KWA UFUPI
- Chama cha CUF kimeanza mkakati wa kuwania dola Zanzibar ikijiandaa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba.
- CUF yamwaga magari, pikipiki na wafuasi wapeperusha bendera ya Afro Shiraz
Z’bar/Dar. Chama cha Wananchi (CUF) jana kilionyesha jinsi kilivyojiandaa kwa “mwaka wa uamuzi” wakati kilipogawa vifaa mbalimbali vya kusimamia kuwezesha wanachama wake kusimamia Uchaguzi Mkuu katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya watu kwenye Uwanja wa Mnazi Mmoja.
CUF, moja ya vyama viwili vikubwa visiwani Zanzibar, iligawa magari kwa kila wilaya na kamati zilizoteuliwa kusimamia uchaguzi, pikipiki aina ya Vespa kwa majimbo yote 50 na katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad alisema lengo la mgawo huo ni kuutangazia umma kuwa “huu ni mwaka wa uamuzi”.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa Kamati za Uchaguzi za chama hicho kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Maalim Seif alisema safari ya uchaguzi tayari imeanza na CUF imejipanga vizuri kuliko chaguzi zote zilizopita na imeamua kutumia miezi minane iliyobakia kukamilisha mkakati wa ushindi.
Alisema kuzinduliwa kwa kamati hizo za Uchaguzi Mkuu ni kuanza safari ya Zanzibar kupata mamlaka kamili na kuongeza “hakuna kuremba ni kazi, kazi, kwa sababu Wazanzibar wanaitegemea CUF kuwakomboa”.
Alisema wamejipanga, wamejizatiti kwa kila hali wala hakuna kinachowatisha na azma ya kutimiza wanachokitaka itatimia kwa umoja wao.
CUF imekuwa ikitoa upinzani mkubwa katika kila uchaguzi tangu kurejeshwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi, na CCM imekuwa ikipata ushindi wa tofauti ndogo ambao mara zote umekuwa ukilalamikiwa, hali iliyosababisha vyama hivyo kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya machafuko kutokea mwaka 2005.
“Sitaki visingizio, nimewapa vitendea kazi; magari, pikipiki, mashine za kutolea nyaraka mbalimbali, mashine za matangazo (PA) sasa kafanyeni kazi huku mkiyakumbuka maazimio yetu ya mwaka huu ambayo ni kazi kwa kwenda mbele. Huu siyo mwaka 2005, wala 2010. Huu ni mwaka 2015, mwaka tofauti kwa chama chetu,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif, ambaye alihutubia kwa zaidi ya saa moja na nusu, aliamsha shangwe na vigeregere kutoka kwa watu waliohudhuria mkutano huo wa uzinduzi wakati aliposema kuwa wanaungana na tamko la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutoshiriki katika upigaji Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Katibu Mkuu huyo alisema kuwa katika kuhakikisha huu ni mwaka wa uamuzi na siyo wa uchaguzi, wananchi wa Zanzibar wasishiriki kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa kwa sababu siyo yao badala yake wajipange kuhakikisha Chama hicho kinashika dola.
“Wamepiga ngoma wenyewe, wamecheza wenyewe, tuwaache waipigie kura wenyewe. Katiba hiyo ni ya Dodoma na itabaki huko,” alisema Maalim Seif.
Alisema wananchi wamechoka kutawaliwa na utawala usio na upeo, dira, uadilifu, ubunifu, na mwelekeo, chama kisichojiamini, kinachoshindwa kusimama kidete kutetea masilahi ya Wazanzibari.
Alifafanua kuwa CUF ipo tayari na imejipanga kwa ajili ya kutetea masilahi ya wananchi wote, kufanya uamuzi ndani ya Zanzibar badala ya kufanyia Dodoma.
Alisema uongozi uliopo unaangalia maslahi yao badala ya wananchi, huku ukiweka mbele itikadi za kisiasa, badala ya kuangalia masilahi ya wananchi.
Huku akijihakikishia nafasi ya urais, Maalim alisema: “Kazi ya kwanza ya serikali ya awamu ya nane baada ya kuapishwa Rais na kuunda baraza lake la mawaziri, ni kuondoa kasoro zilizojitokeza wakati wa utawala CCM, ikiwamo vitendo vya ubaguzi.”
Salamu kwa CCM
Huku akiigiza kulia, Maalim Seif alisema kuwa salamu za chama hicho zimeifikia CCM na sasa wanalizana katika vikao vyao kwa kuwa wamechanganyikiwa na hivyo hawajitambui.
Alisema hivi sasa askari wote wanaotoka visiwani waliokuwa Bara wanarudishwa ili kukipa nguvu chama wakati wa uchaguzi.
Alisema dalili nyingine ya kuchanganyikiwa ni kukiunga mkono chama kipya (bila kukitaja) na kukitaka kisimamishe mgombe urais kwa gharama zao ili kuzigawa kura, lakini hilo haliwatishi.
Alisema kama CCM itashinda kihalali hawana tatizo , lakini isijidanganye kuwa itafanikiwa kuiba kura au kudanganya kwa namna yoyote ile.
Kuhusu Muungano, Maalim Seif alisema: “Hatuwezi kupata maendeleo kwa mfumo huo. Kila kitu kipo kwao, nchi kama Qatar na Uturuki walitaka ndege zao zifike Zanzibar zikakataliwa, lakini kama tungekuwa na mamlaka tungeangalia tunanufaika vipi likapitishwa hilo.”
Maalim alitumia muda mwingi kumsifu Waziri wa zamani wa SMZ, Mansour Yusuph Himid, ambaye amepewa jukumu la kumshauri Katibu Mkuu mkakati wa kufanikisha ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, akisema uamuzi huo umeongeza nguvu ya kuleta mabadiliko ya utawala na kuusimika uongozi.
Awali, Mansour alisema kuwa nyakati za kuburuzwa, kutoshirikishwa zimekwisha sasa kila Mzanzibari anataka Serikali yenye mamlaka kamili ambayo bila shaka italetwa na CUF.
Mshauri huyo wa Katibu Mkuu kabla ya kupanda kwenye membari na kuhutubia alicheza kuashiria furaha ya uzinduzi huo alisema kuwa wananchi wafanye maamuzi ya kuutoa utawala na kuweka viongozi katika uchaguzi wa mwaka huu.
Alisema kwa kufanya hivyo watajenga Zanzibar moja itakayompa uhuru Mzanzibari wa kujitawala na kujinasibu nayo badala ya sasa watu wanaogopana.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema yupo tayari kupoteza maisha kupigania masilahi ya Zanzibar.
Mazrui ambaye pia ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, alisema CUF ni chama kinachotokana na wananchi na kamwe hakitashiriki udalali wa kuiuza nchi katika himaya ya Tanganyika na itaendelea kupigania mamlaka kamili.
Mkutano huo ulitanguliwa na maandamano yaliyoanzia katika Uwanja wa Malindi na kupita Mtaa wa Darajani na kumalizikia katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Katika hatua nyingine CUF kimeendelea kupeperusha bendera ya zamani ya chama cha Afro Shiraz Party (ASP), ambacho kimefutwa kisheria baada ya kuungana na chama cha Tanu na kuzaliwa Chama cha Mapinduzi(CCM), Februari 5, 1977.
Bendera hiyo ya ASP ilipamba mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika jana kwenye uwanja wa Mnazi Mmoja ambako chama hicho kilikuwa kinazindua rasmi kamati za uchaguzi za chama hicho ambazo ni maalumu kwa ajili ya kushughulikia masuala yote yanayohusu uchaguzi mkuu ujao ikiwa ni pamoja na maandalizi.
Tofauti na ilivyozoeleka wafuasi wa chama hicho waliingia uwanjani hapo kwa makundi huku karibu kila mmoja akiwa amebeba bendera ya ASP, yenye rangi tatu za kijani, nyeusi na bluu bahari.
Kwa mujibu wa taarifa wafuasi wa CUF wameanza utaratibu wa kupeperusha bendera ya ASP kwa madai ya kuienzi Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), na pia kutanguliza uzanzibari kwanza.
Hata hivyo siku za karibuni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka aliiomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kukichukulia hatua za kisheria chama cha CUF kwa madai ya kupeperusha bendera ya zamani ya chama ASP kinyume na sheria namba 5 ya mwaka 1992.
Shaka alisema kwa mudu mrefu kumekuwa na ukiukaji huo wa sheria ukifanywa na viongozi wa CUF na wafuasi wake, wakipeperusha bendera yenye rangi ya ASP kwenye mikutano yao ya hadhara na kusema inatokana na CCM.
“Tunazitaka mamlaka za kidola na ofisi ya msajili hapa Zanzibar kukizuia chama cha CUF kiache kupeperusha bendera ya ASP, CUF hawana nasaba na ASP, asili yao ni ZNP, tumevumilia sasa hatutakubali tena dhihaka hiyo,” alisema Shaka.
.
No comments :
Post a Comment