mara moja.
Mbali na kuyatambua Mapinduzi Dk. Shein alieleza kuwa katika miaka 50 ya mapinduzi, China imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na watu wa Zanzibar katika harakati zao za kujiletea maendeleo.Alitolea mfano kuwa nchi hiyo ilisaidia katika uanzishaji wa viwanda mbalimbali, misaada katika kuendeleza kilimo cha kisasa, michezo, sekta ya habari pamoja na uimarishaji wa sekta ya afya ambayo ilikuwa nyuma sana.
Kwa upande wake, Jiang alieleza kuwa ni heshima kubwa kwake kuwasilisha salamu za pongezi na za kirafiki kutoka kwa Rais Xi Jinping na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na wananchi wa Zanzibar wakati huu wa kuadhimisha miaka 50 ya mapinduzi.
Alisema serikali na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China wanajivunia na kuthamini uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa umejengwa katika msingi ya usawa na heshma kati ya serikali na wananchi wa nchi hizo.
Alisema miaka 50 ya wananchi wa Zanzibar kujitawala kutoka kwenye makucha ya wakoloni imeshuhudia maendeleo makubwa katika kila sekta na kwamba nchi yake ina matumaini makubwa k kwa hatua hiyo iliyofikia ina nafasi nzuri zaidi ya kupiga hatua kubwa kwa haraka zaidi hivyo kuimarisha ustawi wa wananchi wake.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment