Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amewasili nchini Uturuki akiongoza ujumbe wa Zanzibar katika mkutano wa Kimataifa wa Uchumi ulioanza leo jijini Istanbul.
Katika mkutano huo uliolenga kuweka mikakati ya matumizi bora ya rasilimali kwa maendeleo ya kiuchumi, zaidi ya wajumbe 500 kutoka mataifa tafauti, wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara, wataalamu wa uchumi na fedha na wawakilishi wa sekta binafsi wanahudhuria.
Akizungumza katika kikao cha utangulizi kabla ya kufunguliwa rasmi mkutano huo, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kimataifa na Serikali wa Mkutano wa Kiuchumi wa Dunia (WEC), Carl Bjorkman ameyahimiza mataifa kutoa kipaumbele katika kuimaarisha miundo mbinu ya kiuchumi kama njia muhimu ya kuwapatia fursa za kimaendeleo wananchi wao.
Mkurugenzi huyo amesema mataifa mengi bado hayaoneshi mafanikio makubwa katika ukuaji wa uchumi, huku sekta nyingi zinazogusa maendeleo ya watu wao zikiyumba, hali ambayo inapaswa kudhibitiwa kwa mataifa kuwa na mikakati ya pamoja ya kukuza maendeleo ya kiuchumi.
Amesema miongoni mwa matatizo makubwa kwa nchi nyingi ni kukosekana fursa za kiuchumi zinazoweza kuzaa ajira nyingi kwa wananchi, hali inayochangia kukosekana imani ya wananchi na baadaye kuathiri utulivu na amani ambao ni msingi wa ukuaji wa uchumi na maendeleo.
“Tukiungana mataifa ya Ulaya, Asia, America na Afrika tukiweza kuzitumia rasilimali tulizonazo katika maeneo yetu kwa kuzingatia vipaumbele vya ukuaji wa uchumi, tutaweza kuleta mabadiliko na kuunda fursa nyingi kwa wananchi katika Mabara yote”, amesema Bjorkman.
Mkurugenzi huyo amehimiza utaratibu wa mataifa kuchagua maeneo machache yenye ufanisi kushirikiana kwa mujibu wa mazingira yao, ambapo mataifa yataweza kushirikiana katika kuyaendeleza, badala ya kuweka vipaumbele vingi kwa wakati mmoja, hali ambayo haileti mafanikio makubwa katika utekelezaji wake.
Ujumbe wa Zanzibar pia unawashirikisha Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, Katibu wa Tume ya Mipango, Amina Khamis Shaaban na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitegauchumi (ZIPA) Nd. Salum Nassor.
No comments :
Post a Comment