Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, February 20, 2015

Mjumbe Baraza la Wawakilishi Z'bar afariki dunia ghafla.

Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Mnadhimu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Salmin Awadhi Salmin.
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, ambaye pia ni Mnadhimu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Salmin Awadhi Salmin, amefariki dunia baada ya kuugua ghafla.
  
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, amethibitisha kifo hicho kilichotokea jana, ambacho kimewashtua watu wengi visiwani hapa.
 
“Tulikuwa naye katika vikao leo (jana), lakini ghafla akaugua na kukimbizwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, ambako alifariki dunia majira ya saa saba mchana,” alisema Vuai kwa masikitiko.
 
Alisema mazishi yatafanyika leo kijijini kwa marehemu huko Makunduchi, mkoa wa Kusini Unguja.
 
Akimuelea marehemu, Vuai alisema alikuwa ni mtu muhimu ndani ya CCM kutokana na juhudi zake za kukiimarisha chama hicho.Kwa upande wake, Katibu wa Baraza hilo, Yahya Khamis Hamad, alisema ni pigo kubwa kwa baraza kwa sababu marehemu alikuwa mwakilishi hodari.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alisema kifo cha Salmini hakina utata, bali ni cha kawaida kwa kuwa mwili ulipelekwa hospitali na kupimwa na kukabidhiwa jamaa zake kwa ajili ya mazishi.
 
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amempelekea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Salmin, ambaye alikuwa pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Baraza hilo.
 
Salmin, ambaye alikuwa pia Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM katika Baraza hilo, alifariki dunia ghafla jana mchana, wakati akihudhuria kikao cha chama hicho kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Kisiwandui, mjini Zanzibar.
 
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, jijini Dar es Salaam jana, ilimnukuu Rais Kikwete akimwambia Rais Shein kuwa amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha ghafla cha Salmin, ambaye amejulishwa kuwa ameanguka ghafla wakati akihudhuria kikao mjini Zanzibar.
 
“Nimemjua Mheshimiwa Salmin kwa muda mrefu na hakuna shaka kuwa katika miaka 10 iliyopita tokea mwaka 2005 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia Baraza la Wawakilishi ameliwakilisha vizuri Jimbo lake la Magomeni na watu wake, na ameonyesha uongozi katika Baraza la Wawakilishi na kutoa mchango mkubwa katika chama chetu cha CCM. Tutaendelea kukosa mchango wake na busara zake za uongozi,” alisema Rais Kikwete.
 
Aliongeza: “Nakutumia Mheshimiwa Rais salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo hiki kikubwa. Aidha kupitia kwako, nawatumia salamu za rambirambi wananchi wa Magomeni ambao wamepoteza mwakilishi wao na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliopoteza mwenzao na kiongozi wao.”
 
“Kupitia kwako, vile vile, natuma pole nyingi sana kwa familia, ndugu na jamaa wa Mheshimiwa Salmin kwa kuondokewa na mhimili mkuu wa familia na mlezi. Wajulishe niko nao katika msiba huu mkubwa na kuwa msiba wao ni msiba wangu pia. Napenda pia uwajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyeji Mungu aiweke pema roho ya marehemu. Amen.”
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment