Kwa ufupi
Hata hivyo, Hamad Rashid ambaye alifukuzwa uanachama
wa CUF na kupinga hatua hiyo mahakamani hakusema atawania kiti hicho
kupitia chama kipi.
Dodoma/Dar/Mwanza. Mwenyekiti
wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta jana alitoa dakika tano kwa
Mjumbe wa Bunge hilo, Hamad Rashid Mohamed ‘kujibu mapigo’ dhidi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Maalim
Seif Sharif Hamad.
Sitta alitoa fursa hiyo baada ya wenyeviti wa kamati kadhaa kumaliza kuwasilisha ripoti za vikao vyake.
“Tumefikia mwisho wa uwasilishaji wa ripoti za
kamati lakini Hamad Rashid ana kitu cha kusema, karibu,” alisema Spika
Sitta akimkaribisha na kuongeza kwamba
anatumia Kanuni ya 27(1) (e) ya Bunge hilo ambayo
inampa mamlaka kuingiza shughuli yoyote anayoiona inafaa kushughulikiwa
kwa wakati huo.
“Nimepata malalamiko kutoka kwa Hamad Rashid
Mohamed kwamba hakutendewa haki katika moja ya vipindi vya TV.
Nampa dakika zisizozidi 10,” alisema Sitta kabla ya kuahirisha Bunge hadi leo.
Nampa dakika zisizozidi 10,” alisema Sitta kabla ya kuahirisha Bunge hadi leo.
Hata hivyo, kitendo hicho kimekosolewa na
mwanazuoni wa sheria na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, James
Jesse, akisema: “Hatua hiyo si sahihi lazima ikemewe kwa kuwa hapa
nchini hatuna sheria inayotoa haki ya kujibu mapigo bungeni kama ilivyo
kwa nchi za wenzetu ambao mtu akishambuliwa bungeni anapata nafasi ya
kujibu na majibu yake yanaingia kwenye hansard (kumbukumbu rasmi za
Bunge).”
Alisema pamoja na kwamba kanuni inasema inatoa mamlaka hayo kwa mwenyekiti, kitu chochote lazima kiwe na mipaka.
“Kwa kuwa kitu kinachojadiliwa pale ni Katiba na
si kitu kingine, hiyo nafasi ya kuzungumzia mambo mengine haikuwapo.
Siungi mkono na suala kama hilo lazima likemewe.
Alichosema Hamad Rashid
Mbunge huyo wa Wawi (CUF), alisema katika
mahojiano yaliyorushwa na Kituo cha Televisheni cha Star TV juzi kuwa
Maalim Seif alimshambulia yeye binafsi, kamati yake na Bunge la Katiba.
“Amesema mimi ni dalali wa CCM na kwamba nimepewa
fedha ili kuwahonga watu ili waje kwenye kikao hiki (Bunge). Hili
nimemwachia mwanasheria wangu,” Mohamed alimnukuu Maalim Seif na
kuongeza:
“Nimemkabidhi (mwanasheria) CD. Nimemwambia naomba uipitie ili
twende mahakamani. Nimemwambia wakili wangu kwa hili alilosema
akathibitishe mahakamani kama mimi ni dalali.”
Katika mazungumzo hayo Hamad Rashid alitumia
dakika tano kuzungumzia masuala ya kamati yake na nyingine tano
kumzungumzia Maalim Seif, alisema Makamu huyo wa Rais wa SMZ
anamshambulia kwa vile amesikia kuwa anataka kugombea urais... “Sasa
natangaza rasmi kuwania urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.”
Hata hivyo, Hamad Rashid ambaye alifukuzwa
uanachama wa CUF na kupinga hatua hiyo mahakamani hakusema atawania kiti
hicho kupitia chama kipi.
Alisema si mara ya kwanza kwa Maalim Seif kutoa
tuhuma nzito zisizo na ushahidi kama ilivyotokea mwaka 1995 alipodai
kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Salmin Amour anapanga kumuua (maalim).
Alisema yeye ni mtu mwaminifu na hajawahi kupata
kashfa yoyote hapa nchini hata alipokuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi na Naibu Waziri wa Fedha wa SMZ.
“Mtu mzima unaposema maneno ambayo huwezi
kuyapanga vizuri kwa sababu tu Hamad katangaza kugombea urais hilo ni
tatizo,” alisema na kuongeza:
“Nilitaka kugombea ukatibu mkuu ukanitimua, sasa
huna nafasi ya kunitimua kwenye urais. Nakwenda kugombea urais. Nilikuwa
sijasema nakwenda kugombea wapi, nakwenda kugombea Zanzibar,” alisema.
Mjumbe huyo ambaye hakuungana na wapinzani wenzake
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia Bunge hilo,
alimtaka Maalim Seif asiingiwe na kiwewe kwa yeye kutangaza kugombea
urais wa Zanzibar mwaka 2015.
Pia alikanusha madai kwamba yuko bungeni kwa
sababu ana uchu wa madaraka na kuwa Maalim Seif ndiye mwenye uchu huo
kwa kugombea urais mara nne.
“Mimi sijagombea mara nne urais wala sijawahi
kutoka makamu mwenyekiti (wa CUF) nikarudi kuwa katibu mkuu wa chama,
halafu nikarudi tena umakamu na nikarudi tena kwenye ukatibu mkuu,”
alisema na kuongeza: “Sijawahi kuwa kama Putin (Vladmir - Rais wa Urusi)
hata siku moja. Ningeomba sana wananchi wa Tanzania wajue kuwa viongozi
ni kama popo. Hajulikani ni mnyama au ni ndege. Putin aliachia madaraka
ya urais na kuwa waziri mkuu kabla ya kurejea tena kwenye nafasi hiyo.
“Huku mtu anakwambia nautaka muungano huku anataka
Serikali ya Mkataba. Serikali ya mkataba ni lazima uvunje muungano.
Huwezi kuwa kiongozi unayejifanya unapenda watu wakati wewe ndiye
unayeleta chuki na fitina. Haiwezekani kiongozi anayejua mahitaji ya
nchi na vipaumbele vyake apinge mchakato wa kuipata Katiba Mpya kama
anavyofanya Seif. Kama lengo lake ni kuvunja Muungano ni vyema akaweka
wazi.”
Mjumbe huyo pia alikanusha madai ya Maalim Seif
kuwa kuwapo kwake ndani ya Bunge hilo ni kunatokana na kubebwa na Spika
wa Bunge (la Muungano), Anne Makinda kwa vile kesi aliyoifungua
ilishakwisha.
“Naomba nitoe taarifa rasmi kwako kwamba shauri nililolifungua
mahakamani bado linaendelea na kesi ipo tarehe 26/9/2014 na siyo kwa
kuhukumiwa, bali kwa kuendelea kusikilizwa,” alisema.
Alisema mara zote Spika amekuwa makini katika
jambo hilo akisema hana mamlaka ya kuingilia Mahakama ambayo ndiyo
iliyoizuia CUF kumfukuza uanachama ambao pia ungemvua ubunge.
“Kwa hiyo kumpandikizia Spika kwa lawama kama hii haistahiki hata kidogo na ni vizuri akamuomba radhi,” alisema.
Maalim Seif amshukia Sitta
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika
Viwanja vya Furahisha, Mwanza jana jioni, Maalim Seif alimlaumu Sitta
kuwa anachangia kuvuruga Bunge la Katiba kwa kupindisha kanuni za Bunge
hilo.
Bila kugusia mambo yaliyozungumzwa juu yake
bungeni, Maalim Seif alisema Katiba Mpya haiwezi kupatikana na kuwa hata
kama CCM italazimisha kuipitisha bungeni, hatalala usiku na mchana
kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanaikataa.
No comments :
Post a Comment