Rais Kikwete
Hatua ya Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya siasa
vilivyo wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na kukubaliana
kuhusu mambo matano ya msingi yanayohusu mustakabali wa nchi yetu, ni ya
kijasiri na ya kupongezwa.
Moja ya mambo waliyokubaliana ni kuahirishwa kwa Bunge la Katiba ifikapo
Oktoba 4, mwaka huu kama Tangazo la Serikali Namba 254 linavyotaka.
Itakumbukwa kwamba Agosti 5, mwaka huu Bunge hilo lilitoa azimio ambalo
lilirekebisha Kanuni ya 14(4) na kuzifanya Jumamosi, Jumapili na siku za
sikukuu kuwa siku zake za mapumziko.
Hatua hiyo ya Bunge hilo ilipingwa na wananchi kila kona ya nchi, kwani
ilimaanisha kwamba lingeendelea na shughuli zake hadi Oktoba 31. Wengi
walishangazwa na hatua ya wajumbe wa Bunge hilo kujiongezea muda, huku
wakijua kuwapo kwa tangazo hilo la Serikali.Hasira za wananchi zilitokana na Bunge hilo kuonekana halina uhalali wa
kisiasa na pia kutumia fedha nyingi za walipakodi kulipana posho pasipo
kuzingatia ukweli kuwa, Katiba mpya isingepatikana kutokana na wajumbe
hao waliokuwa wameunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia
shughuli za Bunge hilo.
Tambo za uongozi wa Bunge hilo na wajumbe kutoka chama tawala ambao hasa
ndiyo waliosababisha Bunge hilo kupasuka vipandevipande, zilikuwa
kwamba Bunge lingeendelea na hatimaye Katiba mpya ipatikane pasipo
wajumbe wa Ukawa kushiriki.
Pia walisema wajumbe wa Ukawa wasijidanganye kwamba Rais Kikwete
atakutana nao tena kusikiliza malalamiko yao kama alivyofanya huko nyuma
wakati mchakato wa Katiba mpya ulipoanza.
Ndiyo maana tunasema hatua ya Rais Kikwete kukutana na viongozi wa TCD
na kushirikiana nao kufanya uamuzi mgumu ni wa kijasiri na wa kupongeza.
Tangu wajumbe wa Ukawa wasusie shughuli za Bunge hilo Aprili 16,
wamekuwa wakimsihi Rais Kikwete kukutana nao ili kupata suluhu ya
malalamiko yao.
Wananchi wengi, wakiwamo viongozi wa kidini wamekuwa wakisisitiza kwamba
Katiba itakayopatikana pasipo maridhiano na mwafaka wa kitaifa,
haitakubalika.
Kwa maoni yao, Bunge hilo limepoteza muda mrefu pasipo kufanya jambo
lolote la maana, kwani kususiwa na wajumbe wa Ukawa kulitokana na
kutawaliwa na mijadala ya kupandikiza chuki na mifarakano yenye kuwagawa
wajumbe katika makundi yanayokinzana kisiasa na kiitikadi.
Kama tulivyosema hapo juu, mazungumzo kati ya Rais Kikwete na viongozi hao wa TCD yamezaa uamuzi mgumu.
Pamoja na kuamua kuahirisha Bunge hilo ifikapo Oktoba 4, uamuzi mwingine
ni: Uchaguzi Mkuu ufanyike mwakani kwa kutumia Katiba ya sasa ya mwaka
1977; kuahirishwa kwa kura ya maoni hadi baada ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba
2015; na kuahirishwa kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hadi mapema
mwakani.
Uamuzi mwingine ni kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, mshindi wa Uchaguzi
Mkuu awe na zaidi ya asilimia 50 ya kura, kuwapo mgombea binafsi na
matokeo ya urais pia kupingwa mahakamani.
Tunampongeza Rais Kikwete kwa hatua hiyo itakayoleta maridhiano na
kuepusha nchi yetu na vurugu. Hatua hiyo bila shaka itakuwa imewaudhi
wengi ndani ya chama chake, lakini ni kwa masilahi mapana ya Taifa letu.
Matarajio yetu ni kwamba wananchi wote watamuunga mkono, kwani hatua yake hiyo siyo uthibitisho wa udhaifu, bali ujasiri wake.
No comments :
Post a Comment