Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, September 10, 2014

Othman Masoud: Jemedari wa Kupigania Haki

Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Othman Masoud Othman,



Na Ahmed Rajab.
MSIMAMO wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othman Masoud Othman, ni msimamo wa kizalendo, wa kupigiwa mfano na unaofaa kuigwa na wakuu wengine wa Serikali wenye hisia na nchi yao.
Ni nadra siku hizi, hasa nchini mwetu, kuwaona au kuwasikia viongozi wenye vyeo vikubwa kama hicho cha Mwanasheria Mkuu wakijitokeza wazi, tena bila ya woga, kuitetea misimamo inayopingana na ile ya wakubwa wa nchi. Hivyo, Mheshimiwa huyu yuko katika tabaka la wale waliojitolea kuipigania nchi yao.
Huo ndio uzalendo. Tena ni uzalendo wa hali ya juu. Si tu kuwa mtu ana mapenzi na nchi yake lakini pia kuwa ana moyo wa kujitolea kuipigania nchi yake na kuwa tayari kuziondoa, kuziweka upande au kuzipuuza tafauti zozote zilizopo — ziwe za kidini, za kikabila za kichama au za kiitikadi za kisiasa — baina yake na wananchi wenzake. Daima anakuwa anaiweka mbele nchi yake, naliwe liwalo.
Othman Masoud ameudhihirishia ulimwengu na muhimu zaidi amewadhihirishia Wazanzibari wenzake kwamba yeye ni mzalendo wa aina hiyo. Tena ni mtu mwenye kujiamini.
Nafikiri sababu inayomfanya ajiamini ni kuwa anaamini kwa dhati kwamba anaitetea haki. Hataki kuona dhulma inatendeka baina ya nchi mbili zilizo katika Muungano. Hataki kuiona nchi moja inaidhalilisha nyingine.
Huko kujiamini kwake ndiko kunakomfanya asiwe na hata chembe ya woga kwa kuwakwaa wakubwa wenye sera zinazopingana na msimamo wake. Wale wenye kumbeza na waliojitokeza kimbele mbele kumshauri Rais Ali Mohamed Shein amfukuze kazi wamekosea.

Kwa kuuchukua msimamo aliouchukua Othman Masoud ameonyesha kuwa hana ubinafsi. Hayuko tayari kuiuza nchi yake kwa vijipesa viwili vitatu au kwa ulwa wa aina yoyote ile.
Alipokuwa analihutubia kongamano la Baraza la Katiba la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Zanzibar, Othman hakutafuna maneno, hakujifanya kibogoyo alipoutamka ukweli na wala hakubabaika kwa namna yoyote ile. Sauti yake ilijaa hamasa ya uzalendo wake; aliyaeleza mambo kwa busara na hikma, tena kwa taratibu.
Kwa ufupi aliililia na kuipigania nchi yake. Hamna shaka yoyote kwamba yeye ni jemedari mzuri wa kuipigania ardhi iliyozikiwa kitovu chake. Inafaa tumshukuru Mungu kwani kila uchao anachomoza jemedari mwingine wa kuipigania Zanzibar yetu. Kila mmojawao akili kichwani. Vipi tushindwe kwenye vita hivi?
Othman Masoud anautetea muundo wa Muungano utaokuwa na Serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Katiba iliyo chini ya Jaji (Mstaafu) Joseph Warioba.
Pamoja na kuubainisha msimamo wake kuhusu suala la Muungano Mwanasheria huyo Mkuu zaidi aliutumia wadhifa wake na uweledi wake wa mas’ala ya kisheria kutuelimisha Wazanzibari wenzake kuhusu mambo ya Katiba na jinsi Zanzibar inavyopunjwa ikiwa ndani ya Muungano wa serikali mbili kama ulivyo sasa chini ya ule aliouelezea kuwa “ukoloni kasorobo”.
Alieleza pia kwamba muundo uliopo wa Muungano ndio wenye hatari ya kuuvunja Muungano kinyume na wanavyofikiria wahafidhina wa CCM/Zanzibar na wale walio Bara wanaotishwa na wahafidhina hao.
Ninaamini kabisa kwamba itikadi halisi ya wahafidhina hao ni kuendelea kuwa na madaraka ili wayatumie madaraka yao kujichumia mali. Huo ndio mkakati wao na hiyo ndiyo hali halisi ilivyo.

Aghalabu watu wenye kuipenda nchi yao na walio tayari kujitolea mhanga kwa sababu ya nchi yao huwa hawawajali hao wahafidhina. Huwa hawawatii maanani. Wanafanya hivyo kwa sababu katika nyakati kama hizi za uwazi na demokrasia watu wa sampuli ya wahafidhina wetu wenye kuonya kuhusu ‘maafa’ mara nyingi, kama si zote, huwa ndio wasioisoma vizuri historia. Matokeo yake ni kwamba huishia kutupwa katika debe la taka la historia.
Kwa upande mwingine, watu wa sampuli ya Masoud Othman, hata kama awali watakumbwa na misukosuko, misukosuo hiyo huwa ya mpito tu kwani huishia kubebwa na umma na kushangiriwa kwa ushindi wao kwa sababu daima wanakuwa wanapigania haki.


No comments :

Post a Comment