1. Historia
ya Mradi
Mheshimiwa Spika, Katika miaka ya tisini (1990s), Tanzania ilikuwa
ikikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme, hali
iliyopelekea kuwepo kwa upungufu wa umeme na kuathiri shughuli za maendeleo ya
kiuchumi na kijamii nchini. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ilichukua
hatua za dharura za kuanzisha mradi wa kufua umeme wenye uwezo wa kuzalisha
Megawati (MW) 100.
2. Upatikanaji
wa IPTL
Mheshimiwa Spika, Mwaka 1994 Serikali ilitoa kazi ya uwekezaji kwa
Kampuni ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL) iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni za VIP Engineering and Marketing Ltd ya Tanzania iliyokuwa na Asilimia 30 na MECHMAR Corporation ya Malaysia (MECHMAR) iliyokuwa na Asilimia 70.
Kampuni ya IPTL ilipewa leseni ya kujenga, kumiliki na kuendesha (Build-Own-Operate) Mtambo wenye uwezo wa
kuzalisha umeme wa MW 100 kwa kutumia mafuta mazito eneo la Tegeta-Salasala,
Dar Es Salaam.
Katika Ukurasa wa 52 Aya ya 2,
ya Taarifa ya PAC, Kamati imependekeza Mtambo huo utaifishwe.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika, Kulingana na Mkataba wa PPA kati ya TANESCO na IPTL, majukumu ya IPTL
yalikuwa ni kujenga, kumiliki na kuendesha (Build, Own and Operate – BOO).
Hivyo, kutaifisha Mtambo huo ni kukiuka makubaliano katika Mkataba wa PPA wa
tarehe 26 Mei 1995, ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza Serikali
katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwenye Mahakama za
kibiashara za kimataifa. Aidha utaifishaji wa miradi ya uwekezaji
binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza
wawekezaji binafsi
|
Mheshimiwa Spika, Tarehe 26 Mei, 1995, TANESCO na IPTL walisaini Mkataba
wa PPA kwa muda wa miaka ishirini (20), kwa ajili ya kununua umeme utakaozalishwa
na IPTL. Kwa mujibu wa Mkataba huo, IPTL ilitakiwa kuiuzia TANESCO umeme
usiopungua Asilimia 85 ya uwezo wa Mtambo (minimum
off take). Hata hivyo, uzalishaji wa umeme haukuanza mara moja kutokana na
mgogoro uliotokea kati ya TANESCO na IPTL kuhusu gharama halisi za uwekezaji na
namna ya kukokotoa Capacity Charges.
Hivyo, IPTL ilianza kuzalisha umeme tarehe 15 Januari, 2002. Kutokana na hali
hiyo muda wa miaka 20 ya Mkataba ulianza kuhesabiwa tarehe 15 Januari, 2002
baada ya kuanza uzalishaji (Commercial Operation
Date).
Mheshimiwa Spika, Pamoja na mambo mengine muhimu yaliyokuwemo katika
PPA, Kifungu Na. 6 cha Mkataba huo kinaipa TANESCO wajibu wa kulipa malipo
yaliyotajwa hapo juu na kwamba endapo kutakuwa na mgogoro wowote kuhusiana na
malipo hayo (Disputed Amount),
itafunguliwa Akaunti maalum (Escrow
Account) ya kuhifadhi fedha hizo hadi pale pande mbili zitakapokubaliana
juu ya uhalali wa malipo yanayobishaniwa. Aidha, chini ya PPA, migogoro yote
kuhusiana na masuala ya utekelezaji wa Mkataba huo ilitakiwa kuwasilishwa na
kuamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji
(ICSID) ya London. Hivyo, ilikuwa ni jukumu la kila mhusika katika Mkataba huu
kuwasilisha malalamiko yake ICSID yanapotokea.
Katika Ukurasa
wa 8 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa mwaka 2004 TANESCO ilifungua
shauri la ICSID 2 kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya Capacity Charge.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Taarifa
hiyo siyo kweli. TANESCO haijawahi kufungua shauri lolote ICSID ya London au
Mahakama yo yote dhidi ya IPTL kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama inavyoelezwa
katika Taarifa ya PAC. Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa tarehe 31 Oktoba 2010
na Standard Chatered Bank Hong Kong (SCBHK) kwa ajili ya kudai malipo ya deni
ililonunua kutokana na mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya Malaysia
kwa IPTL. Wahusika katika Shauri hilo
la ICSID 2 ni SCBHK na TANESCO na wala siyo TANESCO na IPTL.
Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Februari, 2014 ICSID
ilitoa uamuzi kuhusiana na Shauri la SCBHK na TANESCO na kuwashauri wakae
kukokotoa upya malipo ya Capacity
Charge. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo kutekeleza uamuzi huo kutokana
na pande hizo kutokuwa na Mkataba wa kibiashara baina yao. Vile vile, kupitia
Shauri la Madai Na. 60/2014, lililofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na IPTL
tarehe 4 Aprili, 2014 ilizuia utekelezaji wa maelekezo hayo.
|
3. Mgogoro
kati ya IPTL na TANESCO
Mheshimiwa Spika, Migogoro kati ya TANESCO na IPTL ilianza muda
mfupi baada ya PPA kusainiwa tarehe 26 Mei, 1995. IPTL waliitaka TANESCO
wakubaliane bei za kununua umeme kwa kuzingatia gharama za uwekezaji. Pande
hizo mbili zilishindwa kukubaliana gharama za Capacity Charge kwa vile TANESCO walidai kuwa gharama
zilizoainishwa na IPTL ni kubwa kuliko gharama halisi za uwekezaji. Mwaka 1998,
TANESCO iliajiri Kampuni ya Mawakili ya Mkono
& Co. Advocates kutoa huduma za kisheria kwa kushirikiana na Huntons & Williams ya Marekani.
Kutokana na tofauti za gharama za Uwekezaji, Mawakili hawa waliishauri TANESCO
ifungue Kesi ICSID nchini Uingereza dhidi ya IPTL ili kupinga gharama hizo.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia ushauri huo wa Mawakili, TANESCO
ilifungua Kesi Na.ARB/98/8 ya Mwezi Agosti, 1998 ikidai kuwa gharama halisi za uwekezaji
ni Dola za Marekani milioni 90 na siyo milioni 163.53 kama ilivyodaiwa na IPTL.
Aidha, IPTL ilidai kuwa kiwango cha marejesho ya uwekezaji (Internal Rate of Return-IRR) ni Asilimia 23.10 ambacho pia
kilipingwa na TANESCO.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 12 Julai, 2001, ICSID ilitoa uamuzi wa Kesi
hiyo pamoja na mambo mengine kwamba:-
i. Gharama halisi za uwekezaji zikiwemo Mtambo na
nyumba za wafanyakazi wa IPTL zilizoainishwa katika hesabu ya IPTL zilikuwa ni
Dola za Marekani milioni 163.53 lakini ICSID iliona kuwa gharama halisi ni Dola za Marekani milioni 127.20;
ii. Kiwango cha
marejesho ya uwekezaji (Internal Rate of
Return-IRR) ilikuwa Asilimia
22.31 badala ya Asilimia 23.10 iliyodaiwa na IPTL; na
iii. TANESCO na IPTL wakubaliane mfumo wa malipo ya
kununua umeme ukizingatia gharama halisi za uwekezaji na kiwango cha marejesho
ya uwekezaji (IRR) cha Asilimia 22.31 kwa kutumia financial model iliyokubalika na ICSID.
Katika Ukurasa wa 11 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC, imeelezwa kuwa
mtaji wa uwekezaji katika Mtambo wa IPTL ni Shilingi 50,000/= na kwamba huo
ndio ungetumika kukokotoa Capacity
Charges ili kulipa tozo ndogo kuliko ilivyo sasa.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Maelezo hayo siyo sahihi.
Ukweli ni kwamba kutokana na maamuzi ya ICSID 1 ya tarehe 12 Julai, 2001,
gharama za ujenzi wa Mtambo wa Tegeta ni Dola za Marekani 127.20 kama
ilivyoelezwa katika Ukurasa wa 47 Aya ya
4 ya Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika Taarifa
hiyo, pia imeelezwa kuwa ilikubalika kuwa uwiano wa deni na mtaji utakuwa
70:30. Hii ikiwa na maana kwamba, deni ni Dola za Marekani milioni 89.04 na
mtaji ni Dola za Marekani milioni 38.16. Uamuzi huo haujabadilishwa na
Mahakama yo yote au mtu ye yote.
Mheshimiwa Spika, tunakubaliana kwamba fedha
iliyopokelewa kutoka Mabenki ya Ushirika ya Malaysia kama mkopo ni Dola za
Marekani milioni 85.86. Kati ya Dola za Marekani milioni 105 zilizokuwa
zimeidhinishwa. Swali la kujiuliza, je Mtambo huo ulikamilikaje kwa gharama
ya Dola za Marekani milioni 85.86, huku
gharama halisi ya ujenzi wa Mtambo wa Tegeta ikawa Dola za Marekani milioni
127.20?
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba kuna
matumizi ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 38.16 ambazo pia zimetumika
kwenye uwekezaji. Taarifa ya Kamati ya PAC haikuonesha fedha hiyo kuwa sehemu
ya uwekezaji.
|
Mheshimiwa Spika, Tarehe 30 Juni, 2004, Kampuni
ya Mawakili iliyokuwa ikiiwakilisha TANESCO katika kesi ya kwanza ya
usuluhishi, Kampuni ya Mkono & Co Advocates, iliishauri TANESCO iendelee
kupinga kiwango cha malipo ya Capacity
Charge kilichokuwa kimeafikiwa tarehe 12 Julai, 2001 na pande hizi mbili katika
Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) ya
London. Hii ilikuwa ni miaka miwili tu baada ya usuluhishi uliochukua miaka
minne kukamilika na Mtambo kuanza kuzalisha umeme tarehe 15 Januari, 2002.
Mheshimiwa Spika, Hata
hivyo, baada ya ushauri huu, Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates)
hawakuishauri TANESCO ifungue kesi katika Mahakama za Tanzania wala katika
Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kimataifa (ICSID) ya London.
Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia tarehe 5 Septemba, 2013 wakati Mheshimiwa
Jaji Utamwa anatoa hukumu yake juu ya mgogoro wa WanaHisa wa IPTL hapakuwepo na
kesi yo yote kwenye Mahakama yo yote ya kupinga
gharama za Capacity Charge kati ya TANESCO na IPTL, iwe katika Mahakama za
ndani au za nje. Kwa kutokuwepo Msuluhishi (Broker)
katika suala hili, madai yo yote ya TANESCO yanakuwa ni madai ya upande mmoja
ambayo kisheria hayawezi kuchukuliwa kuwa ndiyo madai halisi. Kwa sababu hiyo haikuwepo formula rasmi ya
kuutatua mgogoro huo zaidi ya majadiliano na maafikiano kati ya pande mbili
(TANESCO na IPTL).
4. Uuzaji
wa Hisa za VIP
Mheshimiwa Spika, Kutokana na VIP Engineering and Marketing Limited
(VIP) kuona kuwa hainufaiki na ubia wake katika IPTL, ilikusudia kuuza Hisa
zake kwa MECHMAR. Hata hivyo, MECHMAR haikuweza kununua Hisa hizo kwa sababu
ilitaka thamani ya Hisa za VIP zitokane na ripoti ya ukaguzi ya mwaka (Audited Financial Report) na taratibu za
kihasibu za kimataifa (International
Accounting Rules), VIP haikukubaliana na utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na kutokubaliana, MECHMAR iliishauri VIP ifungue
Shauri la madai hayo kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Uingereza (LCIA)
kulingana na Mkataba wa Wanahisa wa IPTL. Hata hivyo, VIP haikufungua Shauri
katika Mahakama ya usuluhishi kama ilivyoshauriwa na MECHMAR badala yake tarehe
25 Februari, 2002 VIP ikafungua Shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania
(Miscellaneous Civil Application No. 49/2002) ikiomba Kampuni ya IPTL ifilisiwe
ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuanza uzalishaji.
5. Uamuzi
kuhusu Ufilisi wa IPTL
Mheshimiwa Spika, Shauri lililofunguliwa na VIP tarehe 25 Februari,
2002 liliendelea kuwa Mahakamani hadi ilipofika tarehe 16 Desemba, 2008.
Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya Jaji Oriyo, J ilitoa uamuzi wa kuiweka IPTL
katika Ufilisi wa Muda (Provisional Liquidation) chini ya Kabidhi Wasii Mkuu
(Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini - RITA). Mfilisi wa Muda alipewa
majukumu maalum yafuatayo:
i.
Kulinda
mali zote za IPTL katika kipindi chote cha Ufilisi wa Muda; na
ii.
Kufanya
uchunguzi wa tuhuma zote zilizotolewa na VIP dhidi ya MECHMAR na kutoa ripoti
za uchunguzi huo ili Mahakama iweze kutoa uamuzi.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 15 Julai, 2011, Mahakama Kuu ya Tanzania
(Kaijage, J) ilitoa uamuzi kwamba, IPTL iwekwe kwenye Ufilisi Kamili (Full
Liquidation) na RITA ilithibitishwa kuwa Mfilisi wa IPTL.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Standard Chartered Bank Hong Kong (SCBHK) iliyokuwa imenunua deni la IPTL
kutoka kwa DANHARTA, ilipinga na kuiomba Mahakama ya Rufaa ifanye mapitio ya
uamuzi wa Mahakama Kuu (Application for Revision – Civil Revision No. 1/2012)
ikiainisha dosari katika uamuzi wa Mahakama Kuu ulioamuru kufilisiwa kwa IPTL.
SCBHK ilibainisha dosari za maombi ya kutaka IPTL kufilisiwa kwa kuwa maombi ya
SCBHK ya kutaka Mahakama iteue msimamizi (Administrator) wa kuisimamia IPTL
(kwa niaba ya SCBHK) yalikuwa hayajasikilizwa.
Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilikubaliana na hoja
za SCBHK na hivyo kuamuru shauri hilo lirejeshwe Mahakama Kuu ili IPTL irudi
mikononi mwa Mfilisi wa Muda (Provisional Liquidator) ambaye alipewa majukumu
yafuatayo:-
i.
Kukusanya
mali na madeni yote ya IPTL;
ii.
Kupokea na
kusajili madeni yote dhidi ya IPTL;
iii.
Kusuluhisha
migogoro kati ya wanahisa wa IPTL; na
iv.
Kusimamia
na kuendesha Mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL kwa niaba ya IPTL.
Mheshimiwa Spika, Baada ya kuteuliwa, Mfilisi wa Muda (Provisional
Liquidator) alifanya juhudi ya kumaliza mgogoro huo wa IPTL nje ya Mahakama kwa
kushirikisha wadau mbalimbali (Stakeholders) wa IPTL kupitia kikao chake cha
tarehe 9 Novemba, 2011. (Kiambatisho Na.1). Juhudi hizo
hazikufanikiwa na ikalazimu shauri liendelee Mahakamani.
6. Uhalali wa uhamishwaji wa
Asilimia 70 za Hisa za
MECHMAR
kwenda PAP
Mheshimiwa Spika, Suala
la uhalali wa umiliki wa Hisa katika Kampuni hizi linahusu wanahisa wa Kampuni
wenyewe. Serikali haiwajibiki
kuingilia mahusiano ya kibiashara ya wanahisa katika
Kampuni Binafsi. Hata hivyo,
kulingana na Sheria za nchi ikiwa ni pamoja na Kifungu cha 172 cha Sheria ya Makampuni (Sura 212), mauziano ya Hisa
yaliyofanyika nje ya nchi yatatambuliwa tu, endapo usajili wa Hisa hizo
utafanyika hapa nchini. Kwa mujibu wa taarifa za BRELA za tarehe 31
Desemba, 2013, zinaonesha kuwa uhamishaji wa Hisa 7 za MECHMAR katika IPTL
kwenda PAP ulisajiliwa hapa nchini. Kwa maana hiyo, PAP ni mmiliki wa Asilimia
70 za IPTL.
Katika
ukurasa wa 44 Aya ya 1 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa PAP siyo mmiliki
halali wa Hisa 7 za MECHMAR katika IPTL.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, katika
maelezo ya Kamati ukurasa wa 30, Kamati imethibitisha kwamba nyaraka za
mauziano kati ya MECHMAR na Piper Link zilipokelewa na Harbinder Singh Sethi
ambaye pia ndiye mmiliki wa PAP. Kwa uthibitisho huo, Kamati inakubali kuwa
Hisa za MECHMAR katika IPTL zinamilikiwa na PAP.
|
Katika
Ukurasa wa 25 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa hakuna ushahidi wa
PAP kumiliki Asilimia 70 ya Hisa zilizokuwa zikimilikiwa na MECHMAR katika
IPTL.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa umiliki wa Hisa 7 za IPTL unatambuliwa
hata na SCBHK ambayo ilisaini makubaliano tarehe 25 Novemba, 2011 na PAP ya
kulipwa deni la mkopo wa fedha za kununua deni la ujenzi wa Mtambo wa Tegeta.
Kiambatisho Na 2.
|
7. Majadiliano
ya mikopo ya IPTL na Wadai
Mheshimiwa Spika, Kutokana na Hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania
iliyotolewa tarehe 5 Septemba, 2013, Kampuni ya PAP ilijadiliana na wadai halali wa mikopo ya IPTL na kuingia Mkataba
wa kuwalipa wadai wote wa IPTL. SCBHK inayodai kuidai IPTL mikopo katika ujenzi
wa Mtambo wa Tegeta haikuwasilisha madai ya aina yo yote ili iweze kulipwa.
Mheshimiwa Spika, Ukweli ni kwamba, SCBHK iliyokuwa ikiidai IPTL
fedha ilizotumia kununua deni lililotokana na kufilisiwa kwa MECHMAR kule
Malaysia (siyo Tanzania) haijawahi kujadiliana na IPTL kuhusu malipo ya mkopo
wake kama upo. Mvutano huu unaendelea ICSID kati ya TANESCO na SCBHK, ukiitaka
TANESCO ilipe gharama za kununua umeme ikijumuisha deni la IPTL. Madai ya SCBHK
dhidi ya TANESCO yanatokana na madai ya kuwepo kwa Deed of Assignment ya MECHMAR kuhusiana na Mkopo
wa IPTL ambapo Mtambo wa IPTL uliwekwa kama dhamana ya Mkopo.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo Deed
of Assignment hiyo haikuwahi kusajiliwa hapa nchini kama inavyotakiwa
katika Kifungu Na. 172 cha Sheria za Makampuni Sura. 212 zinavyoelekeza.
Kutokana na kutokusajili Assignment Deed
hiyo, SCBHK ilikosa sifa za kufungua
madai yake hapa nchini badala yake ilifungua madai haya ICSID nchini Uingereza.
Kitendo hicho kinaonesha kudharau Mahakama zetu na PAC inataka tuziamini
Mahakama za nje kuliko za kwetu.
8. Jitihada za Makampuni mbali mbali kununua Hisa
za VIP
Mheshimiwa Spika, Kutokana na tofauti
zilizokuwepo kati ya MECHMAR na VIP kuanzia mwanzo wa mradi, VIP iliamua kuuza Hisa
zake zilizoko IPTL kwa makampuni mbalimbali kwa nyakati tofauti ikiwemo MECHMAR
kama mwanahisa mwenzake, NSSF, Camel
Oil, Great White Shark Opportunity Fund pamoja na SYMBION lakini haikuwezekana
kutokana na kutoafikiana katika bei.
Mheshimiwa Spika, Baadaye VIP chini ya
usuluhishi ya RITA, iliuza Hisa zake kwa PAP kwa thamani ya Dola za Marekani
milioni sabini na tano (US$ 75,000,000/=). Ununuzi wa Hisa Asilimia 30 za VIP
uliofanywa na PAP ndiyo uliyomaliza mgogoro wa Wanahisa uliyokuwa Mahakamani na
kuufanya Mtambo wa IPTL kumilikiwa na PAP kwa kuwa ndiyo iliyomiliki Hisa zote Asilimia
100 za IPTL.
Taarifa ya PAC: Katika ukurasa wa 58 wa Taarifa
ya PAC imeelezwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye aliyekuwa Dalali Mkuu
aliyewakutanisha Bw. Harbinder Sethi na Bw James Rugemalira
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Taarifa hii siyo sahihi kwa
kuwa tangu tarehe 9 Novemba, 2011, RITA aliitisha mkutano na kuwakutanisha
wadau wote wa IPTL. Wakati huo, Waziri wa Nishati na Madini aliyeko sasa
alikuwa bado hajateuliwa kwenye wadhifa huo.
|
9. Kufungua
ESCROW Akaunti
Mheshimiwa Spika, Tarehe 30 Juni, 2004, TANESCO kwa ushauri wa Mkono & Co Advocates walitoa hoja
kuwa gharama za kununua umeme zilikokotolewa kwa kutumia IRR ya Asilimia 23.10
na makadirio ya gharama za mtaji wa Asilimia 30 ambao ni Dola za Marekani milioni 38.16, wakati mtaji halisi (equity) wa IPTL ni chini ya Dola za
Marekani 100. Hivyo, TANESCO walikuwa wakitoa notisi (Dispute Notice) kwa kila Ankara ya malipo kupinga gharama hiyo
kulingana na Kifungu Na. 6.8 cha Mkataba wa PPA. Kifungu hicho kinaeleza kuwa
ikiwa upande wote haukubaliani na usahihi wa malipo katika Ankara
zilizowasilishwa kwa ajili ya malipo ya gharama za umeme wanatakiwa watoe notisi
(Invoice Dispute Notice) kwa upande
mwingine. Vile vile, Mawakili wa TANESCO (Mkono & Co Advocates) walishauri
kwamba kutokana na pingamizi hilo, ifunguliwe Akaunti Maalum (Escrow Account) kwa ajili ya kuhifadhi
fedha ambazo zilitokana na Ankara zilizokuwa zinapingwa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ushauri wa Mkono Co. & Advocates tarehe 5 Julai, 2006,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilisaini Mkataba wa kufungua
Akaunti Maalum (Escrow Account) kwa
ajili ya kuweka fedha zote za Ankara zilizopaswa kulipwa kwa IPTL.
10.
Mmiliki wa Fedha za
Akaunti ya Escrow:
Mheshimiwa
Spika, katika Taarifa ya Kamati ya PAC ukurasa wa 22 imeelezwa kuwa Akaunti ya
Escrow ilipaswa kuwa na Shilingi bilioni
306.70 ambazo zingekuwa zimewekwa na TANESCO. Hata hivyo, katika
mapendekezo ya Kamati ya PAC ukurasa wa
50, Kamati imeeleza kwamba imethibitisha bila chembe ya mashaka kwamba
mchakato mzima wa kutoa fedha katika Akaunti ya Escrow umegubikwa
na mchezo mchafu na kwamba Mfumo mzima wa Serikali ulipata ganzi ili kuwezesha
zaidi ya Shilingi bilioni 306
kuporwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania na kutakatishwa kupitia benki mbili hapa
nchini.
11. Tahadhari iliyochukuliwa na Serikali wakati wa
kutoa
fedha kwenye akaunti ya Escrow
Mheshimiwa Spika, kwa kuelewa kwamba kunaweza kukatokea madai kwa
IPTL, na kwa kuwa Serikali ilitoa dhamana kwa TANESCO ya kununua umeme wa IPTL,
Serikali ilihakikisha inachukua KINGA (Indemnity)
kutoka IPTL katika maeneo yote muhimu. Kwa mujibu wa KINGA hiyo, kama
kutajitokeza madai yo yote yale, IPTL yenyewe itawajibika. Ikumbukwe kuwa kabla
ya kusaini, KINGA hiyo ilipitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
kuthibitisha kwamba inakidhi matakwa ya kulinda maslahi ya Taifa. KINGA hii ilitolewa
tarehe 27 Oktoba, 2013. Inasema, nanukuu:
“IPTL do hereby
agree to INDEMNIFY and keep INDEMNIFIED the Government and the Escrow Agent
(jointly and severally) against all present
and future claims, actions and legal proceedings that may arise in respect of
and/or all losses, charges, costs, and expenses the Government and the Escrow
Agent may suffer or incur consequent upon the release and payment of the funds
in the Tegeta Escrow Account or part thereof to IPTL pursuant to the Agreement
for Delivery of Funds”.
KatikaUkurasa wa 48 wa Taarifa ya
PAC, imeelezwa kuwa Serikali haikuchukua tahadhari ya kutosha dhidi ya madai
mengine yanayoweza kujitokeza kabla ya kutolewa kwa fedha kutoka akaunti ya
Escrow.
Ufafanuzi
Mheshimiwa
Spika, KINGA iliyochukuliwa inakidhi matakwa ya kisheria na imezingatia
athari yo yote ambayo ingeweza kutokea baadaye kutokana na kutolewa kwa fedha
katika Akaunti ya Escrow. Kwa hiyo siyo kweli kwamba Serikali haikuchukua
tahadhari kama ilivyodaiwa na PAC.
|
12.
Dhana ya Madai ya Shilingi Bilioni 321
Mheshimiwa Spika, Madai
ya kwamba TANESCO inaidai IPTL Shilingi bilioni 321 msingi wake ni dhana kwamba
mtaji wa IPTL ni Dola za Marekani 100, sawa na Shilingi za Tanzania 50,000/- kwa wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola
za Marekani milion 38.16 ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta. Aidha, Bodi ya
TANESCO imekana kuyatambua madai hayo ya Shilingi
bilioni 321. Kimsingi hata Vitabu
vya Hesabu vya TANESCO ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG, havioneshi kuwepo
kwa deni hilo.
Mheshimiwa Spika, Madai ya Shilingi
bilioni 321 yaliyowasilishwa kwa Mfilisi na Mwanasheria wa TANESCO (Mkono
& Co. Advocates) ulihitaji kuhakikiwa kabla ya kukubaliwa na Mfilisi kama
madai halali. Hata hivyo, uhakiki huo haukufanyika kwa sababu ya Hukumu ya
Mahakama ya Rufaa katika Civil Revision
No. 1 ya Mwaka 2012, ambayo ilifuta maamuzi ya Mahakama Kuu ya kuiweka IPTL
katika Ufilisi na kuirudisha kwenye Ufilisi wa Muda. Hivyo, madai hayo ya Shilingi bilioni 321 na kiapo chake ambacho
hakitambuliwi na Bodi ya TANESCO hayakuwa tena na uhalali wo wote.
Kamati ya PAC: Katika ukurasa wa 47 Aya ya 2 Kamati
imejiridhisha kuwa madai ya TANESCO ya Shilingi Billioni 321 yana uhalali japo
usahihi wake utapatikana baada ya kutekelezwa kwa uamuzi wa ICSID 2 na
TANESCO na IPTL kukubaliana kiwango sahihi cha Capacity Charge.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika,
Madai ya kwamba TANESCO inaidai IPTL Shilingi bilioni 321 msingi wake ni
dhana kwamba mtaji wa IPTL ni Dola za Marekani 100, sawa na Shilingi za
Tanzania 50,000/- kwa wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola za
Marekani milion 38.16 ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta. Aidha, Bodi ya
TANESCO imekana kuyatambua madai hayo ya Shilingi bilioni 321. Kimsingi
hata Vitabu vya Hesabu vya TANESCO ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG,
havioneshi kuwepo kwa deni hilo.
|
13.
TANESCO
na IPTL kufanya Reconcillation
ya fedha iliyokuwa kwenye Akaunti ya Escrow
Mheshimiwa Spika, TANESCO
kwa kushirikiana na IPTL ilifanya uhakiki (reconciliation)
tarehe 9 Oktoba, 2013 ili kujua madai halali ya IPTL kabla ya kufanya malipo. Takwimu za Mfilisi wa Muda
wa IPTL (RITA) wakati akikabidhi mali na madeni ya IPTL, ilionesha kwamba deni
lote alilokuwa akidaiwa TANESCO na IPTL kama Capacity Charges ni Shilingi
bilioni 370.70, sawa na Dola za Marekani milioni 224.30. Katika majadiliano
kati ya TANESCO na IPTL, gharama zilizokubaliwa kama Capacity Charges zilizokuwa zinadaiwa ni Shilingi bilioni 275.20. Fedha hizi ni pungufu kwa Shilingi bilioni 95.50 ya madai ya
IPTL. Hadi kufikia tarehe 25 Novemba, 2013, fedha iliyokuwa katika Akaunti ya Escrow
ilikuwa jumla ya Dola za Marekani milioni
22.20, sawa na Shilingi bilioni
36.72 na Shilingi bilioni 161.39.
Mheshimiwa
Spika, ukaguzi maalum umeonesha pia kuwa fedha
zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow wakati wa kuifunga ni Shilingi bilioni 182.77 na kuwa na upungufu wa Shilingi bilioni
123.90 wa madai ya IPTL.
14.
Iwapo
Serikali ilistahili kutoa fedha katika Akaunti
ya
Escrow wakati Shauri la ICSID, London inaendelea.
Mheshimiwa Spika, Kesi
iliyopo ICSID, London ilihusu madai ya Benki ya Standard Chatered ya Hong Kong yaliyotokana
na kununua deni lililotokana na uwekezaji katika Mtambo wa IPTL wa Tegeta. Katika Mkopo huo, Mkataba wa kuuziana
umeme (PPA) na Mtambo wa kuzalisha umeme wa Tegeta viliwekwa kama dhamana.
Mheshimiwa Spika, TANESCO haikuhusishwa kwenye
majadiliano ya dhamana hiyo. IPTL ilishindwa
kumaliza marejesho ya Mkopo huo na hivyo Benki ya Standard Chartered ya Hong
Kong kuanza kuidai TANESCO madeni yaliyotokana na Mkopo huo. Hata hivyo, fedha
katika Akaunti ya Escrow ilitokana na Ankara za Capacity Charges zilizokuwa zikibishaniwa kati ya TANESCO na IPTL
kuhusu viwango vilivyotumika
kukokotoa malipo hayo na siyo mikopo ya IPTL.
Mheshimiwa Spika, Hata
hivyo, Standard Chartered Bank Hong
Kong siyo mhusika (not a party)
katika Mkataba wa tarehe 26 Mei, 1995 wa PPA kati ya TANESCO na IPTL. Kwa
mujibu wa Sheria za Tanzania, madai yo yote yaliyotokea nje ya nchi yakihusu
uwekezaji ulioko nchini ni lazima yasajiliwe hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kwa
mantiki hiyo, Shauri lililoko ICSID, London halihusiani na fedha za Akaunti ya Escrow bali
mikopo ya IPTL. Hata hivyo, wadai wa IPTL waliamriwa na Mahakama Kuu ya
Tanzania tarehe 5 Septemba,
2013 kuwasilisha madai yao kwa PAP. Benki ya Standard Chatered ya Hong Kong haijafanya
hivyo.
15.
Ulipwaji
wa Madai na Madeni
Mheshimiwa Spika, Kuhusu
madai na madeni dhidi ya IPTL ikiwemo VAT, Serikali na BOT ziliitaka IPTL iweke
KINGA (Indemnity)
ili kuihakikishia Serikali kuwa endapo kutakuwa na madai au madeni ya aina
yo yote, IPTL itawajibika kuyalipa. Tarehe 27 Oktoba, 2013, IPTL ilitoa KINGA
hiyo, nanukuu:
“IPTL do
hereby agree to INDEMNIFY and keep INDEMNIFIED the Government and the Escrow
Agent (jointly and severally) against all present and future claims, actions
and legal proceedings that may arise in respect of
and/or all losses, charges, costs, and expenses the Government and the Escrow
Agent may suffer or incur consequent upon the release and payment of the funds
in the Tegeta Escrow Account or part thereof to IPTL pursuant to the Agreement
for Delivery of Funds”.
16.
Gharama
za Mawakili (Mkono & Co. Advocates na
Hunton
& Williams ya Marekani) Katika Kuendesha Kesi za IPTL
Mheshimiwa Spika, Hadi
Hukumu ya Mheshimiwa Jaji Utamwa inatolewa tarehe 5 Septemba mwaka 2013, TANESCO
na Serikali zilikuwa zimewalipa Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton &
Williams) jumla ya Shilingi za Tanzania
bilioni 62.90 na bado Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates na Hunton
& Williams) wanaidai TANESCO Dola za Marekani milioni 4.50. Katika ushauri wao walikuwa wamependekeza
kwa Serikali wapewe kazi nyingine ya kwenda kutetea Guarantee ya Serikali pamoja na kupinga
Hukumu ya tarehe 12 Februari, 2014 iliyotolewa katika uamuzi wa ICSID-2. Ushauri
wao upo katika Memorandum ya tarehe 9
Oktoba, 2013 waliyowasilisha TANESCO.
Mheshimiwa
Spika,
Wakati
ambapo hatukujua ni kiasi gani Serikali na TANESCO ingeweza kupata kwa
kuendelea kupinga Capacity Charges za IPTL, tunajua
fika ni hasara gani tumepata
kupitia malipo ya Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams)
yaani ya Shilingi bilioni 62.9 na bado
wanadai Dola za Marekani milioni 4.5.
Mheshimiwa Spika, kumalizika kwa mgogoro huu wa
IPTL si tu kwamba kumetuondoa kwenye hatari ya kuendelea kukamuliwa na Mawakili
(Mkono & Co. Advocates na Hunton &
Williams) hawa bali pia katika mazungumzo yaliyofanywa kati ya TANESCO na IPTL tumeweza
kuokoa takribani Shilingi bilioni 95 katika madai ya awali ya IPTL.
17.
Ushauri
wa Mawakili (Mkono & Co. Advocates na
Hunton
& Williams) wa TANESCO wa Tarehe 4
Oktoba, 2012
Mheshimiwa
Spika, Mawakili wa TANESCO na Serikali yaani Kampuni za
Mkono & Co Advocates na Hunton & Williams waliandika ushauri wa pamoja
wa tarehe 4 Oktoba, 2012 ambapo
walifafanua kwa kina juu ya Shauri
lililokuwa likiendelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro
ya Kibiashara (ICSID) ya London. Katika Ushauri wao walionyesha wazi kwamba
TANESCO ilikuwa na nafasi finyu mno ya kushinda katika Kesi iliyokuwa
ikiendelea kati ya TANESCO na SCBHK.
Mheshimiwa
Spika, katika ushauri wao walieleza mambo muhimu ambayo
ni vema Bunge lako Tukufu likayaelewa hasa kwa ajili ya watu wanaodhani kwamba
ilikuwa ni makosa kwa TANESCO kukaa na IPTL baada ya Hukumu ya Mahakama Kuu ya
tarehe 5 Septemba, 2013. Baadhi ya maeneo walioshauri TANESCO ikae na IPTL
kujadiliana kwa kile kilichoelezwa na Mawakili (Mkono & Co. Advocates na
Hunton & Williams) kuwa uwezekano wa kushinda kesi ni mdogo ni pamoja na:-
18.
Ushauri
wa Mawakili unaokinzana
Mheshimiwa Spika, tarehe
4 Oktoba, 2012, Mawakili wetu (Mkono & Co.
Advocates na Hunton & Williams) walitoa ushauri kwamba, kwa kuzingatia
utetezi walioutoa kwa TANESCO kwenye kesi hii kule ICSID, London kiasi cha
chini kabisa kinachoweza kuidhinishwa na Mahakama ya ICSID, London kama malipo
ya Capacity Charges kwa IPTL ni kati ya Dola za Marekani milioni 85
hadi 90 na Mawakili wetu (Mkono & Co. Advocates na Hunton &
Williams) wakasema, nanukuu, “This
could be considered TANESCO’s Best Case
Scenario”. Hata hivyo waliendelea kusema “This best Case Scenario is
overly optimistic”
Mheshimiwa
Spika,
katika
maelezo yao mengine ya tarehe 4 Oktoba, 2012, Mawakili hawa (Mkono & Co.
Advocates na Hunton & Williams)
wanasema, “In these circumstances, SCBHK may recover 100% of its claimed
damages of USD 130 milion even if substantially TANESCO prevails on a portion
of its equity defense”.
Kwa lugha nyingine Mheshimiwa Spika Mawakili
hawa (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) wanasema kiasi cha
chini kabisa ambacho TANESCO ingedaiwa na SCBHK kingekuwa Dola za Marekani milioni 130 bila
kujumuisha gharama nyingine za moja kwa moja kwa IPTL.
Mheshimiwa
Spika, Katika majumuisho yao
ya tarehe 4 Oktoba, 2012, Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton &
Williams) waliishauri TANESCO ikae na SCBHK na kukubaliana nje ya Mahakama na
kumlipa Dola za Marekani kati ya milioni 75 na milioni 90 na kiasi
kitakachobaki kikidaiwa kilipwe
kwa wadai wengine, wakiwemo IPTL, Law
Associates na Kampuni ya Mafuta ya TOTAL.
Mheshimiwa
Spika, Kufikia tarehe 5 Septemba, 2013 kwa mujibu wa Taarifa ya Mfilisi (RITA),
ilionesha kuwa Kampuni ya IPTL ilikuwa
ikiidai TANESCO zaidi ya Dola za
Marekani milioni 224.30, sawa na
Shilingi bilioni 370.70. Majadiliano yaliyofanyika kati ya TANESCO na IPTL tarehe
9 Oktoba, 2013 yaliwezesha kukubaliana kuwa malipo stahiki kwa IPTL ni jumla ya
Dola za Marekani milioni 166, sawa
na Shilingi bilioni 274.56. Kati ya
hizo, Dola za Marekani milioni 121, sawa
na Shilingi bilioni 220.13 zilikuwa
kwenye Akaunti ya ESCROW na Dola za Marekani milioni 45, sawa na Shilingi bilioni 74.43 zitalipwa kwa
kipindi cha muda mrefu usiozidi miaka mitano.
19. Kama
fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow ni za Umma
Katika ukurasa wa 58 wa Taarifa ya
PAC imeelezwa kuwa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow zilikuwa za
Serikali.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Huu si ukweli zipo sababu kuu zinazothibitisha kuwa fedha hizo hazikuwa za
Serikali.
1. TANESCO
ilikuwa inapata huduma ya umeme bila kulipa moja kwa moja IPTL, lakini ikawa
inapeleka fedha hizo katika Akaunti ya Escrow.
2. TANESCO
ilisimamisha kupeleka malipo kwenye Akaunti ya Escrow na wala kulipa IPTL kuanzia
tarehe 30 Oktoba, 2010.
Pamoja na kutokulipa, TANESCO iliendelea kupata
huduma ya umeme kwa kadri ilivyohitaji kutoka IPTL.
Mheshimiwa
Spika, katika Ukurasa wa 36 hadi 42
wa Taarifa ya Ukaguzi Maalum ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali ambayo tumekabidhiwa inaonesha kiasi ambacho TANESCO inadaiwa na
IPTL.
Mheshimiwa
Spika, Kulingana na Taarifa hiyo ukurasa
wa 36 hadi 42 imeonesha kuwa
kiasi ambacho kilipaswa kuwekwa kwenye Escrow Account kwa mujibu wa Ankara za
IPTL ni Shilingi bilioni 306.68. hata
hivyo, kwa mujibu wa Ukaguzi huo fedha zilizokuwa kwenye Akaunti wakati wa kuifunga ni Shilingi bilioni 182.77 na kuwa na upungufu wa Shilingi bilioni 123.90 ikiwa ni deni ambalo TANESCO bado wanadaiwa
na IPTL.
Mheshimiwa
Spika, Kwa msingi huo fedha zote
zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow ni mali ya IPTL na IPTL kama Wakala wa
Kodi anastahili kudaiwa na mwisho kulipa kodi yo yote ambayo hajalipa.
Kwa
msingi huo, Taarifa ya PAC haisemi ukweli kuhusu fedha zilizowekwa katika
Akaunti ya Escrow kuwa ni fedha za umma.
|
Mheshimiwa
spika, ili kuthibitisha kwamba fedha hizi siyo za Umma,
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ukaguzi wake wa
Hesabu za TANESCO wa tarehe 31 Desemba, 2012 alielekeza kutoa fedha za Escrow
kwenye Vitabu vya Hesabu vya TANESCO na kupunguza deni kwa kiasi hicho hicho
kwa maelezo yafuatayo:
“As a result,
the deposit balance in Escrow account does not meets the definition of an asset
of the Company and therefore an adjustment has been made to de-recognize the
asset and related liability to the tune of the amounts available in the Escrow
account”.
20. Iwapo kwa mujibu wa Mkataba wa PPA TANESCO na IPTL
walilazimika kutumia Mtaalamu wa Upatanishi (Mediation Expert) katika utatuzi wa mgogoro kabla ya kutolewa fedha zilizopo
kwenye Akaunti ya Escrow.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Kamati ya PAC ukurasa wa 9, imeeleza kuwa kwa mujibu wa Mkataba wa PPA, TANESCO na IPTL walipaswa
kutumia Mtaalam wa Upatanishi katika mgogoro wa Capacity Charge.
Mheshimiwa Spika, tunapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa kwa mujibu wa Ibara ya
18.1 ya Mkataba wa PPA, wahusika wa Mkataba huo ambao ni TANESCO na IPTL
wanatakiwa kwanza kumaliza mgogoro baina yao kwa njia ya upatanishi (amicable settlement). Iwapo watashindwa
kufikia makubaliano ndipo watalazimika kutumia Mtaalam wa Upatanishi kutatua
mgogoro huo. TANESCO na IPTL walimaliza mgogoro baina yao kwa njia upatanishi
kwa kufanya uhakiki wa kiasi ambacho kila upande ulikuwa unastahili kulipwa
katika Akaunti ya ESCROW kabla ya akaunti hiyo kufungwa. Kwa msingi huo,
hapakuwa na sababu ya kutumia Mtaalam wa Usuluhishi kama ilivyoelezwa katika Taarifa
ya PAC.
21.
Kama
muda wote wa Mkataba wa TANESCO na IPTL hapakuwahi kuwa na Kamati ya Uendeshaji
Mheshimiwa Spika, taarifa ya PAC inaeleza kuwa hapakuwahi kuwa na Kamati ya Uendeshaji
kwa kipindi chote cha Mkataba wa PPA. Ukweli ni kwamba, Kamati ya Uendeshaji
iliundwa kabla ya kuanza uzalishaji wa Mtambo hapo 2002 na imeendelea kuwepo
hadi leo. Kamati hiyo ina wajumbe sita.
Wajumbe watatu kati ya hao wanatoka TANESCO. Wajumbe watatu waliobakia wanatoka
IPTL. Wajumbe wa TANESCO walikuwa ni kama ifuatavyo:
1. Mhandisi Masanyiwa Malale;
2. Mhandisi Christian Msyani; na
3. Mhandisi James Mtei.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo si kweli kwamba Kamati ya
Uendeshaji haikuundwa kama ilivyoelezwa na Kamati ya PAC katika ukurasa wa 10.
22. Wizara
kutambua Hati za Hisa za Makampuni
Mheshimiwa
Spika, katika ukurasa wa 27 wa Taarifa ya Kamati ya PAC, Kamati hiyo imeitaka
Wizara ya Nishati na Madini kutambua usajili wa Hati za Hisa za Makampuni. Tunaomba
ieleweke kuwa siyo majukumu ya Wizara kutambua na wala kujishughulisha na Hati
za Hisa za Makampuni Binafsi. Aidha, katika ukurasa wa 45, imeelezwa kwamba “Waziri wa Nishati na Madini ndiyo
Mamlaka ya kuthibitisha uhamishaji wa umiliki wa Kampuni katika sekta yake”.
Ningependa kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba jukumu hilo pia siyo la Wizara
ya Nishati na Madini ni vizuri majukumu ya Wizara yakaangaliwa vizuri na
kutoleta mkanganyiko na kuwadanganya wananchi wetu. Hii inaonesha kuwa kamati
haikupitia vizuri majukumu ya Wizara.
Mheshimiwa
Spika, katika Taarifa ya PAC, ukurasa wa 30 Aya ya 2, imeelezwa
nanukuu “nilishuhudia nyaraka kwamba
Piper Link ilinunua Hisa za MECHMAR na katika mauziano hayo Kampuni hiyo
iliwakilishwa na Bw. Harbinder Singh Sethi hivyo huyu bwana ndiye Piper Link na
ndiye PAP”. Kwa maneno haya ya Kamati ya PAC, aliyekuwa na hati za Piper
Link ni Bw. Sethi na aliyenunua Piper Link ni Bw. Sethi anayemiliki PAP. Kwa
kuzingatia maelezo haya ya kamati ya PAC, inaonesha kwamba hakuna tatizo la
uhamishaji wa Hisa Asilimia 70 kwenda kwa PAP.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na maelezo ya Aya
iliyotangulia, bado Kamati ya PAC ukurasa
44 wa taarifa yake, inaonesha kuwa Hisa hizo zinashikiwa na Martha Renju
huko BVI lakini Martha Renju amefungua kesi mara mbili Mahakama Kuu ya Tanzania
kwa kutumiwa na SCBHK akiwa na lengo la kutaka kujipatia fedha za Escrow bila
uhalali. Hata hivyo, amekuwa akiziondoa kesi hizo mahakamani.
23.
Mikutano
ya Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO
Mheshimiwa
Spika,
katika ukurasa wa 29 wa Taarifa ya
PAC, inasema kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ilifanya mikutano miwili
mfulilizo kati ya tarehe 16 na tarehe 19 Septemba, 2013 na kwamba uharaka huo
unatia mashaka kwamba kulikuwa na njama.
Mheshimiwa
Spika, muda wa siku 3 kwa Bodi kukutana si jambo la kutiliwa
mashaka kwani Bodi haikutani kwa ajenda moja tu. Napenda kulijulisha Bunge lako
Tukufu kuwa tarehe 16 Septemba, 2013 hapakuwa na kikao cha Bodi isipokuwa kikao cha Bodi kilifanyika tarehe 19
Septemba, 2013. Hivyo si sahihi kusema kuwa Bodi ya TANESCO ilikuwa ina njama
katika kushughulikia na kulitolea maamuzi suala la Akaunti ya Escrow na kwamba
ilikutana ndani ya siku tatu.
24.
Hoja
ya Mwanasheria wa TANESCO Kufukuzwa Kazi
Mheshimiwa
Spika, katika ukurasa
wa 30 wa Taarifa ya PAC kuna hoja kuwa Mwanasheria wa TANESCO kwa wakati
huo Bw. Godwin Ngwilimi aliagizwa na TANESCO kwenda Malaysia kufanya Due Diligence ya Kampuni ya MECHMAR
Corporation na kwamba taarifa hiyo ya Due
Diligence ilifikishwa katika Bodi na Bodi iliipuuza na kinyume chake
Mwanasheria huyo aliachishwa kazi.
Mheshimiwa
Spika, Taarifa hizi si za kweli na ni uongo uliokithiri
kwa aliyekuwa Mtumishi wa Umma kuudanganya umma wa Watanzania kwa kiasi cha
kutisha na Kamati inatoa taarifa ya uongo ndani ya Bunge.
Mheshimiwa
Spika, ukweli wa jambo hili ni kama ifuatavyo:
1. Mwanasheria
huyo Bw. Ngwilimi alileta ombi la kusafiri kwenda Malaysia kwa kumdanganya Mwajiri
wake kwa kudai kuwa alipewa ushauri wa kwenda Malaysia na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali. Katika barua ya kuomba ruhusa alisema kuwa alikuwa aende na Mwanasheria
Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliruhusiwa. Hata hivyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali haikutoa Ofisa huyo na hivyo kuamua kwenda peke yake.
2. Bw. Ngwilimi hakufukuzwa kazi na Bodi kama ilivyodaiwa
katika Taarifa ya kamati ya PAC katika ukurasa
wa 30, bali aliomba kuacha kazi mwenyewe kwa kutoa taarifa kwa Mkurugenzi
Mtendaji kwa barua ya yenye Kumb na. SEC.215/Conf/2/2014 ya tarehe 27 Februari,
2014 iliyokuwa inasomeka “Notice to
Terminate my Service with TANESCO” akitoa notisi ya siku 90 kwa mujibu wa Mkataba
wake wa kazi.
3. Katika ombi lake alidai kuwa anaacha kazi kwa hiari
yake mwenyewe kwa kuwa anahitaji kufanya shughuli nyingine na akaushukuru
uongozi wa TANESCO kwa ushirikiano kwa kipindi chote alichofanyakazi. Machi 10,
2014 Shirika lilimjibu Bw. Ngwilimi kwa barua yenye Kumb. Na. N.837 kuwa
Uongozi na Bodi ya TANESCO wamekubali ombi lake la kuacha kazi.
Mheshimiwa
Spika, kwa maelezo hayo ni wazi kuwa Bodi haikuwahi
kumfukuza na Bodi haikukataa utoaji wa fedha za IPTL katika Akaunti ya Escrow.
Badala yake Bodi ilielekeza IPTL ipewe fedha zilizopo kwenye Akaunti ya Escrow
tu na kwamba usuluhisho uliyofanyika unakubalika. Aidha, Bwana Ngwilimi aliamua kuacha kazi mwenyewe na kukimbia baada ya kuelewa
kuwa angechukuliwa hatua kutokana kumsingizia Mtumishi wa Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali kuwa walitumwa wote na kusafiri wote kwenda kufanya kile
alichodai due diligence.
No comments :
Post a Comment