NA WAANDISHI WETU
Wakati umma ukitarajia hayo kutoka kwenye hotuba ya rais kwa wazee wa Dar es Salaam, zimejiumba jumuiya ambazo hazijawahi kutokea nchini, moja ikijiita Jumuiya ya Wamachinga na nyingine Jumuiya ya Vijana Wanazuoni, kila moja ikipiga debe la kuwatetea watuhumiwa wakuu wa kashfa ya Escrow.
Wanaotetewa kwa nguvu zote huku wakimwagiwa sifa, ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakim Maswi. Utetezi kwa viongozi hao unajengwa kwenye hoja dhaifu kwamba wamehukumiwa na Bunge bila kusikilizwa na pia madai kwamba fedha zinazodaiwa kukwapuliwa siyo za umma.
JUMUIYA YA WAMACHINGA, WANAZUONI
Miongoni mwa jumuiya zilizoibuka na kutoa matamko yaliyotawala kwenye mijadala ya kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii ni pamoja na ile inayojiita kuwa ni Jumuiya ya Wafanyabiashara Ndogondogo Machinga; Jumuiya ya Wanazuoni Vijana na nyingine Jumuiya ya Wanazuoni wa Vyuo Vikuu Dodoma.
Katika mbinu hiyo ya kujaribu kuwaokoa watuhumiwa wa Escrow wakiwamo kina Muhongo, jumuiya hizo zimetoa matamko yanayojaribu kuonyesha kila hali kuwa Bunge halikuwa sahihi kutoa mapendekezo ya kutaka mamlaka ya uteuzi iwawajibishe viongozi mbalimbali waliohusika na uchotwaji wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutokana na msingi wa kutetea fedha za umma.
Aidha, mbinu nyingine zilizobainika ni pamoja na kutolewa kwa matamko mbalimbali ambayo baadhi yamekwenda mbali kiasi cha kudhalilisha maazimio ya Bunge yaliyotokana na taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyoegemea uchunguzi wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na taarifa za vyombo vingine mbalimbali vya umma ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katika taarifa iliyodaiwa kutolewa na mtu anayejitambulisha kuwa ni Katibu Mtendaji, jumuiya ijiitayo ya wanazuoni wa Dodoma imeenda mbali zaidi kwa kulidhalilisha Bunge, ikidai kwamba limejaa upuuzi na uzandiki na kwamba lilichofanya ni kutengeneza tuhuma na kisha kumtaka Rais Jakaya Kikwete awawajibishe kina Muhongo. "Kwa kuwa swala zima la Escrow limegubikwa na siasa, maslahi binafsi, chuki, wivu na kukomeshana, hivyo tunamuomba Rais asitekeleze azimio hata moja mpaka kwanza umma utakapoelezwa ukweli halisi wa mbivu na mbichi...," inasema sehemu ya mapendekezo ya jumuiya mojawapo iliyoibuka kuwatetea Muhongo, Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema kwa madai kwamba hawana kosa lolote.
“Sisi wanazuoni tunawajibu mkubwa wa kuitetea nchi na kuisemea pale tunapoona kuna jambo baya limefanyika, kwa kuwa uelevu wetu umetokana na kupata elimu bora iliyotokana na kodi za Watanzania wenzetu na hatupo tayari kuona mambo yakienda mrama,” imeeleza taarifa ya Jumuiya ijiitayo ya wanazuoni Dodoma. Jumuiya nyingine inayojiita ya Wafanyabiashara ndogondogo Wamchinga nayo pia imetoa utetezi kwa watuhumiwa wa Escrow.
Katika taarifa yao iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, imeeleza kuwa inayo mashaka makubwa juu ya namna uamuzi wa bunge ulivyopatikana,”
Taarifa hiyo imeeleza kuwa maamuzi ya Bunge siyo sahihi kwa sababu yana uonevu kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali na ni kivuli kikubwa cha chuki dhidi ya viongozi, hasa Muhongo.
Hata hivyo, wakati mbinu hizo za kuwatetea watuhumiwa kwa kutumia matamko yanayofikia kulidhalilisha Bunge, inaelezwa kuwa bado jitihada hizo hazielekei kufanikiwa kutokana na kile ambacho Watanzania tayari wameshakijua kutokana na ripoti ya CAG na pia taarifa ya uchunguzi wa PAC iliyojadiliwa bungeni kwa kina kabla ya kutolewa kwa maazimio manane yaliyoridhiwa kwa kauli moja na wabunge wa pande zote, yaani wa Chama Cha Mapinzudi (CCM) na wenzao wa kambi ya upinzani.
Mbali na viongozi wa wizara hiyo, wengine wanaotajwa kutaka kulindwa wasichukuliwe hatua ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof.Anna Tibaijuka na viongozi wengine waliotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika sakata hilo. Kadhalika, inaonekana kuwa mkakati wa kuwalinda viongozi hao ambao walitajwa kwenye maazimio ya Bunge yaliyotolewa wakati wa mkutano wa 16 na 17, unaonekena kuongezwa nguvu kutokana na kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na hivyo dhamira iliyopo sasa ni kutaka kuchukuliwa kuwa hatua pekee ya kujiuzulu kwa Werema inatosha hivyo wengine hawastahili kuchukuliwa hatua.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana kiliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa kinazo taarifa kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, wanataka kulindwa wasichukuliwe hatua licha ya kuwepo na maazimio yaliyotolewa na Bunge ya kutaka viongozi hao wawajibishwe.
“Habari tulizozipata kutoka ndani ya Ikulu kwenyewe zinasema kuna mpango wa kumlinda Muhongo na Maswi kwa kisingizio cha uchunguzi wa Ikulu,” alisema Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Arcado Ntagazwa.
Wakati hayo yote yakiendelea, Rais Kikwete leo atalihutubia Taifa kupitia kwa wazee wa Dar es Salaam. Hatua hiyo inafuatia taarifa ya kurugenzi ya mawasiliano ya rais Ikulu Desemba 9 kuwa kuanzia wiki iliyopita Rais angefanya maamuzi kuhusu kashfa ya Escrow.
Hata hivyo, wiki iliyopita Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alijiuzulu.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema huenda Rais Kikwete akatangaza hatma ya Mawaziri wawili waliotakiwa kuachia ngazi ambao ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Profesa Anna Tibaijuka, wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Bodi ya Shirika la Umeme (Tanesco), ambayo Bunge liliazimia ifutwe kwa kuwa rais anamteua mwenyekiti. Kadhalika, wadadisi hao wanaeleza kuwa Rais Kikwete anaweza kutangaza kuunda tume ya Kimahakama kuwachunguza majaji wawili waliotajwa kupokea mgawo kutoka kwa mfanyabiashara, James Rugemalila.
MAAZIMIO YA BUNGE
Maazimio kadhaa yalitolewa yakiwamo ya kuwawajibisha kwa kutengua uteuzi wa Profesa Muhongo, Maswi, Profesa Tibaijuka na Jaji Werema ambaye amejiuzulu mwenyewe. Wengine waliopendekezwa kuvuliwa uongozi wao kwenye kamati za Bunge ni Endrew Chenge (Bajeti), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini). Chenge akipewa Sh. bilioni 1.6 na Ngeleja Sh. milioni 40.2, kwa mujibu wa taarifa ya CAG na PAC.
Pia Bunge hilo liliazimia, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi kwa watu wote waliotajwa kuhusika na vitendo vyote vya jinai, kuhusu miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow, na watu wengine watakaogundulika baada ya uchunguzi mbalimbali unaondelea katika vitendo hivyo vya jinai.
Miongoni mwao ni mmiliki wa kampuni ya PAP, Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira wa VIP Engineering Ltd, Jaji Werema, Profesa Muhongo, Maswi, wajumbe wa Bodi ya Tanesco, ambao inasemwa kuwa walihusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha kufanyika kwa miamala haramu ya fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow kwenda PAP na VIP Engineering and Marketing Ltd.
Kuhusu ushiriki wa majaji katika kashfa hiyo, ni kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeweka utaratibu mahususi wa Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa nidhamu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Bunge liliazimia kushughulikia nidhamu ya majaji ambao kwa mujibu wa Katiba hiyo, unamtaka Rais aunde Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji.
Pia Bunge liliazimia serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi, na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.
Kadhalika Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
MAAMUZI YA JK KUHUSU ESCROW LEO
Wakati Rais Kikwete akitarajiwa kutoa maamuzi yake kuhusiana na maamuzi ya Bunge juu ya uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, kuna mambo kadhaa yanaelekea kumkabili.
Jambo mojawapo linalomkabili Rais Kikwete leo ni kuchukua maamuzi ambayo yatajibu kiu ya nchi wafadhili zinasosaidia bajeti ya serikali, baada ya kuzuia kutoa takribani Sh. trilioni moja kwa ajili ya kusaidia bajeti ya maendeleo ya mwaka wa fedha wa 2014/15 hadi watakapopata taarifa ya hatua zitakazochukuliwa na serikali juu ya uchotwaji wa fedha za Escrow.
Jambo jingine linalosubiri hukumu ya Rais Kikwete leo ni matarajio ya umma ya kutaka kuona uwajibikaji kwa vigogo wote wa serikali waliotajwa katika kashfa hiyo hasa baada ya ripoti ya uchunguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kusema wazi kuwa ndani ya fedha ambazo zilikuwa zimewekwa kwenye Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zilikuwako fedha za umma ndiyo maana hata Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikuwa inadai kiasi cha Sh. bilioni 21 kama kodi, lakini hazikulipwa.
Aidha, hotuba ya Rais Kikwete leo inatazamwa na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama tiba ya kejeli na kusakamwa kwa chama chao na Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwamba serikali yao inahusika na kashfa hiyo.
Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongozi uliofanyika Jumapili iliyopita, yemeonyesha kuzidi kuimarika kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, huku CCM ikiporomoka kwa kiwango kikubwa.
Kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa waliozungumza wiki hii juu ya uchanguzi huo, kuimarika kwa Ukawa kumeelezwa kuchangiwa pia na kashfa ya Escrow ambayo imeonekana kuwagusa viongozi serikalini, huku serikali ikitakiwa kuchukua hatua za kuwajibisha wahusika wote.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment