Toleo
la 370
10
Sep 2014
“KAMA
kuna nchi ambayo ingekuwa na visingizio vya kuwa nyuma kimaendeleo kuliko nchi
yeyote ya Afrika ni Vietnam. Iliharibiwa na vita nyingi dhidi ya China, Japan,
Ufaransa na Marekani, iligawanywa na ukoloni na kuwekewa mifumo ya utawala ya
kigeni na ilifuata siasa ya ujamaa kikweli kweli.
“Hii
ingekuwa nchi masikini zaidi duniani. Hata hivyo, ikiwa imeanza bila kitu
chochote, imeweza kuzishinda nchi nyingi za Kiafrika kwa kipato cha mtu kwa
mwaka. Mabadiliko makubwa yalitokea pale viongozi wake walipoamua kuachana na
sera kandamizi na kuanza kukuza uchumi wao kwa kasi.
“Matokeo yake imebakia katika njia ya
kukuza uchumi na maendeleo kuliko Afrika” Haya ni maneno wa mwandishi Greg
Mills na Mwenzake Jeffrey Herst katika kitabu chao ‘Africa’s Third
Liberation: the new search for prosperity and jobs.
Nimechagua
kipande hiki kuelezea namna ambavyo nchi iliyokuwa fukara wa kutupwa na yenye
sifa kama zetu imeweza kujikwamua, kutokomeza umasikini na kuendelea kwa kasi.
Sikubaliani kiitikadi na Mills kwani
yeye anaamini kabisa kuwa ni mfumo wa soko tu ndio suluhisho la matatizo ya
Afrika wakati mimi ninaamini kuwa dola inapaswa kuchukua nafasi yake katika
kuzuia makosa ya soko (market failures).
Hata
hivyo, Vietnam na Tanzania zina mambo mengi yanayofanana na hivyo ni vema
kuangalia wenzetu waliwezaje katika kutafuta kujikwamua na uduni wa maendeleo
ya watu wetu.
Kama
ilivyokuwa Tanzania, Vietnam ilifuata mfumo wa uchumi unaendeshwa na dola kwa
kila kitu. Dola ilijenga viwanda na kuviendesha kama ilivyokuwa Tanzania.
Serikali ya Vietnam ilijenga viwanda vya
nguo kama nguzo kuu ya kukuza ajira kwa watu wake. Kiwanda maarufu cha nguo
nchini humo ni The Number Three Factory of May 10. Kiwanda hiki
kiliajiri watu 3000. Tanzania nayo ilikuwa na viwanda maarufu kama Urafiki
kilichoajiri watu 1500.
Baba
yangu, Mzee Kabwe Zuberi Kabwe, alikuwa ni miongoni mwa vijana wa mwanzo kabisa
kuajiriwa katika kiwanda hiki, walichukuliwa kutoka kila kona ya nchi kuendesha
mashine na kuzalisha kanga, mashuka na kila aina ya vitambaa vya nguo.
Leo
Kiwanda hiki cha Hanoi kinaendelea kufanya kazi, hiki cha Urafiki sina uhakika.
Mara ya mwisho nimemsikia Mbunge wa Ubungo akitaka Kamati Teule ya Bunge kuhusu
utendaji wa kiwanda hiki. Tanzania ilikuwa na viwanda vya nguo 12 nchi nzima.
Kama
nilivyopata kuandika katika siku za nyuma, viwanda hivi vilijengwa kimkakati
ili kuhakikisha kwanza pamba inayozalishwa Tanzania inaongezewa thamani nchini
na pili kuzalisha ajira kwa wananchi, kuongeza kipato na kutokomeza umasikini.
Kama Tanzania, Vietnam walifuata sera za
kurekebisha uchumi wao ikiwemo kubinafsisha baadhi ya viwanda vyao ili kukuza
ufanisi. Kiwanda cha The Number Three Factory of May 10 kilibinafsishwa
mwaka 2001 kwa kuuza sehemu ya hisa zake kwa watu binafsi.
Kutokana
na uwekezaji uliofanyika, hivi sasa kiwanda hicho kimeajiri watu 8000 na
kinauza Ulaya mashati, suruali na fulana zenye thamani ya Dola za Marekani
milioni 40 kwa mwaka. Ukuaji huu upo pia katika sekta nzima ya nguo.
Hivi
sasa Vietnam ina makampuni 3700 ya nguo yenye kuajiri watu milioni mbili na
nusu. Mauzo ya nguo kutoka Vietnam hivi sasa yana thamani ya Dola za Marekani
11.2 bilioni kwa takwimu za mwaka 2010.
Tanzania
hivi sasa inauza pamba takribani yote inayozalishwa nchini kama ghafi na
takribani viwanda vyote vya nguo vilivyobinafsishwa havifanyi kazi na vingine
vimegeuzwa maghala.
Maendeleo hayo katika sekta ndogo ya
nguo yaliendana kabisa na maendeleo katika sekta ya Kilimo. Mwaka 1990, Vietnam
ilikuwa inaagiza mchele kutoka nje (net importer) lakini mwaka 2005 nchi
hiyo ilikuwa ya pili duniani kwa kuuza mchele nje ya nchi.
Asilimia
31 ya mchele unaouzwa na Vietnam hununuliwa na nchi za Afrika, zenye ardhi
kubwa zaidi na rutuba kuliko Vietnam. Uzalishaji wa kahawa pia uliongezeka na
kuifanya nchi hiyo kuwa ya pili duniani baada ya Brazil kwa kuuza kahawa katika
soko la dunia ambapo waliuza tani 900,000 za kahawa mwaka 2012.
Mwaka
huo, Tanzania iliuza tani 71,000 tu za kahawa. Kwa upande wa korosho, Vietnam
sio tu imeweza kuongeza uzalishaji lakini imeachana na kuuza korosho ghafi na
pia hivi sasa ina teknolojia yake ya mashine za kubangua korosho na kuiuza nje.
Mwaka
2012 nilipotembelea viwanda vya korosho vilivyobinafsishwa, niliona mashine
hizi kutoka Vietnam katika kiwanda cha Mtwara Mjini kinachoendeshwa na kampuni
ya Olam kutoka Singapore.
Mifano
hii ya nchi ya Vietnam inatuambia jambo moja kubwa kuwa inawezekana kabisa
kuleta maendeleo ya watu na nchi kwa haraka. Kinachotakiwa ni sera makini,
dhamira na uwezo wa kutekeleza sera bila kutetereka.
Vietnam
walifanya ubinafsishaji kama Tanzania, lakini wao walihakikisha kuwa mali za
taifa zilizojengwa na watu wote katika Taifa hazipotei. Walihitaji teknolojia
mpya na mitaji ilhali wakiendelea kushikilia sehemu kubwa ya viwanda ili
kuhakikisha havigeuzwi maghala.
Pia walitofautisha ‘privatisation’ na ‘liberalisation’ ambapo
kulegeza masharti ya biashara haikumaanisha kuuza kila kitu. Bali walikaribisha
mitaji binafsi kushindana na mitaji ya umma na hivyo kukuza uzalishaji.
Vietnam
iligawa mashamba ya umma kwa raia wake mmoja mmoja na kuwawezesha kuzalisha kwa
viwango na tija. Miradi mikubwa ya uzalishaji mchele iliyokuwa ya umma
haikuuzwa kwa makabaila bali iligawiwa vipande vya ekari kumi kumi na kugawa
kwa wananchi ili wazalishe.
Hapa
Tanzania mashamba mengi ya Ushirika yaliachwa tu na kutelekezwa na mengine
kuuzwa kwa ‘wawekezaji’. Mwaka 2009 nilikwenda wilayani Mbarali nikiwa
Mwenyekiti wa Kamati ya POAC kukagua zoezi la ubinafsishaji ambapo nilikuta
Serikali imeuza shamba la Kapunga na kijiji kizima cha Kapunga. Mgogoro wa
Kapunga bado unaendelea mpaka sasa na uzalishaji wa mwekezaji umesimama.
Vietnam
ilijifunza kutokana na makosa ya sera yao ya ukomunisti na kuamua kufanya
mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Dhamira kubwa ilikuwa ni kuona watu wa Vietnam
wanaondokana na Ufukara na sio kuondoa ufukara wa wachache wenye maslahi na mfumo
wa dola.
Mabadiliko
ya kiuchumi yaliyofanyika Tanzania yameshindwa kwa sababu moja kubwa kwamba
waliokuwa wanatekeleza mipango hiyo walijitazama wao badala ya kutazama Taifa.
Ndio Maana viwanda vingi vilivyouzwa kwa ‘wazalendo’ havifanyi kazi kwa sababu
‘wazalendo’ hawa walikuwa ni watu wenye maslahi na sio watu wenye dhamira ya
kuendeleza.
Hebu
tukaeni na kujitafakari upya. Vietnam wamewezaje na sisi tushindwe?
+255-756809535
http://www.zittokabwe.comZitto Kabwe ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Naibu Kiongozi wa kambi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali.
See more at: http://www.raiamwema.co.tz/vietnam-wamewezaje#sthash.lRS9ZYEl.dpuf
No comments :
Post a Comment