- Ahofia kukamatwa akirejea
- Vyombo vya Dola vyamwinda
MMILIKI wa kampuni ya IPTL, Harbinder Sethi Singh, ametoweka na vyombo vya usalama vimejiandaa kumkamata endapo atarejea nchini, Raia Mwema limeelezwa.
Singh ambaye kampuni yake ya Pan African Power Solutions (PAP) inadaiwa kununua umiliki wa kampuni ya kufua umeme ya IPTL katika mazingira yaliyozua utata, anadaiwa kuwa yupo nchini Kenya au Afrika ya Kusini.
Gazeti hili lilielezwa kwamba Singh aliondoka nchini siku chache kabla ya Bunge la Tanzania kutoa maazimio yaliyotaka wahusika wote wa makosa ya kijinai katika suala hilo wakamatwe na hatua za kisheria dhidi yao zichukuliwe.
Azimio namba moja la Bunge lilisema;….. “Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya Ulinzi na Usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na Taarifa Maalumu ya Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea”.
Raia Mwema limeelezwa kwamba Singh ambaye katika siku za nyuma alikuwa akipenda kufikia katika hoteli tofauti ikiwamo Sea Cliff ya jijini Dar es Salaam, sasa hayupo Dar es Salaam lakini anafuatilia kwa karibu yanayoendelea.
“Naweza kukuthibitishia kwamba Sethi hayupo nchini hivi sasa. Kwenye hili suala sitaki kuwa mzungumzaji wake lakini nafahamu kwamba aliondoka kabla ya Bunge kuazimia wahusike wakamatwe.
“Sasa kama alifanya hivyo kwa kujua hayo yanaweza kutokea mimi sijui. Siwezi pia kujibu swali lako la atakuja lini kwa sababu sijaambiwa. Hata hili la kukwambia kwamba hayupo nimekwambia kwa sababu tunafahamiana na sitaki kukudanganya,” alisema mmoja wa watu wafanyakazi wa Seth ambaye hata hivyo gazeti hili haliwezi kumtaka jina.
Mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege, ambaye pia ndiye msemaji wa kampuni hiyo, hakupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa maneno kupitia njia ya simu aliyoandikiwa na gazeti hili tangu juzi.
Hata hivyo, gazeti hili limeambiwa kwamba vyombo vya usalama vinafahamu Seth hayupo na vimejipanga kumkamata endapo atarejea nchini ili ajibu tuhuma zinazomkabili.
Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani, hakutaka kuthibitisha wala kukana kuhusu mpango wa taasisi hiyo kumkamata Singh, kwa maelezo kwamba kwa sasa yuko likizo na hana taarifa rasmi.
“Ningeshauri umtafute Mkurugenzi Mkuu, Dk. Edward Hoseah, ili akupe taarifa rasmi. Mimi niko likizo na hivyo sina taarifa zozote. Mkurugenzi anaweza kuwa na taarifa mpya zaidi,” alisema Kapwani.
Ingawa Seth ni mzaliwa wa Iringa, Tanzania, anaishi nchini Afrika Kusini ambako inaelezwa anafanya biashara; akitajwa kuwa mshirika muhimu wa kibiashara wa mtoto wa Rais mstaafu wa Kenya, Daniel Moi, aitwaye Gideon Moi.
“Hatuwezi kutangaza kwamba tutamkamata Singh. Hii itamfanya ajifiche huko aliko na asije. Wewe subiri arudi uone. Wengine waliopo hapa nchini ambao tutahitaji kuwakama tutawakamata tu. Ngoja kwanza tuanze naye huyo,” alisema mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina.
Nchini Kenya, Singh anafahamika kama mmoja wa wahusika katika ufisadi wa Goldenberg ambako yeye na baadhi ya wafanyabiashara kama Kamlesh Pattni na familia ya Moi walihusishwa nayo.
Katika kipindi cha wiki iliyopita, Singh amezungumza na baadhi ya vyombo vya habari vya hapa nchini ambapo katika mahojiano yake yote, amekataa kueleza alipo.
Baadhi ya tuhuma ambazo zinamkabili Singh moja kwa moja kutokana na maazimio ya Bunge ni madai ya kukwepa kulipa kodi, kughushi nyaraka na kutakatisha fedha haramu.
Chanzo cha habari cha gazeti hili kimeeleza kwamba Singh hana pa kukimbilia zaidi ya Kenya au Afrika Kusini ambako kimsingi ndiko kwenye biashara zake na makazi yake.
Singh alikwenda nchini Kenya kwenye miaka ya 1980 ambako alifanikiwa kujiingiza kwenye familia ya Moi na kutengeneza urafiki na baadhi ya wanasiasa wenye nguvu na ushawishi nchini humo kama Nicholas Biwott.
Mbali na IPTL, Singh tayari ameingia katika biashara ya kutafuta mafuta katika Visiwa vya Songosongo, eneo la Mnazi Bay, ambako yeye ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Hydrotanz ambayo inaendeshwa kwa ubia na kampuni ya Adhunik.
Suala la Singh limefika hapa kutokana na kazi ya uchunguzi iliyofanywa na Takukuru pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo iliwasilishwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo ilichambua taarifa hizo na kisha kuzipeleka bungeni.
PAC ilipendekeza Sethi akamatwe na kuhojiwa kutokana na tuhuma mbalimbali kama vile utakatishaji wa fedha, kukwepa kulipa kodi na udanganyifu lakini maazimio ya Bunge ndiyo yaliyojumuisha na wahusika wengine katika suala hilo.
Katika gazeti hili wiki iliyopita, iliripotiwa kwamba mtu wa karibu zaidi na Sethi hapa Tanzania kwa sasa anafahamika kwa jina la Rajiv Bhesania, ambaye jina lake limeonekana katika miamala iliyofanywa kupitia akaunti ya PAP ya Benki ya Stanbic ya hapa nchini ambayo inafanyiwa uchunguzi kwa sasa.
“Kama Serikali inataka kupata chochote kutoka kwa Sethi inabidi wambane huyuhuyu Rajiv Bhesania. Yeye ndiye kila kitu kwa Sethi hapa Tanzania. Hata akitaka mambo yake yanyooke mahali huwa anamtumia huyu.
“Nafahamu si rahisi kusema kila kitu lakini nafahamu kwamba kama vyombo vya ulinzi vitambana kisawasawa, anaweza kutoa siri zote za Sethi na hatimaye Watanzania wakapata wanachokitaka,” alisema mfanyakazi huyo wa IPTL.
Ni katika benki hiyo ndiko ambako muamala wenye thamani ya shilingi bilioni 73.5 ulifanyika siku ya Januari 23 mwaka huu; muamala ambao sasa ndio unachunguzwa na vyombo vya ulinzi.
Ripoti za CAG na Takukuru zilieleza kwamba kuna watu waliondoka katika ofisi za benki hiyo wakiwa na magunia yaliyojaa fedha.
“Kwa mujibu wa Takukuru baadhi ya watu walienda kugawana fedha kwenye Benki tajwa (Stanbic) wakiwa na mifuko ya rambo, sandarusi, maboksi, magunia na lumbesa,” ilisema sehemu ya ripoti iliyowasilishwa bungeni na PAC.
Muamala huo unachunguzwa vikali na Takukuru pamoja na ule wa Februari, 2014 katika Benki ya Mkombozi jijini Dar es Salaam ambapo kiasi cha shilingi bilioni 3.3 zinadaiwa pia kuchukuliwa kwa siku moja.
Habari hizi za Stanbic kuhusishwa na fedha za Escrow zimesababisha benki hiyo kumpa uhamisho aliyekuwa Meneja wake, Paul Omara, ambaye sasa anadaiwa kurejeshwa nchini Uganda.
Omara anaelezwa kuitumikia benki hiyo kwa muda wa miaka zaidi ya 11 na Raia Mwema limeelezwa kwamba ofisa huyo tayari amehojiwa na Takukuru kuhusu suala hilo kabla hajaondoka.
Mmoja wa maofisa wa Takukuru aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina kwa maelezo kwamba uchunguzi unaendelea, alisema wamepata ushirikiano mzuri kutoka Stanbic na kuna uwezekano kwamba “ watu watakula Krismasi wakati tayari Takukuru ikiwa imemaliza kazi”.
Suala la fedha za Escrow lililiteka Taifa wiki iliyopita na sasa wananchi wanasubiri kwa hamu hatua itakayochukuliwa na serikali kuhusu vigogo wanaotajwa kusaidia kutokea kwa kashfa hii.
No comments :
Post a Comment