dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, September 8, 2014

ZEC yakamilisha awamu ya kwanza uchunguzi wa majimbo

Na Khamis Mohammed
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imekamilisha awamu ya kwanza ya kazi ya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya  majimbo ya uchaguzi Zanzibar baada ya kupokea maoni mbali mbali ya wadau Unguja na Pemba.

Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alipokuwa akizungumza na waandishi habari ofisi za ZEC, Maisara mjini Unguja jana ambapo alisema, kinachofanyika hivi sasa ni kuyachambua maoni yaliotolewa katika mchakato huo uliochukuwa karibu miezi mitatu.

Alisema katika utaratibu huo wa kupokea maoni ya wadau juu ya idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi, ZEC ilikutana  ana kwa ana na kupokea maoni ya vyama vya siasa 14 vikiwemo vya CCM na CUF huku vyama vyengine vinane viliwakilisha  maoni yao kwa maandishi.
Alizitaja taasisi nyengine  zilizotoa maoni ni pamoja na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wawakilishi wa Asasi mbali za kijamii pamoja na wananchi.

Alisema maoni makuu yaliosikilizwa na kupokelewa na tume ni pamoja na matatizo ya mipaka ya majimbo katika wilaya, wadi za uchaguzi na mipaka ya shehia, matatizo ya majimbo  yatokanayo na mgawanyo wa hali ya jiografia, ongezeko la idadi ya watu katika majimbo ya wilaya na maoni ya jumla ya wadau.


"Yapo baadhi ya majimbo yenye idadi kubwa ya watu na mengine yakiwa na idadi chache na kukosekana kwa uwiano katika mgawanyo wa majimbo uliopo hivi sasa," alisema.

"Watu wanazaliana, mamlaka zinapeleka  huduma, lakini ni vyema kukawepo uwiano wa kuwahudumia," alisema.

"Katiba haijasema  kuwa lazima jimbo lizingatie  idadi ya watu, lakini inataka  kuangaliwa uwiano na ZEC itazingatia hilo," alisema.

Alisema  ZEC haijakaa kwa lengo  la ukataji au upunguzaji wa majimbo ya uchaguzi na kwamba kinachofanyika ni uvumi unaoenezwa na watu wachache kwa maslahi binafsi.

"Ni uvumi na hofu za wanasiasa, ZEC haijafanya uamuzi huo kwa sasa,"alisema.

Naye Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali, alisema, kazi hiyo inaendeshwa kwa matakwa ya  katiba ambayo inaelekeza kufanyika kila baada ya miaka minane hadi 10 ambapo mara ya mwisho  ilifanyika mwaka 2005 ikiwa sasa ni miaka tisa tokea Tume ya Uchaguzi  ya Zanzibar ilipofanya uchunguzi wa idadi, mipaka na majina ya majimbo ya uchaguzi.

Alisema, kulikuwepo na changamoto mbali mbali juu ya zoezi hilo la ukusanyaji wa maoni ikiwemo baadhi ya maeneo watu kuonekana kuwa na jazba za kisiasa.

"Watu walikuja  kama vile ilivyokuwa wakati wa ukusanyaji wa maoni ya katiba mpya ya Tanzania, lakini, mishowe walituelewa na kufanikisha kazi yetu.
Juu ya mchakato huo kuhodhiwa na wanasiasa, alisema,ZEC imejidhatiti kufanikisha mchakato huo kwa kuzingatia matakwa ya katiba na kwamba haitokuwa na nafasi ya kwenda kinyume na matakwa hayo kwa maslahi ya taifa na wananchi wake kwa ujumla.

"Mtaji wa wanasiasa ni wapiga kura, huo ndio uhalisia, lakini si katika hili," alisema.

Mkurugenzi huyo alikiri kuwepo kwa baadhi ya majimbo yenye idadi kubwa ya watu likiwemo jimbo la Fuoni lenye watu zaidi ya 60,000, Dimani watu 58,000 na Dole lenye idadi ya watu karibu 35,000.


"Haya ni baadhi ya majimbo yenye idadi kubwa ya watu, lakini, yapo yenye idadi chache likiwemo jimbo la Rahaleo, Chambani na Mgogoni," alisema. 

No comments :

Post a Comment